Tuesday, August 6, 2013

Juhudi za amani zashika kasi Misri


Wafuasi wa Mohammed Morsi
Maseneta wawili wa Marekani John McCain na Lindsey Graham wamewasili mjiniCairo, wakati jitihada zikishika kasi kuutatua mzozo wa kisiasa nchini Misri uliozuka baada ya kupinduliwa rais aliyechaguliwa kidemokrasia Mohammed Morsi.
Wasiwasi unazidi kutanda baada ya serikali mpya inayoungwa mkono na jeshi kutangaza mpango mpya wa kuyasitisha maandamano, ambako wafuasi wa Morsi wanataka arudishwe madarakani.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na wageni mashuhuri wa kiimataifa wanaozuru Misri, wanaotarajia kusaidia kusimamia kupatikana suluhu ya amani katika hali ya suitofahamu iliopo kati ya wafuasi wa rais aliyepinduliwa na serikali inayoungwa mkono na jeshi.
Lakini mpaka sasa hakuna taarifa zaidi zimetolewa kuhusu hatua zilizopigwa.
Kwa wakati mmoja kulikuwa na ripoti kwamba baraza jipya la mawaziri lilikuwa tayari kuwaachia viongozi wa vuguvugu la Muslim Brotherhood kutoka gerezani na kuwapatia nyadhifa za mawaziri iwapo watasitisha maandamano mjini Cairo.
Hata hivyo mshauri wa rais amekana tuhuma hizo na wafuasi wa Morsi wamesisitiza hawatokubali chochote isipokuwa kurudishwa Morsi madarakani.

Kiongozi wa upinzani Burundi arejea nchini


Rwasa alitoroka Burundi baada ya uchaguzi wa mwaka 2010
 akihofia maisha yake
Kiongozi rasmi wa upinzani na zamani akiongoza waasi nchini Burundi Agathon Rwasa ametoka mafichoni baada ya miaka mitatu ya kuwa nje ya nchi.
Alikanusha madai kuwa alikuwa anaishi katika nchi ya kigeni muda huo wote na kusema kuwa atagombea uchaguzi wa mwaka 2015
Maafisa wa serikali walimzuia kuhutubia wafuasi wake wakisema kuwa hana ruhusa kufanya hivyo , na kwa hivyo akahutubia waandishi wa habari nyumbani kwake.
Bwana Rwasa alimaliza uasi wake mwaka 2009 lakini akatoweka kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010 kufanyika akisema alihofia maisha yake.
Uchaguzi huo ulikuwa wa pili kufanyika tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 12.
Aliambia BBC kuwa yeye anaunga mkono demokrasia hasa kwa kuwa uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika mwaka 2015.
"Wakati wa silaha umekwisha,'' alisema.
alikanusha ripoti kuwa alikimbia nchi jirani ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo, akisema kuwa muda wote alikuwa nchini Burundi.
Hata hivyo alisema kuwa angali ana wasiwasi kuhusu usalama wake.
Rais Pierre Nkurunziza na Bwana Rwasa waliongoza makundi ya waasii wa Kihutu waliokuwa wanapigana dhidi ya jeshi lililokuwa na watu wengi wa kabila la wa Tutsi waliokuwa wachache,wakati wa vita vya wenyewe kwa wnyewe vilivuosababisha vifo vya watu laki tatu.
Chama cha Rwasa cha FNL kilikataa kumaliza uasi wakati makundi mengine yaliyokuwa yanapigana kuungana na kuunda serikali ya muungano iliyofuatiwa na uchaguzi wa mwaka 2005.

Wednesday, July 31, 2013

UN yaamrisha M23 kusalimisha silaha


Waasi wa M23

Umoja wa Mataifa umewapa wapiganaji wa M23 walioko Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia
saa 48 kusalimisha silaha, la sivyo watakabiliwa kijeshi.
Kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa cha wanajeshi 3000 kitasaidiana na jeshi la Congo kuweka eneo la usalama mjini Goma.Kikosi hicho kimekubaliwa kutumia nguvu dhidi ya waasi wanaolaumiwa kwa kuwaua raia katika maeneo karibu na mji wa Goma.
Mapema mwezi huu mapigano kati ya M23 na jeshi la Congo yalizuka mashariki mwa nchi ambapo Umoja wa Mataifa ulilaumu waasi wa M23 kwa kuwaua kiholela raia katika eneo la Mutaho viungani mwa Goma.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa umewataka waasi wote na raia walioko Mashariki mwa Congo kusalimisha silaha walizonazo katika kambi ya jeshi la Umoja wa Mataifa ifikapo Alhamisi jioni.Onyo hilo limeongeza yeyote atakayepatikana na silaha atachukuliwa kuwa mpiganaji.
Hali ya usalama imeendelea kudorora Mashariki mwa nchi na onyo la sasa linanuia kuzuia waasi dhidi ya kukaribia mji wa Goma. Takriban watu 70,000 wamekimbia makwao, kufuatia mapigano kati ya jeshi na waasi. Umoja wa Mataifa unasema Wengi wamekimbilia nchi jirani ya Uganda.

Aliyekuwa Kiongozi wa zamani Mali aongoza kwa Kura


Ibarhim Boubakar Keita
Waziri Mkuu wa zamani nchini Mali Ibrahim Boubakar Keita anaongoza kwa kura za Urais, katika uchaguzi unaonuia kurejesha utawala wa demokrasia nchini humo. Duru za serikali zinasema aliyekua Waziri wa Fedha, Soumaila Cisse anafuata bw keita, huku thuluthi moja ya kura ikiwa imehesabiwa.
Upande wa Bw. Cisse imepinga matokeo hayo na kutaka tume ya kimataifa kuhesabu kura za uchaguzi huo wa Jumapili. Mali ilikumbwa na mapinduzi ya kijeshi mwaka jana pamoja na maasi Kaskazini mwa nchi. Ufaransa ilituma kikosi cha wanajeshi 4,000 kuyakomboa maeneo ya kaskazini kutoka kwa wanamgambo wa kiisilamu.
Vuguguvu la Ukombozi wa jamii ya Tuareg ikisaidiana na wapiganaji wa kiisilamu walitwaa eneo nzima la Kaskazini, kabla ya muungano huo kusambaratika. Makundi hayo yalifanikiwa kunyakua Kaskazini mwa nchi baada ya jeshi kuipindua serikali ya kiraia ikilalamikia kutopata ufadhili kukabiliana na maasi Kaskazini mwa nchi.
Mapema mwezi huu, kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kilitumwa Mali ili kusaidia katika shughuli za uchaguzi na kurejesha utawala wa kidemokrasia.Ufaransa umepongeza uchaguzi wa Mali, huku Muungano wa Ulaya ukisema shughuli hiyo ilifanyika bila visa vyovyote. Bw Keita maarufu kama "IBK" ana sifa ya kuwa na mabavu.
Mwanasiasa huyo aliendesha kampeini yake kwa ujumbe wa kurejesha hadhi kwa Mali akisema taifa liliisha hadhi yake kwa kuomba msaada wa Ufaransa ili kuinusuru dhidi ya kuporomoka.Viongozi wa kidini wengi wakiwa Waisilamu waliwaomba raia kumpigia kura, pia anaonekana kuungwa mkono na jeshi. Bw. Cisse aliunda chama cha Union for the Republic and Democracy (URD) mwaka wa 2003 na ametaka jeshi kutojihusisha na siasa.Jumla ya wagombea 27 walichuana Urais, huku watu milioni 6.8 wakijiandikisha kupiga kura nchini Mali.

Afya ya Mandela yaendelea kuimarika


Mandela alitaka sana kuona kuwa kombe la dunia 
linachezewa nchini humo
Rais mstaafu nchini Afrika Kusini , Nelson Mandela aliyelazwa hospitalini tangu tarehe nane mwezi Juni, anaonyesha dalili za afya yake kuimarika.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa serikali. Hata hivyo Mandela mwenye umri wa miaka 95 angali hali mahututi ambayo inadhibitiwa na madaktari.
Rais Jacob Zuma amewataka watu kuendelea kumuombea Mandela na kuwashukuru wale waliotenda mema kwa niaba ya Mandela.
Mandela ambaye ni rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa kidemokrasia, anatazamiwa na wengi kama baba wa taifa.
Alifungwa jela miaka 27 baada ya kuanzisha vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.
Anajulikana na ukoo wake kwa jina Madiba, na alichaguliwa kama rais wa Afrika Kusini mwaka 1994 baada ya wazungu kumaliza utawala wao na kisha akaondoka mamlakani baada ya miaka mitano ya kutawala nchi.
Katika taarifa yake, bwana Zuma alitoa wito kwa wafanyabiashara kuunga mkono mradi unaofadhiliwa na wakfu wa Mandela kujenga hospitali ya watoto.
"Madiba anapenda sana watoto, na anawatakia afya nzuri. Anatutaka tuhakikishe kuwa wanaishi maisha mazuri katika siku za baadaye,'' alisema Zuma.
Wakfu wa Mandela , ungependa kujenga hospitali yenye uwezo wa kuwashughulikia watoto 238 wa kulazwa pamoja na kuwatibu watoto kote nchini Afrika Kusini.

Thursday, July 18, 2013

AMISOM yakutana kuhusu kuchangia taarifa

 
Harakati za AMISOM Somalia
Ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia (Amison), kwa ushirikiano na wahisani wake, umeanza mkutano hii leo na washirika wake mjini Mombasa Pwani ya Kenya kuhusu kuchangia habari na taarifa muhimu.
Lengo la mkutano huo ni kubuni mpango utakaowezesha nchi zilizochangia wanajeshi kwa AMISOM kuchangia taarifa mara kwa mara kati ya Amisom, mashirika ya usalama nchini Somalia na mashirika mengine ya kikanda .
Mkutano huo wa siku tatu, umehudhuriwa na maafisa kutoka mashirika ya usalama nchini Somalia, viongiozi wa nchi zilizo na vikosi vyao nchini Somalia, waakilishi kutoka Ethiopia, Sudan Kusini, Mali, Chad, IGAD , AU na wengineo.
Akiongea wakati wa sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo, mjumbe maalum wa muungano wa Afrika nchini Somalia,Mahamat Saleh Annadif aliwakumbusha washirika kuwa vitendo vya kigaidi vinavyofanywa nchini humo havina mpaka.
Kwa hivyo, vita dhidi ya ugaidi lazima vifanywe kwa mpangilio unaofaa. Baada ya kukabiliwa na changamoto nyingi, kundi la Al-Shabab limeanza kubuni njia mbadala za kupambana na maadui wake kwa kukusanya taarifa za kijasusi.
Mkutano huu unatarajiwa kuangazia kwa kina hali inayokumba Somalia hususan vitendo vya kigaidi, uhalifu wa kupangwa na kuongezeka kwa idadi ya silaha ndogondogo
Pia unalenga kuimarisha miundo mbinu ili kuwezesha nchi kuchangia taarifa wakati wote pamoja na mengi mengineyo.

Mzee Nelson Mandela afikisha miaka 95

 
Leo ni siku ya kimataifa ya shujaa wa kupinga Ubaguzi wa Rangi Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela pia anaadhimisha siku ya kuzaliwa leo akitimiza miaka 95 akiwa bado amelazwa hospitalini.
Mandela amelazwa hospitalini kutokana na matatizo ya kupumua.
Serikali ya Afrika Kusini imewaomba wananchi wake kusaidia watu wasiojiweza na kutenda mema kama heshima kwa Madiba.
Rais Barack Obama alimtakia kila la heri Mandela anayetambulika kama shujaa wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Madiba anasalia hospitalini mjini Pretoria, lakini madaktari wake wamethibitisha kuwa afya yake inaendelea kuimarika.
Naye rais Jacob Zuma amemtakia kila la heri Mandela katika sherehe za siku ya kuzaliwa kwake.
Watoto kwenye shule kote nchini humo walitarajiwa kuanzisha sherehe hizo kwa kumuimbia Mandela wimbo wa kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake katika siku ambayo pia iliadhimishwa miaka kumi na mitano ya ndoa yake kwa mke wake wa tatu Graca Machel.
Mwanawe Mandela wa kike, Zindzi, alisema Jumatano kuwa afya ya Mandela imeimarika pakubwa na kwamba alimpata akiwa anatazama televisheni huku akiwasiliana kwa macho yake na mikono alipomzuru wiki jana.
''Nina matumaini kuwa atarejea nyumbani wakati wowote sasa'' Zinzi aliambia shirika la habari la Uingereza Sky News.
Siku ya kimataifa ya Mandela iliwekwa na umoja wa mataifa kama njia ya kumkumbuka mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel kwa juhudi zake za kupatanisha watu.
Mandela anasifika kote duniani kwa juhudi zake za kumaliza vita vya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Baadaye alichaguliwa kama rais wa kwanza mwafrika wa nchi hiyo mwaka 1994.
Chama cha kitaifa cha (ANC) kimesema kuwa katika siku hii ya kusherehekea siki ya kimataifa ya Mandela, ni heshima kwa miaka yake 95 kwa maisha yake aliyoishi vyema na ambayo ameitumia kupigania wananchi wa Afrika Kusini.