
Meshael Alayban
Mama mmoja ambaye ametajwa kuwa
mwana mfalme kutoka Saudi Arabia amekamatwa katika jimbo la California
nchini Marekani na kutuhumiwa kuhusika na ulanaguzi wa watu.
Meshael Alayban, 42, anakabiliwa na mashtaka ya
kumlazimisha mama mmoja kutoka Kenya kufanya kazi kwa zaidi ya masaa
kumi na sita kila siku, na kumlipa kiasi kidogo cha pesa kuliko
walivyokuwa wameafikiana.
Utawala wa eneo hilo, umesema kuwa Bi Alayban alichukua pasi ya kusafiria ya mama huyo, hatua iliyomfanya atoroke.
Mawakili wa mwana mfalme huyo wametaja kesi hiyo kuwa mzozo kuhusu hali ya utendaaji kazi.
Novemba mwaka uliopita, wapiga kura katika jimbo
la California, waliidhinisha sheria kali dhidi ya watu watakaopatikana
na hatia ya kuhusika na ulanguzi wa watu.
Ikiwa atapatikana na hatia, Bi Alayban, huenda
akahukumiwa kifungo cha miaka kumi na miwili gerezani, adhabau ambayo ni
asilimia mia moja zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya wapiga kura
kuidhinisha mageuzi sheria hiyo mpya.
Waendesha mashtaka wanasema Bi Alayban, ni mmoja
wa wake sita wa Mwana Mfalme Abdulrahman bin Nasser bin Abdulaziz
al-Saud, mmoja wa wanawe wa kiume wa familia moja ya kifalme nchini
Saudi Arabia.
Mtumwa
Mama huyo kutoka Kenya ambaye jina lake
halijatolewa, aliajiriwa na Bi Alayban miaka miwili iliyopita, baada ya
kusaini mkataba na shirika moja la kutoa uajiri nchini Saudia.
Mama huyo alihaidiwa kulipwa dola elfu moja mia sita kila mwezi na kuwa atafanya kazi masaa manane kila siku kwa siku tano.
Lakini, Bi Alayban amekuwa akimlipa dola mia
mbili ishirini kila mwezi na kulazimishwa kufanya kazi kwa zaidi ya
masaa kumi na sita kila siku.
Mama huyo kutoka Kenya vile vile amedai,
kupokonywa pasi yake ya kusafiria na alikabithiw muda mfupi tu kabla ya
wao kusafiri kwenda Carlifonia na Bi Alayban.
Akiwa California, alilazimishwa kufanya majukumu
mengi zaidi ya kinyumbani kwa familia ya watu wanane waliokuwa katika
vyumba vinne tofauti, ambako amedai alizuiliwa mateka.
Wakati alifanikiwa kutoroka, alisimamisha basi moja na kwenda moja kwa moja hadi kituo cha polisi.
Biu Alayban alikamatwa siku ya Jumatano na kufikishwa mahakamani siku ya Alhamisi.
Aliachiliwa huru kwa dhamani ya dola milioni tano na kuamriwa kurejesha pasi ya kusafiria ya amama huyo kutoka Kenya.
Aidha Bi Alayban sasa atavalia chombo maalum
ambacho kitatoa maelezo ya mahala aliko na hataruhusiwa kuondoka
Marekani hadi kesi hiyo itakapokamilika.
Viongozi wa Mashtaka walitaka jaji kumuachilia
kwa dhamani ya dola milioni Ishirini au anyimwe dhamana kwa kuwa yeye ni
tajiri mkubwa na aweza kutoweka.