Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameiponda Serikali kwa kuwa na uchumi unaokua kwenye makaratasi wakati maisha ya wananchi yakiendelea kuwa magumu siku hadi siku.
Profesa Lipumba alisema hayo jana kwenye mkutano wa 18 wa mwaka wa Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini Tanzania (Repoa).
Akizungumza mbele ya Makamu wa Rais, Dk Mohamed Bilal, Profesa
Lipumba alisema uchumi wa Tanzania hivi sasa unakwenda kama mtoto
anayetambaa akiwa na watu wazima wanaokimbia.
“Tulikuwa na mipango mingi lakini isiyotekelezeka, tulielezwa ni
lazima tukimbie wakati wenzetu wanatembea, lakini badala ya kuongeza
mbio, sasa tunatambaa wakati nchi za wenzetu zinakimbia kwa kasi
kimaendeleo,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema ingawa uchumi unakua kwa asilimia saba kwa mwaka, lakini
ukuaji huo haulingani na maisha ya wananchi ambayo yanazidi kuwa magumu
siku hadi siku.
Profesa Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi, alisema sekta ya kilimo
ambayo inaajiri asilimia 75 ya wananchi inakuwa kwa asilimia 25.
“Unategemea nini kama sekta ambayo inawahusisha wananchi wengi,
lakini bado haijaboreshwa ili iwanufaishe,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema ingawa Serikali imekuwa na mipango mizuri, lakini imeshindwa
kuitekeleza hatua ambayo inawafanya wananchi wakate tamaa ya maisha.
Akitoa mfano, alisema kitendo cha kuwa na vipaumbele vingi wakati uwezo wa fedha ni mdogo ni kikwazo cha kuleta maendeleo.
“Hata kwenye bajeti zetu tumekuwa na vipaumbele vingi kiasi kwamba
hata kuvitekeleza inakuwa vigumu, tuchague vipaumbele vichache na
tuvifanyie kazi,” alisema Profesa Lipumba.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Dk Bilal alisema kukua kwa uchumi
unaowafikia wananchi ni mchakato ambao hauwezi kuja ghafla. Alisema
kitendo cha Serikali kutengeneza miundombinu ikiwamo barabara ni moja ya
juhudi zinazofanywa ili wananchi waweze kunufaika.
“ Ni kweli ukuaji wa uchumi haufanani na maisha ya wananchi wengi,
lakini hatua zinazochukuliwa na Serikali kama kujenga barabara, maji
,huduma za afya na elimu zinasaidia kukuza uchumi kwa watu walio wengi,”
alisema Dk Bilal.
No comments:
Post a Comment