Wednesday, May 22, 2013

Wanajeshi wa Misri waachiliwa Sinai

 22 Mei, 2013

Magari ya jeshi katika rasi ya Sinai
Maafisa saba wa kikosi cha usalama cha Misri, waliokamatwa katika rasi ya sinai , wameachiliwa.
Maafisa wanasema kuwa wanaume hao waliokamatwa wakati wakisafiri kwa basi ndogo kuelekea Mashariki ya mji wa El Arish waliachiliwa na wako salama.
Kwenye ukurasa wake wa Facebook, msemaji wa jeshi alisema waliachiliwa kufuatia juhudi za jeshi kwa uwezo wa msaada wa kijasusi pamoja na viongozi wa kijamii.
Rasi hiyo imegeuka na kuwa hatari tangu aliyekuwa rais Hosni Mubarak kung'olewa mamlakani mwaka 2011.
Msemaji wa jeshi, Kanali Ahmed Ali, alisema kuwa wanaume hao saba walikuwa njiani kuelekea mjini Cairo.
Wanajeshi wa Misri walianzisha operesheni ya kuwasaka washukiwa wa utekaji nyara Jumanne.
Mnamo Jumatatu, rais alisema hakuwa tayari kuzungumza na waliofanya kitendo hicho akisema kuwa hana nafasi ya kuzungumza na wahalifu.
Utekaji nyara huo ulisababisha polisi waliokuwa na ghadhabu kufunga kivukio cha kuingia Gaza na Israel hadi mateka walipoachiliwa
Inatarajiwa kuwa kivukio cha Rafah kati ya Misri na Gaza kitafunguliwa Jumatano.
Haijulikani ni akina nani walikuwa wamewateka nyara maafisa hao, lakini ripoti zinasema kuwa huenda walikuwa wanamgambo wa kiisilamu.
Wanamgambo wa kiisilamu Kaskazini mwa Sinai, wamekuwa wakifanya uhalifu mipakani hasa kwa sababu ya ukosefu wa ulinzi thabiti kuweza kukabiliana nao.
Kumekuwa na matukio kadhaa ambapo watalii na wageni wengine wa kimataifa wametekwa nyara katika rasi hiyo.

No comments:

Post a Comment