Tuesday, May 7, 2013

Nane wakamatwa kuhusiana na shambulio mjini Arusha


ARUSHA
Watu wanane wakiwemo raia wa Saudi Arabia wamekamatwa nchini Tanzania, kuhusiana na shambulio lililofanyika dhidi ya Kanisa moja wakati wa ibada ya Jumapili jijini Arusha.

Tukio hilo la mripuko hadi sasa inasemekana watu watatu tayari wameuwawa na wengine kujeruhiwa.

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete ameliita shambulio hilo kuwa ni la kigaidi, lililofanywa na mtu au kundi la watu wakatili, ambao ni maadui wa nchi hiyo.
Watu wengine wasiopungua 30 walijeruhiwa katika shambulio hilo, ambalo ni la kwanza la ukubwa huo kulilenga kanisa.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo amesema wasaudi wanne waliokamatwa kuhusiana na shambulio hilo waliwasili katika uwanja wa ndege wa Arusha siku ya Jumamosi, na kwamba Watanzania wanne waliokamatwa ni wakristu, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Balozi wa Vatican nchini Tanzania Francisco Montecillo Padilla, alikuwa akihudhuria misa katika kanisa hilo ambalo limejengwa upya, lililoko katika viunga vya jiji la Arusha, lakini hakudhuriwa.
Maafisa bado hawajatoa ishara zozote kuhusiana na nani aliefanya shambulio hilo, lakini wasiwasi umekuwa ukiongezeka kati ya jamii za Wakristu na Waislamu katika miezi ya hivi karibuni.
Aidha Rais Kikwete ametowa wito kwa raia wa Tanzania kuwa watulivu wakati polisi ikiendelea na uchunguzi wake.

No comments:

Post a Comment