Monday, April 8, 2013

Kongamano la msaada kwa Darfur, Qatar

 8 Aprili, 2013 - Saa 11:08 GMT
Hali ya njaa katika Darfur
Taifa la kiarabu la Qatar ndio mwenyeji wa mkutano wa siku mbili kuhusu maendeleo na ukarabati katika jimbo la Darfur nchini Sudan.
Kongamano hilo linalenga kuchangisha dola bilioni 7.2 kama msaada wa maendeleo unaonuia kulifanya Darfur eneo la kujitegemea.
Kabla ya mkutano huo kufunguliwa rasmi, Uingereza ilitangaza kuwa itatoa kima cha pauni milioni 33.
Takriban watu 300,000 wanaaminika kufariki wakati wa mapigano ya mwongo mmoja katika jimbo hilo, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Wengine milioni 1.4 wanasalia kuwa wakimbizi.

Wakosoaji wanasema kuwa juhudi za kuleta amani katika jimbo hilo, zimehujumiwa kwani migogoro na migawanyiko haiishi katika jimbo hilo.
Maandamano yanayopinga kongamano hilo yalifanyika Darfur siku ya Ijumaa .
Wanaharakati wanasema kuwa maandamano yaliitishwa kwa sababu ukosefu wa usalama ulihujumu shughuli za ukarabati.
Pia wanasema kuwa wanapinga mkataba wa amani ulioafikiwa mwaka 2011 ambao ulitiwa saini nchini Qatar lakini ukakataliwa na makundi ya wapiganaji.
Hata hivyo, rasimu ya mkakati wa maendeleo, uliochapishwa kabla ya kuanza kwa mkutano, ulisema kuwa kucheleweshwa kwa shughuli hiyo utatatiza ukarabati.
Mgogoro katika jimbo la Darfur ulianza mwaka 2003 wakati waasi walipoanza kushambulia maslahi ya serikali na kutuhumu serikali ya Rais Bashir kwa kuwakandamiza waarabu weusi.
Kundi la wapiganaji wa kiarabu la Janjaweed lilituhumiwa kwa kuwaua waarabu weusi katika jimbo la Darfur
Ingawa ghasia katika jimbo hilo zimepungua, bado kuna makabiliano kati ya serikali na wanajeshi wa serikali, wapiganaji, wezi wa mifugo na makundi hasimu ya kikabila.
Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, anatakikana na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kwa mauaji ya kimbare katika jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment