Friday, January 4, 2013

Yaliojijiri Mahakamani Vuga jana dhidi ya Viongozi wa Uamsho


Baadhi ya Viongozi wa Uamsho wakitoka Mahakamani kurudi Rumande


 
 
 
 
 
 
Rate This

Miongoni mwa Viongozi wa Uamsho walioendelea kukamatwa hivi karibuni ni Katibu wa Jumuiya hio ambae ni  Abdallah Said Ali (48)aliunganishwa  katika kesi inayowakabili viongozi wezake wanane wa Uamsho mjini Zanzibar.
Kiongozi huyo kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani jana na mwezake Fikirini Majaiiwa Fikirini (48) ambapo  walisomewa mashitaka manne likiwamo lile  la uharibifu wa mali pamoja na  kuhatarisha usalama wa Nchi.
Kabla ya Mwendesha Mashitaka, Rashid Abdallah  kusomewa mashitaka yao  aliwasilisha ombi mahakamani  hapo la kubadilisha hati ya mashitaka ili kutoa nafasi ya washtakiwa hao kuunganishwa na wenzao katika kesi hiyo.
Alidai kuwa washtakiwa hao wanadaiwa Oktoba 18, mwaka jana saa 6:00 mchana hadi usiku, katika sehemu mbalimbali za mji wa Zanzibar, walifanya vitendo vya uharibifu wa barabara, majengo na magari na kusababisha hasara isiopungua sh, Sh. milioni 500 kinyume na kifungu cha 3 (d) sura ya 47 cha Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 2002.
Mwendesha Mashitaka huyo alidai kuwa kwa muda tofauti, washtakiwa hao mnamo Mei 18 na Oktoba 19, mwaka jana, waliwahamasisha  na kushawishi watu kufanya makosa kutokana na mihadhara iliyofanyika viwanja vya Lumumba, Msumbiji na maeneo mengine tofauti.
Aidha alidai kwamba washtakiwa hao wanadaiwa kuwashawishi watu kuweka vizuizi yakiwamo mawe, magogo, matangi ya mafuta, kuharibu nyumba,  kusitisha huduma za jamii na kuathiri maslahi ya Taifa kinyume na kifungu cha 11 cha Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 2002.
Sambamba na hayo pia walidaiwa kula njama za  makusudi na kufanya makosa yaliosababisha  Sheikh Farid Hadi Ahmed, kujificha mwenyewe, kitendo ambacho kilisababisha uvunjifu wa amani hapa nchini kinyume na kifungu 399 cha Sheria namba 6 ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2004 ya Zanzibar.
Pamoja na hayo  mshtakiwa Azzan Khalid Hamdani, alisomewa shitaka kwa upande wake pekeakee la shambulio la matusi ya nguoni  kwa Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar kinyume na kifungu cha 74 (1) (d) cha Sheria namba 6 ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2004.
Mshtakiwa alidaiwa kuwa Oktoba 19, mwaka jana, saa 1:30 mchana, katika Msikiti wa Mbuyuni, alimtukana Kamishina huyo wakati akitoa mawaidha msikitini baada ya kutoweka kwa kiongozi wa Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed.
Washtakiwa hao ni Farid Hadi Ahmed (41), Mselem Ali Mselem (52), Mussa Juma Issa (37), Azan Khalid Hamdan (48), Suleiman Juma Suleiman (66), Khamis Ali Suleiman (59), Hassan Bakari Suleiman (39) na  Gharib Ahmada Omar (39).
Hata hivyo, Hakimu Kayange aliwataka washtakiwa kutojibu mashitaka dhidi yao hadi kesi yao itakapopangiwa Jaji na kusomewa mashitaka Mahakama Kuu.
Wakili wa washtakiwa hao, Abdallah Juma Mohamed, aliomba wateja wake wapatiwe dhamana akidai kuwa kwa kuzingatia makosa waliyosomewa, bado yanawapa haki ya kupata dhamana kwa sababu hayamo katika orodha ya makosa yasiyokuwa na dhamana.
Aidha, alidai kwamba wakati umefika kwa kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu haraka na kupangiwa Jaji kutokana na Mahakama ya Mkoa kukosa sifa za kisheria za kusikiliza kesi kama hiyo.
“Ombi langu kesi ihamishiwe haraka Mahakama Kuu na kupangiwa Jaji, kinachoonekana sasa wateja wangu wamekuwa kama wanaofungwa midomo, hawana hata haki ya kujibu mashitaka kama wanakubali au wanakataa,” alidai wakili huyo.
Hata hivyo, Mwanasheria wa serikali, Raya Mselem Issa, alidai kwamba Mahakama ya Mkoa haina uwezo wa kisheria wa kupokea maombi ya aina yoyote kuhusu kesi hiyo na kutoa maamuzi zaidi ya Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Alidai kuwa ombi la dhamana ya washtakiwa hao limewahi kuwasilishwa na kukataliwa na Marajis wa Mahakama Kuu kabla ya washtakiwa kufugua kesi ya kupinga kufungwa dhamana yao na kupewa huduma duni mahabusu.
Kesi iliyofunguliwa na viongozi hao wa Uamsho hata hivyo, ilitupwa na Jaji Mkusa Isack Sepetu, kwa maelezo kuwa ilifunguliwa kinyume cha sheria baada ya hati ya kiapo kukosa tarehe na jina la mtu aliyeitayarisha kwa niaba ya washtakiwa.
Hakimu Kayange alikubaliana na upande wa mashitaka kuhusu kufungwa kwa dhamana ya washtakiwa hao na kuwataka kuendelea kusubiri maamuzi ya  Mahakama Kuu kufuatia kesi waliofungua wakitaka Mahakama Kuu ifanye mapitio baada ya Mrajis kuwanyima dhamana.
Hakimu Kayange aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 14, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment