Tuesday, May 7, 2013

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Aadan: Somalia iko wazi kwa biashara

Mwanamke wa kwanza wa Somalia kuwa Makamu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje Fowsiyo Yusuf Haji Aadan alizungumza na Sabahi kuhusu maendeleo yaliiyofikiwa na wizara yake tangu alipoingia ofisini mwezi wa Novemba iliyopita.
  • Waziri wa Uingereza kwa masuala ya Afrika Mark Simmonds akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Fowsiyo Yusuf Haji Aadan (kulia) akijibu maswali katika kilele cha mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa tarehe 25 Januari, 2013. [Na Jenny Vaughan/AFP] Waziri wa Uingereza kwa masuala ya Afrika Mark Simmonds akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Fowsiyo Yusuf Haji Aadan (kulia) akijibu maswali katika kilele cha mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa tarehe 25 Januari, 2013. [Na Jenny Vaughan/AFP]
Alielezea haja ya Somalia kujenga upya na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na majirani zake na kuzungumzia kuhusu matumaini yake katika mkutano wa London wa siku tatu juu ya Somalia, uliopangwa kuanza siku ya Jumanne (tarehe 7 Mei).
Aadan alisifia michango inayofanywa na jumuiya ya kimataifa kwa utulivu wa nchi, lakini alisema Somalia inapaswa kuongoza juhudi hizo ili ziweze kuwa endelevu.
Pia alikaribisha taarifa kutoka kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Pembe ya Afrika (IGAD) hapo tarehe 3 Mei ya kutambua haja ya kusaidiwa kwa uongozi wa serikali ya shirikisho ya Somalia katika mchakato wa kuleta utulivu, na kuutaja kuwa ni ushindi wa kidiplomasia kwa wizara yake.
Aadan alisema kuwa ujumbe ambao serikali yake inataka kufikisha kwa dunia ni rahisi: Somalia ni nchi huru na imefunguka upya kwa biashara.
Sabahi: Nini umuhimu wa taarifa ya IGAD kwa Somalia katika siku za usoni?
Fowsiyo Yusuf Haji Aadan: Huu ni uamuzi muhimu sana kwetu kwa sababu unairuhusu nchi kusimamia kwa uhuru utulivu wake wenyewe. Mpaka sasa, nchi za kigeni zilikuwa zinaendesha mpango wa utulizaji wa nchi yetu pamoja nasi, lakini tunaendelea mbele [tunaweza kuendesha] kama taifa huru.
Sabahi: Nini wajibu wa majeshi ya Kenya huko Kismayu? Je, kuna makubaliano baina ya Somalia na Kenya kuhusu juhudi za kuanzisha utawala wa mkoa kule?
Aadan: Kismayu ni sehemu ya Somalia. Kenya in amajeshi kule [kama sehemu ya Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia], lakini Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametuonesha kuwa anaunga mkono serikali ya Somalia katika kuchukua jukumu lake la kuongoza nchi. Marais wawili wamekutana mara nne na wanakubaliana kikamilifu katika masuala haya.
Sabahi: Kihistoria, kumekuwa na kutoelewana baina ya Somalia na majirani zake, wizara yako inafanya nini kubadilisha hilo?
Aadan: Tumeimarisha kweli uhusiano wetu na Kenya na Ethiopia. Tumekubaliana juu ya umuhimu wa nchi jirani kuishi pamoja kwa amani na mashirikiano. Mataifa ya Afrika kwa kweli yanastahili sifa zetu kwa sababu yanatusaidia kurejesha usalama katika Somalia.
Sabahi: Nini litakuwa lengo la Mkutano wa London kwa Somalia, uliopangwa kuanza tarehe 7 Mei?
Aadan: Mkutano huu umekusudiwa kulenga umakini wa dunia kwa Somalia. Tutajadili mfumo wa haki [wa Somalia], amani, jeshi la taifa na njia za kudhibiti mapato ya nchi.
Pia utahudhuriwa na wafanyabiashara wa Somalia na wa kigeni; tutawaonesha [fursa za] uwekezaji nchini.
Sabahi: Je, ni nini ujumbe wako kwa ulimwengu?
Aadan: Ujumbe wetu ni kuuambia ulimwengu kuwekeza nchini Somalia kwa sababu nchi hii itakuwa miongoni mwa nchi tajiri sana ulimwenguni ikiwa rasilimali zake zitatumiwa.
Tunao ufukwe mrefu zaidi barani Afrika, mifugo na pia uwezo wa nchi kimafuta na madini unaweza kutumiwa. Kwa hivyo ujumbe wetu ni: Njoo uwekeze katika nchi hii.
Sabahi: Unaweza kutuambia nini ingine kuhusu maendeleo ambayo wizara yako imefanya ukiwa madarakani?
Aadan: Kiasi cha mabalozi 20 wameteuliwa kuja Somalia katika miezi mitano iliyopita, wa karibuni wakiwa ni Balozi wa Uingereza kwa Somalia, pamoja na waziri wa mambo ya nje kupeperusha bendera ya Uingereza hapa [mjini Mogadishu].
[Serikali ya Somalia] imepata kutambuliwa na Marekani, na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, na kupata upya uanachama wetu katika mashirika hayo. Tuliondolewa kikwazo cha silaha na kujenga upya [asasi za] wizara ya mambo ya nje.
Sabahi: Baadhi ya watu wanashutumu uwepo wa Uturuki nchini Somalia. Nini jukumu lao katika Somalia?
Aadan: Uturuki haitaki kitu chochote maalumu kutoka Somalia. Wakati njaa ilipozuka mwaka jana, Uturuki ilisimama na Somalia. Waziri Mkuu wa Uturuki alitembelea Somalia pamoja na familia yake na raia wa Uturuki walitoa msaada wa mamilioni ya dola kwetu.
Wanajenga hospitali kubwa kabisa barani Afrika, wameanzisha shule ambazo zinafundisha kilimo na uvuvi, na wanajenga viwanda vingi. Kwa hivyo, hawana nia mbaya na sisi.
Sabahi: Somalia na Kenya zimechagua wanawake kuwa mawaziri wa mambo ya nje kwa mara ya kwanza, wewe unahisi nini juu ya jukumu la mwanamke katika uongozi wa sera za kigeni katika Afrika Mashariki?
Aadan: Niliwapongeza wote [Rais Uhuru] na [Waziri wa mambo ya Nje wa Kenya]Amina Mohamed Ni mwenendo ambao unapaswa kuigwa [katika kanda hii yote].
Katika miezi sita ambayo nimekaa ofisini, nimeonesha kuwa mwanamke anaweza kufanya vitu na amefanya mabadiliko makubwa katika sura ya sera ya nje ya Somalia. Ndege hawezi kuruka kwa bawa moja, kwa hivyo [katika jamii yenye mafanikio] wanaume na wanawake lazima wafanye kazi pamoja na ujuzi wa wanawake unapaswa kuchukuliwa kama fursa.

No comments:

Post a Comment