Thursday, July 18, 2013

Mzee Nelson Mandela afikisha miaka 95

 
Leo ni siku ya kimataifa ya shujaa wa kupinga Ubaguzi wa Rangi Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela pia anaadhimisha siku ya kuzaliwa leo akitimiza miaka 95 akiwa bado amelazwa hospitalini.
Mandela amelazwa hospitalini kutokana na matatizo ya kupumua.
Serikali ya Afrika Kusini imewaomba wananchi wake kusaidia watu wasiojiweza na kutenda mema kama heshima kwa Madiba.
Rais Barack Obama alimtakia kila la heri Mandela anayetambulika kama shujaa wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Madiba anasalia hospitalini mjini Pretoria, lakini madaktari wake wamethibitisha kuwa afya yake inaendelea kuimarika.
Naye rais Jacob Zuma amemtakia kila la heri Mandela katika sherehe za siku ya kuzaliwa kwake.
Watoto kwenye shule kote nchini humo walitarajiwa kuanzisha sherehe hizo kwa kumuimbia Mandela wimbo wa kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake katika siku ambayo pia iliadhimishwa miaka kumi na mitano ya ndoa yake kwa mke wake wa tatu Graca Machel.
Mwanawe Mandela wa kike, Zindzi, alisema Jumatano kuwa afya ya Mandela imeimarika pakubwa na kwamba alimpata akiwa anatazama televisheni huku akiwasiliana kwa macho yake na mikono alipomzuru wiki jana.
''Nina matumaini kuwa atarejea nyumbani wakati wowote sasa'' Zinzi aliambia shirika la habari la Uingereza Sky News.
Siku ya kimataifa ya Mandela iliwekwa na umoja wa mataifa kama njia ya kumkumbuka mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel kwa juhudi zake za kupatanisha watu.
Mandela anasifika kote duniani kwa juhudi zake za kumaliza vita vya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Baadaye alichaguliwa kama rais wa kwanza mwafrika wa nchi hiyo mwaka 1994.
Chama cha kitaifa cha (ANC) kimesema kuwa katika siku hii ya kusherehekea siki ya kimataifa ya Mandela, ni heshima kwa miaka yake 95 kwa maisha yake aliyoishi vyema na ambayo ameitumia kupigania wananchi wa Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment