Saturday, December 22, 2012

MAKALA

UFAFANUZI WA HOTUBA YA UPOTOSHAJI YA MHE. ZITTO KABWE ALIYOITOA MAREKANI.

kabwe
UFAFANUZI WA MAMBO MBALIMBALI YALIYOPOTOSHWA NA MHE. ZITTO ZUBERI KABWE – NAIBU KATIBU MKUU WA CHADEMA KATIKA HOTUBA YAKE ALIYOITOA KWA WATANZANIA WAISHIO NCHINI MAREKANI

1.                KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA MPYA
Katika hotuba yake anadai kwamba mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea hivi sasa unatokana na shinikizo la CHADEMA, Asasi za kiraia na viongozi wa dini.
          UFAFANUZI
Huo ni upotoshaji mkubwa na wa wazi kabisa unaolenga kufuta historia sahihi ya mchakato wa uandikaji au upatikanaji wa Katiba Mpya unaoendelea hivi sasa.
Ni jambo lililo dhahiri kabisa kwamba mchakato wa Katiba Mpya ni utekelezaji wa hotuba ya Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyoitoa katika salamu za kuaga mwaka 2010 kukaribisha mwaka 2011 na baadaye katika sherehe za Chama Cha Mapinduzi kutimiza miaka 34 Mjini Dodoma.  Hili ndilo chimbuko halisi la hoja ya Katiba Mpya.
Akitoa maamuzi hayo alisema Katiba iliyopo sasa ni nzuri, imetuvusha salama miaka hamsini iliyopita, tukiwa wamoja, imetujengea umoja wa Kitaifa.  Lakini katika kipindi hicho hicho kumetokea mabadiliko mengi duniani na hapa nchini ya kisayansi, kiteknolojia, kitamaduni, kisiasa n.k.  Hakuna shaka kwamba sasa tunahitaji Katiba Mpya itakayotuvusha miaka mingine 50 ijayo.  Jambo hili Zitto Kabwe kalinukuu kwenye hotuba yake anaposema kuwa:-
“Tanzania tunayoitaka kwa miaka mingine hamsini ….” Mantiki hii ya miaka mingine 50 inatokana na hotuba ya Mhe. Dr. Jakaya M. Kikwete sio yeye.
2.                KUHUSU UBADHIRIFU SERIKALINI
Katika hotuba yake amedai kuwa CHADEMA ndio viongozi waliobeba dhamana ya mpito huu, kutoka Serikali ya kibadhirifu isiyojali watu mpaka Taifa lenye demokrasia iliyokomaa na lenye maendeleo na ustawi wa watu wake.  (Developmental Democratic State).
UFAFANUZI
Kwanza CHADEMA haina “dhamana” ya uongozi wa nchi, mwenye dhamana ya uongozi wa nchi ni Chama Cha Mapinduzi ambacho kina Rais ambaye ni Mkuu wa nchi, Mkuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.  CHADEMA wanachokitafuta ni Mob leadership ambayo ni fujo “Anarchy or law lessness” kitu ambacho huwezi kukidhibiti hata ukishika madaraka (mfano ni Libya, Mali, Algeria n.k.).
Mob leadership ni fujo kwa sababu ina watu ambao hawana sera ya pamoja hawana wajibu wa kisheria, hawana maslahi ya kijamii na kidini, wanadai haki bila wajibu.
Dhamana ya kuwafikisha watu katika Serikali ya kidemokrasia imo mikononi mwa Serikali iliyopo madarakani. Matamshi yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA yanaonyesha dhahiri kuwa hawathamini demokrasia ya nchi, umoja wa kitaifa wala amani na utulivu.
Mfano:-
(i)              Tamko la Mhe. Joshua Nassari la kumzuia Rais, Mkuu wa Nchi, asikanyage Mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania.
(ii)           Tamko la Mhe. Kabwe la kudai kuwa Wazanzibar wameporwa mafuta na gesi.
(iii)        Hata kwenye uchaguzi mdogo wa Mbeya vijijini mwaka 2009 CHADEMA ilitamka kwamba Mhe. Ali Hassan Mwinyi Rais Mstaafu asikanyage Mbeya.
(iv)        Tamko la Mhe. Wenje kuwa Mwanza inajitosheleza kuwa nchi kwa rasilimali zake na hivyo kupendekeza serikali za majimbo ili Mwanza ijiendeshe yenyewe.
Matamko haya hayawezi kutamkwa na kiongozi mmoja wa CHADEMA bila ridhaa ya Chama ama sivyo wangekuwa wanachukuliwa hatua na Chama chao.
Kwa kuwa matamshi haya ni uhaini, uchochezi na ufashisti (ANARCHY). Kauli hizi zinaweza kupelekea machafuko katika nchi, mgawanyiko, ubaguzi, fujo na umwagaji damu, mambo ambayo yatamwathiri kila raia wa Tanzania bila kujali Chama chake cha kisiasa.
Kwa hiyo, Chama Cha Mapinduzi ambacho kina dhamana ya uongozi wa nchi hii kinalaani matamshi hayo na kinawataka viongozi wa vyama vya siasa waache kutoa matamshi ya hovyo na hatari kwa mstakabali wa Taifa letu.  Chama Cha Mapinduzi kinaitaka Serikali kufuatilia matamshi haya kwa kina na itoe taarifa kwa wananchi.
3.                KUHUSU WATANZANIA KUTAKA UONGOZI MPYA
Katika utangulizi wa hotuba yake amedai kuwa “watanzania kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu wameamka na kutaka mabadiliko ya kisiasa na hasa kutaka kabisa uongozi mpya wa nchi kutoka Chama kingine tofauti na Chama kinachoongoza hivi sasa.”
UFAFANUZI
Chama kinachoongoza hivi sasa ni Chama Cha Mapinduzi “CCM” unapozungumza kauli kama hii lazima uangalie na hali halisi ya Chama chenyewe kama Taasisi.
Kwanza, Chama Cha Mapinduzi kina wanachama hai wengi ambao ni watanzania kuliko CHADEMA.
Pili, Chama Cha Mapinduzi kina mashabiki na wapenzi wastaarabu ambao ni watanzania wengi kuliko CHADEMA.
Tatu, Chama Cha Mapinduzi katika mfumo wake hakijapata ombwe la uongozi, kina uongozi katika ngazi za Shina, Tawi, Kata, Jimbo, Wilaya, Mkoa na Taifa na hao wote ni watanzania.  Na kama kuna Chama chenye heshima ya kuwasemea watanzania wote kila kona ni CCM sio Chama kingine chochote.
Nne, katika uchaguzi wa ndani ya Chama wa mwaka 2012, watanzania wameendelea kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi ndani ya CCM.  Mpaka sasa Mashina yamekwishafanya uchaguzi kwa asilimia 97.56.  Hao walioshiriki uchaguzi huo wa mashina ni watanzania.
Tano, katika chaguzi ndogo za Kata, Vijiji, Mitaa na Vitongoji CCM imeendelea kuongoza na wanaopiga kura nao ni wantanzania.
Sita, Chama Cha Mapinduzi tangu 2007 kimefanikiwa kufungua matawi yake nje ya nchi maeneo mbalimbali mfano India, Uingereza na Marekani.  Hao ni watanzania waishio katika ulimwengu wa kwanza na wanaamini kuwa CCM bado ni imara na hata Mhe. Rais alipoalikwa juzi kuhudhuria mkutano wa G8 alikutana na wanachama wa CCM Tawi la Marekani.  Kitendo cha Mhe. Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kualikwa G8 ni heshima kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi na Taifa  kwa kuwa kigezo cha kumwalika kilikuwa ni demokrasia, utawala bora, amani na utulivu nchini vigezo ambavyo vinavutia wawekezaji kutoka nje.
Kwa hiyo, hoja ya Mhe. Zitto ni Batili (futile) kwa sababu anatazama kwa macho ya ubinafsi kwa lengo la kugombea Urais mwaka 2015.
Uongozi mpya kabisa wa nchi ni upi?  Kwa kuwa uongozi wa nchi yoyote huru na ya kidemokrasia unapatikana kwa utaratibu wa uchaguzi wa kawaida unaozingatia Katiba na Sheria za nchi katika mazingira ya uhuru na uwazi na vyama vyote vinashiriki.  Afafanue maana ya uongozi mpya kabisa na namna utakavyopatikana huku akijua kabisa kwamba vyama vyote vya siasa vitakuwa na haki ya kushiriki uchaguzi.  Lazima utapata uongozi mchanganyiko kama ilivyo hivi sasa katika mfumo huu wa vyama vingi.
4.                KUHUSU SERA YA MADINI YA 2009 NA SHERIA YA MADINI YA 2010
Katika hotuba yake amedai kuwa Tanzania haina sera ya Gesi asili na kwamba, sheria ya madini ya mwaka 2010 imetokana na shinikizo la CHADEMA na Asasi za kiraia.
UFAFANUZI
Chama Cha Mapinduzi katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo inapatikana katika website ya CCM www.ccm.or.tz katika ibara ya 55 ya ilani imeeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya madini kwa kipindi cha 2005/2010, ambayo ni pamoja na kukamilika kwa sera ya madini ya 2009 na kupitishwa kwa sheria ya madini ya mwaka 2010.
Mhe. Kabwe mwaka 2009 alikuwa wapi kutoa mchango wake?
Hoja hii ni ya CCM yeye na Chama chake wameidandia kwa malengo ya kibinafsi na sio maslahi ya nchi.
5.                SUALA LA URAIA WA NCHI MBILI (DUAL CITIZENSHIP)
Mhe. Zitto anadai kwamba suala la uraia wa nchi mbili ni sera ya CHADEMA.
UFAFANUZI
Suala la uraia wa nchi mbili limekuwa ni sera ya Chama Cha Mapinduzi na limesimamiwa na Serikali yake, hususan Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe.
Katika hotuba ya bajeti ya 2011/2012 iliyotolewa na Mhe. Bernard Membe Bungeni katika Bunge la Nne kikao cha 31 cha tarehe 22 Julai, 2011 alisema:-
“Ni dhamira ya Wizara yangu kuona suala la uraia wa nchi mbili linazinduliwa sanjari na Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Watanzania mnapaswa kujua jinsi Zitto Kabwe anavyoiba hoja kwa manufaa binafsi alipowadanganya watanzania waishio nchini Marekani na dunia kwa ujumla akisema:-
“CHADEMA inataka suala hili lifikie mwisho kwenye mjadala wa Katiba.”
Huo ni uwongo mkubwa na uzushi, kwa kuwa dhamira hiyo ni ya Serikali ya CCM na ilishawasilishwa na Waziri mwenye dhamana Bungeni na yeye akiwepo.
6.      HALI YA UCHUMI WA NCHI
Amedai kuwa uchumi unaokuwa hivi sasa sio uchumi wa watanzania bali ni uchumi wa watu wachache kwenye sekta chache kama madini, mawasiliano na ujenzi; hivyo kupelekea watanzania wengi zaidi ya 15m kuishi chini ya Tshs. 500 kwa siku, kutokuwa na uhakika wa kula na kukabiliwa na mfumuko wa bei.
          UFAFANUZI
Kwanza, takwimu zake sio za kitafiti kwani hazionyeshi chanzo.  Pili hazina ulinganisho wa hali ya maisha ya wananchi wa nchi zinazotuzunguka ili uchungu alionao moyoni uonekane waziwazi kama ni kweli au ni uzushi.
Mhe. Kabwe amepotosha kwa makusudi ya kulinda maslahi binafsi ya Urais wa 2015 kwa kuwa haiingii akilini kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama takwimu hizo yeye hajazisoma.
Kwa mujibu wa kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2010 kilichotolewa na Wizara ya Fedha kukuwa kwa sekta ya kilimo kumeongezeka kwa 4.2% mwaka 2010 tofauti na asilimia 3.2% mwaka 2009.  Lakini katika taarifa yake anadai kuwa uchumi wa vijijini ambako ndiko kwenye kilimo umekuwa kwa asilimia moja tu (flat lining).
Katika uchambuzi wake wa hali ngumu ya uchumi na mfumuko wa bei kama angelinganisha na nchi jirani angegundua kuwa mfumuko wa bei kwa Tanzania upo chini zaidi kwa asilimia 19 ukilinganisha na nchi zinazotuzunguka ambao mfumuko ni mkubwa zaidi mfano Ethiopia ni 30%.
Katika hali halisi ya maisha ya watanzania wa vijijini chakula chao hakitokani na pesa, wanakula vitu vingi ambavyo haviingii kwenye takwimu za uchumi mfano, kuku, mayai, maziwa, mihogo, viazi vitamu, nyama n.k.  Hivyo vinaliwa bila kuingia kwenye mzunguko wa soko ndio maana hakuna mtanzania anayekufa njaa.  Lakini nchi jirani wanakufa njaa na wanakimbia nchi zao kwa njaa.  Mfumuko wa bei ni tatizo la Dunia nzima sio Tanzania peke yake.
Huyu ni mgombea Urais wa aina gani ambaye si mkweli kwa nchi yake, hasomi takwimu na anaropoka mambo ya ndani ya nchi hovyo hovyo duniani.
7.      SUALA LA FURSA YA ELIMU
Katika hotuba yake ameeleza kuwa “leo mtoto wa maskini Tanzania hapati elimu anayopata mtoto wa mwenye uwezo.” Na kwamba Tanzania ijiandae kupokea bomu litakaloletwa na kundi kubwa la vijana wasio na elimu wala ujuzi.”
UFAFANUZI
Huo ni uwongo na uzushi unaolenga kutetea maslahi binafsi.  Kwa kuwa katika uchambuzi wake amejikita kwenye shule binafsi na sio shule za serikali ambazo zipo katika vijiji vyote Tanzania, vinatoa elimu huru, sawa na bila ubaguzi.
Serikali ya Tanzania imetoa fursa ya Elimu kwa kila mtoto wa Tanzania tangu awali.  Mpaka imefikia wakati hata mabinti wa kazi za ndani (house girls) hawapatikani wote wapo mashuleni.
Kuthibitisha hilo mnamo tarehe 20/9/2010 Tanzania ilipata tuzo ya utekelezaji mzuri wa miradi ya Elimu katika ngazi za awali, elimu ya msingi na sekondari kutoka umoja wa mataifa.  Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokea Tuzo hizo Mjini New York.
Hivi huyu Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA anakuwa wapi asiyaone haya mpaka kwenda kuwadanganya watanzania waishio Marekani huko huko ilikotolewa Tuzo?
Serikali ya CCM imejenga Vyuo vya kutosha vinavyozalisha wasomi wa kutosha na hata bomu tunalojiandaa kulikabili ni la vijana wasomi ambao hawana ajira na sio vijana wasio na elimu kama anavyodai yeye.
IMETOLEWA NA TAWI LA CCM MAKAO MAKUU

DODOMA

Krismasi ina Ushahidi wa Biblia?

SWALI:
Mimi ni mkristo nimekuwa nikiwauliza viongozi wangu wa kiriho lakini sipati jibu lenye hoja, na wengine huniambia kuwa katika dini yetu kuna “DOGMA” mengine hayaulizwi, ila mimi nahitaji kujua ukweli ili niwe huru.

Swali langu ni hili” Je, Krismasi ina ushahidi wa kibiblia? na je ni kweli Yesu alizaliwa 25 Desemba? Santa Claus (Baba Krismas) ni nani? Je Yesu na wanafunzi wake walishawahi kusheherekea Krismasi? Pia kama mtanipa historia ya krismasi ntafarijika sana.
JIBU:
Asante sana, lifuatalo ni jibu la maswali yako:
Historia ya Krismasi
Wakati wa zama za kale, siku ya mwisho ya majira ya baridi huko sehemu za Kusini kulisherehekewa mfano wa usiku ambao mungu wa Mama Watakatifu alijifungua mtoto akijulikana kuwa ni mungu wa Jua. Pia (siku hii) inaitwa Yule, siku ambayo inasherehekewa mno kwa kurushwa pashpashi. Ambapo kila mtu atacheza na kuimba ili kuliamsha jua kutokana na usingizi wake mnono wa majira ya baridi.
Wakati wa Warumi, iliadhimishwa kwa kumsifu Satunusi (mungu wa mavuno) na Mithrasi (mungu wa kale wa nuru), huo ni mtindo wa kuabudia jua ambao umekuja ukitokea Syria hadi Urumi. Karne kabla ya madhehebu ya Sol Invictus, ilitangaza ya kwamba, majira hayo ya baridi sio ya milele, na kwamba maisha yanasonga mbele, na ni mualiko wa kubaki kwenye nguvu nzuri.
Siku ya mwisho ya majira ya baridi huko sehemu za mviringo za Kusini ni baina ya siku ya 20 au 22 Disemba. Warumi waliadhimisha Saturnalia baina ya tarehe 17 na 24 Disemba.
Wakristo wa kale
Ili kuepuka kuchunguzwa wakati wa sherehe ambazo ni za wapagani, Wakristo wa kale walikaa majumbani mwao pamoja na mtakatifu Saturnalia. Kwa vile idadi ya Wakristo iliongezeka na mila zao zikaenea, sherehe zikachukua shuruti za Kikristo. Lakini, Makanisa ya kale hakika hayakusherehekea mwezi wa Disemba kwa kuzaliwa Kristo hadi alipokuja Telesforusi Telesphorus, ambaye alikuwa askofu wa pili wa Roma kutoka mwaka 125 hadi 136 AD, askofu huyo ndiye aliyetangaza kwamba huduma za Kanisa zifanywe wakati huu ili kuadhimisha “Kuzaliwa kwa Bwana wetu na Mwokozi”. Hata hivyo, kwa vile hakuna mtu hata mmoja aliye na uhakika wa mwezi ambao amezaliwa Kristo, kawaida ya Uzawa ulikumbukwa Septemba, ambao ulikuwa ni wakati wa Sherehe za Kiyahudi za Trumpetsi (kwa sasa ni Rosh Hashanah). Ukweli ni kuwa, kwa zaidi ya miaka 300, watu walielewa kuzaliwa kwa Yesu katika tarehe tofauti.
Katika mwaka 274 AD, kikomo cha jua kiliangukia tarehe 25 Disemba. Mfalme wa Roma aitwaye Aurelian alitangaza tarehe hiyo kama ni “Natalis Solis Invicti”, ‘Sherehe Ya Kuzaliwa Jua Lisiloshindikana’. Katika mwaka 320 AD, Papa Julius I aliitangaza tarehe 25 Disemba kama ni tarehe rasmi ya kuzaliwa Yesu Kristo.
Mnamo mwaka 325 AD, Krismasi ilitangazwa rasmi, lakini kiujumla haikutiliwa maanani. Mtakatifu Constantine, ambaye ni Mfalme wa mwanzo wa dhehebu la Ukristo la Kirumi, aliitanguliza Krismasi kama ni sherehe isiohamishika kwa tarehe 25 Disemba. Pia aliitanguliza Jumapili kama ni siku kuu ndani ya siku saba za wiki, na aliitanguliza (Pasaka) kama ni sherehe yenye kuhamishika. Mnamo mwaka 354 AD, Askofu Liberius wa Rumi, alitoa amri rasmi kwa wafuasi wake kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu ndani ya tarehe 25 Disemba.
Hata hivyo, ingawa Constantine aliifanya rasmi tarehe 25 Disemba kama ni sherehe ya kuzaliwa Kristo, Wakristo wakiitambua kama ni tarehe ya sherehe iliyofanana na mapagani, hawakushiriki katika mambo mazuri (kwa siku hii) iliyopangwa na Askofu. Krismasi ilishindwa kupata utambulisho wa kilimwengu miongoni mwa Wakristo hadi kipindi cha hivi karibuni. Huko Uingereza England, Oliver Cromwell alizipiga marufuku sherehe za Krismasi baina ya miaka 1649 na 1660 kupitia kwa inayoitwa Sheria za Rangi Samawati Blue Laws, akiamini kwamba iwe ni siku ya kumuabudu mungu tu.
Hamu ya kuifurahia sherehe ya Krismasi ilikirimiwa pale Waprotestanto (Wakristo wasiokubali baadhi ya mafundisho ya Kanisa la Kirumi) walipokimbia uchunguzi kwa kutorokea sehemu za makoloni yote duniani. Hata hivyo, Krismasi bado haikuwa ni sikukuu halali hadi miaka ya 1800. Na, weka akilini, hakukuwa na picha ya Baba Krismasi (Santa Claus) kwa wakati huo.
Krismasi inaanza kuwa maarufu
Umaarufu wa Krismasi ulianza ghafla mnamo mwaka 1820 kutokana na kitabu cha Washington Irving The Keeping of Christmas at Bracebridge Hall ‘Kuiadhimisha Krismasi Kwenye Jukwaa La Bracebridge’. Mnamo mwaka 1834, Malkia wa Uingereza aitwaye Victoria, alimkaribisha mumewe wa Kijerumani Prince Albert ndani ya Ngome ya Windso Windsor Castle, akimuonesha tamaduni za mti wa Krismasi Christmas tree na Nyimbo Za Kumsifu Yesu Kristocarols ambazo ziliadhimishwa Uingereza kwa Mfalme wa Uingereza. Mwaka 1834, wiki moja kabla ya Krismasi, Charles Dickens alichapisha Nyimbo za Kumsifu Yesu za Krismasi Christmas Carols(ambapo aliandika kwamba Scrooge alimuamrisha Cratchit kufanya kazi, na kwamba Baraza Kuu la Marekani US Congress lilikutana Siku ya Krismasi). Ilikuja kuwa ni maarufu mno hadi kufikia kwamba sio makanisa wala serikali kukana umuhimu wa sherehe za Krismasi. Mnamo mwaka 1836, Alabama ilikuja kuwa ni taifa la mwanzo ndani ya Marekani kutangaza Krismasi kama sikukuu halali. Mnamo mwaka 1860, mfananishi illustrator wa Marekani aitwaye Thomas Nast alichukua kutoka hadithi za Kiingereza kuhusu Mtakatifu Nicholas, muangalizi mtakatifu wa watoto, kumtengeneza Baba Krismasi Father Christmas. Mwaka 1907, Oklahoma ilikuwa ni ya mwisho miongoni mwa mataifa ya Marekani kutangaza Krismasi kama ni sikukuu halali. Mwaka baada ya mwaka, nchi za dunia nzima zilianza kuitambua Krismasi kama ni siku ya kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu.
Nakuombea Krismasi Njema Have a merry Christmas
Leo, mambo mengi yasiyokuwa ya Kikristo yananasibishwa ndani ya Krismasi. Yesu alizaliwa mwezi wa Machi, bado siku yake ya kuzaliwa inasherehekewa Disemba ya 25, wakati wa solstice. Sherehe za Krismasi zinamalizikia siku kumi na mbili za Krismasi (Disemba 25 hadi Januari 6), ni idadi hiyo hiyo ya siku ambazo zilisherehekewa na wapagani wa ki-Rumi wakale kwa kuadhimisha kurudi kwa jua. Hivyo, hakuna mshangano wowote kwamba Wakristo waliosafi puritans – au Wakristo wasiotaka mabadilikoconservative – watahamaki kwa Krismasi kuwa “sio ya kidini kama ilivyotakikana kuwa,” wakisahau kwamba Krismasi haikusherehekewa hata kidogo hadi siku za hivi karibuni.
Yesu Alisemaje Kuhusu Krismasi?
Mazoea ya Krismasi
Mti ulio bora wa Krismasi unanunuliwa. Ukipambwa kwa madoido yenye kung’ara pamoja na kumetameta, unasimamishwa karibu na dirisha. Maduka yanajazana wanunuzi wakisaka zawadi na vile viduchu vinasubiri kwa hamu kubwa ya Baba Krismasi Santa.
Ni mshughuliko na ni homa ya Krismasi Christmas fever, umewahi kufikiri kabla? Je, Biblia au Yesu aliwahipo kusababisha homa ya Krismasi?Tafakari juu ya mchanganuo ufuatao kuhusu Krismasi, na ukweli utakuja kuwa wazi zaidi na zaidi.
Je, Krismasi Ina Ushahidi wa Biblia?
Neno ‘Krismasi’ halipo ndani ya Biblia. Biblia ilifunga midomo ya sherehe yote inayohusiana na Krismasi, isipokuwa kwa kitu kimoja; upambaji wa mti. Biblia wenyewe inashutumu upambaji wa miti (ya Krismasi):
“Mila za watu si chochote, wanakata mti kutokana na msitu, na mchongaji anauchonga kwa patasi yake, wanaupamba kwa fedha na dhahabu, wanaugandanisha kwa nyundo na misumari ili usipate kutikisika” (Jeremia 10-3,4).
Wazungu wa ki-Pagani kabla ya Ukristo, waliamini miujiza kwamba miti ya kijani ina nguvu maalum za ulinzi. Hakika, matumizi ya Miti ya Krismasi imeanza hivi karibuni tu mwa karne ya 17 hukoStrasbourg, Ufaransa na kutoka huko ukaenea hadi Ujerumani, Uingereza na baadaye Marekani. “Ibada ya miti ilikuwa ni jambo la kawaida kwa dini miongoni mwa watu wa Tyutoniki Teutonic na Skandinavia Scandinavia wa Ulaya ya kaskazini kabla ya kuingia kwenye Ukristo…Walowezi wa ki-Jerumani walileta mila za Mti wa Krismasi kwenye makoloni ya Kimarekani mnamo karne ya 17. Kufikia karne ya 19, matumizi yake yalienea sehemu tofauti”. (Angalia Encyclopedia ya Compton, Toleo la 1998)
Je, Yesu Alizaliwa Disemba ya 25?Si tarehe ya Disemba 25 wala tarehe nyengine yoyote iliyotajwa ndani ya Biblia kuhusu kuzaliwa kwa Yesu. Ilikuwa ni hivyo hadi kufikia mwaka 530 C.E kwamba mtawa monk aitwaye Dionysus Exigus, aliweka tarehe isiyobadilika ya kuzaliwa kwa Yesu kuwa ni Disemba 25. “Kulingana na taratibu za ki-Roma, alikosea kuipanga tarehe ya kuzaliwa kwa Kristo (yaani, miaka 754 baada ya kupatikana nchi ya Rumi) kama ni Disemba 25, mwaka 753”. (Angalia: Encyclopedia Britannica, toleo la mwaka 1998) Tarehe hii ilichaguliwa ili iendane pamoja na sikukuu ambazo zimeshagandana na imani za kipagani.
Mapagani wa Kirumi walisherehekea Disemba 25 kama ni ya kuzaliwa kwa ‘mungu’ wao wa nuru, aitwaye Mithra.
“Mnamo karne ya pili A.D, hiyo sherehe ya Mithra ilikuwa ni ya kawaida zaidi ndani ya Ufalme wa Rumi kuliko Ukristo, ambayo ilizaa mifanano iliyo mingi” (The Concise Columbia Encyclopedia, toleo la mwaka 1995).
‘Waungu’ wengine wakipagani waliozaliwa Disemba ya 25 ni: Hercules mtoto wa Zeuz (Wagiriki); Bacchus, ‘mungu’ wa mvinyo (Warumi); Adonis, ‘mungu’ wa Kigiriki, na ‘mungu’ Freyr wa Ugiriki-mapagani wa Roma.
 Je, Vipi Kuhusu Baba Krismasi Santa Claus?
Kama viumbe visivyokuwa binaadamu aliens watafika duniani katika wakati wa Krismasi, bila ya shaka wataamini Krismasi kuwa ni sherehe ya kufurahikia kuzaliwa kwa Baba Krismasi Santa. Majina ya ‘Santa Claus’, hayamo popote ndani ya Biblia.
Hata hivyo, Mtakatifu Nikolas Saint Nicholas (Baba Krismasi Santa Claus) alikuwa ni mtu halisi, askofu, ambaye alizaliwa miaka 300 baada ya Yesu. Kwa mujibu wa hekaya za kale, alikuwa ni mtu mwenye huruma mno na alitenga nyakati za usiku kwenda kutoa zawadi kwa mafukara. Baada ya kifo chake mnamo Disemba ya 6, watoto wa shule huko Ulaya walianza kusherehekea siku hiyo kwa karamu kila mwaka.
Baadaye Malkia Victoria aliibadilisha sherehe hiyo kutoka Disemba ya 6 kuwa ni Disemba ya 24 kuamkia Krismasi.
Je, Yesu au Wafuasi Wake Waliwahi Kusherehekea Krismasi?Kama Yesu alimaanisha kwa wafuasi wake kusherehekea Krismasi, angeliifanyia kazi yeye mwenyewe na kujikusanya pamoja na wafuasi wake. Hakuna sehemu iliyotajwa ndani ya Biblia kwamba kuna mfuasi yeyote aliyewahi kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu kama Wakristo wanavyofanya leo.
“Kanisa halikupatapo kuweka sikukuu kwa ajili ya sherehe za tukio la Krismasi hadi ilipofika karne ya 4” (Angalia: Encyclopedia ya Grolier)
Hivyo, tunaona kwamba sio Biblia wala Yesu na wafuasi wake waliosema kitu kuhusu sherehe za Krismasi ambazo sasa zinahusisha viingilio vya sherehe, biashara, na matumizi yaliyochupa mpaka, ni utovu wa akili kwa mfananisho wowote wa imani.
MWISHO
@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@
IKIWA VIONGOZI WANALIA RUSHWA WANANCHI WAFANYE NINI
KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sura ya kwanza, sehemu ya tatu, inaeleza kuwa binadamu wote wanastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wao.
Sheria zetu hizi zimemtukuza binadamu kama ilivyo kwenye vitabu vya dini. Binadamu akapewa mamlaka ya kutawala vyote vilivyomo duniani.
Tukawa na Bunge, Mahakama na Dola. Tukajiwekea sheria zetu ndani ya katiba yetu kwa kujali ubinadamu wetu.
Tukasema kila mmoja ana haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu na matokeo ya kila kitu kutekeleza wajibu wake kwa jamii kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 12 na 16 ya katiba.
Kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma.
Kuna misingi miwili ya kiuongozi, kwanza ni mtendaji, uwezo wa kutenda. Bila kuwa na uwezo huo wa kutenda, huwezi kuwa kiongozi. Utendaji ni hatua ya uongozi, hii ni hatua ya mwanzo ya kiongozi kuwa mtendaji.
Hatua ya pili ya uongozi ni utumishi, hapa unatakiwa uwe mtu unayetenda mambo kwa manufaa ya jumuia, utendaji wa kiongozi ni wa kihuduma.
Uongozi wake haupimiki kwa kutazama kiasi cha huduma anazotoa na namna anavyotoa huduma hizo kwa manufaa ya utendaji wake.
Kiongozi ambaye kazi yake ni kutekeleza malengo ya jamii husika, kufikia malengo yake ni lazima awe kinyume na vikwazo vya maendeleo ya jamii, vinginevyo atasababisha jamii husika kutofikiwa na malengo yao.
Kiongozi akiwa kinyume na matarajio yaliyokusudiwa na jamii husika kwa dhamira yake binafsi, atasababisha jamii kukata tamaa iwe kisiasa, kiuchumi (maendeleo ya kiuchumi).
Jamii yetu ijihadhari na viongozi walio na mwelekeo au kusababisha vikwazo katika kuleta maendeleo, hasa rushwa.
Rushwa ni kitu chochote kinachotolewa kinyume na sheria ili kupata huduma, utumiaji mbaya wa madaraka kwa mtumishi wa umma ili kujinufaisha. Rushwa inaweza kuleta madhara makubwa kwa mtu mmoja mmoja au kwa umma.
Mambo yanayoweza kusababisha rushwa ni ‘mishahara’ midogo kwa wafanyakazi wa serikali na taasisi zingine. Mfanyakazi analazimika kupokea rushwa ili kukabiliana na hali ya maisha, kwani gharama ya maisha ipo juu, wakati malipo hayakidhi haja.
Vyama vyetu vina ilani tu ya kuzuia rushwa, lakini hakuna mikakati ya kuimaliza.
Watu wenye mamlaka ya kutoa maamuzi, husababisha rushwa katika nafasi zao walizonazo kwa namna moja au nyingine kwa kutumia huduma kuanzia ngazi ya familia hadi taifa wakiwa kinyume na maadili tuliyojiwekea.
Elimu ndogo kwa wananchi juu ya haki zao, watu kutumia njia ya mkato kukamilisha mambo na kutatua matatizo yao, nidhamu duni miongoni mwa wafanyakazi, mmomonyoko wa maadili miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma pia ni athari ya rushwa.
Kwa ujumla, rushwa inaleta athari kubwa sana katika jamii, kwa mtu mmoja mmoja au taifa kwa ujumla.
Rushwa huleta madhara au athari kubwa kwa utekelezaji wa majukumu ya serikali na jamii kwa ujumla, kukosekana kwa haki inayotokana na maamuzi ya upendeleo, kuzuka kwa matabaka ya wenye pesa na wasio na pesa, wananchi kukosa imani na serikali yao.
Pia husababisha vifo; mfano wagonjwa hospitali, wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kukosa imani na vyombo husika kama polisi.
Rushwa husababisha pia kushuka kwa pato la taifa na kuingia gharama zisizo za lazima katika miradi mbalimbali, hatimaye serikali kushindwa kutoa huduma zinazostahili kwa wananchi, na pia husababisha uonevu kuongezeka mfano dawa za kulevya, ubakaji.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilianzishwa baada ya Bunge kuifanyia marekebisho sheria ya kuzuia rushwa ya 1971 kabla kufanya marekebisho mengine katika sheria hiyo mwaka 1991.
Taasisi hiyo inashirikiana na vyombo vya dola; Jeshi la Polisi, Mahakama, Idara ya Usalama wa Taifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, na idara nyingine.
Rushwa ikishaingia katika jamii kwa kutekeleza majukumu yao husababisha ubadhilifu na uvujaji wa mali za umma.
Watu hushirikiana kusaidia vitendo viovu kwa mamlaka waliyopewa kwa manufaa yao, kula njama na matumizi mabaya ya mamlaka, kutumia ushawishi wao kwa lengo la kuwapatia manufaa yasiyo halali kutoka kwa mamlaka ya umma na uhamishaji wa mapato ya rushwa.
Viongozi wanapaswa kufuata maadili yao waliyojiwekea katika katiba kwa kukubali uongozi wao mbele ya umma wa Watanzania.
Rushwa huzaa mambo mengi katika jamii kwa kutoelewana kuwa ni halali kutoa rushwa. Rushwa huzaa mambo ya takrima na ufisadi katika jamii ikiwa ni pamoja na kulangua, kuchakachua ili mradi malengo yanafikiwa bila kujali utu wa mtu mwingine.
Tulio na mamlaka tufuate katiba ya nchi na kuwasaidia Watanzania, tutoe huduma bora kwa umma bila ubaguzi na kudhulumu haki ya wale wanaoongozwa.
Unaweza kufika mahali ukajiuliza, kama kongozi mkuu wa nchi analia, wabunge wanalia, wananchi wanalalamika, nani anayepasa kubeba jukumu la kuwakomboa wananchi na rushwa?
CHANZO TANZANIA DAIMA.
MWISHO
@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@

La Uamsho na ukimya wetu – 2

DSCF2002
Wiki iliyopita nilisema kwamba haistahiki kunyamaza kimya dhidi ya yale yanayoendelea kuwakumba viongozi wa Uamsho, ambao kwa zaidi ya mwezi sasa wametupwa ndani na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakishitakiwa kwa makosa kadhaa wa kadha. Hilo, hapana shaka, halihusiani kabisa na kuingilia uwezo na uhuru wa mahakama ya Zanzibar kufanya kazi zake.
Na hili la kusema hivi pia halimaanishi kuwa ninaamini uwezo na uhuru huo wa mahakama unaweza kuathiriwa kwa namna yoyote ile, maana sio tu kwamba sitaki uathirike, bali zaidi sijashawishika na uadilifu wake.
Msimamo wangu ni kwamba kinachowakabili viongozi wa Uamsho ni kesi ya kisiasa zaidi kuliko kuwa kesi ya uhalifu, na ndio maana mwenendo mzima wa kesi hii, kwa jicho la sisi wengine, unakwenda kisiasasiasa tu. Ni siasa iliyohalifishwa, kwa maana ya kwamba ni msimamo wa kisiasa wa viongozi wa Uamsho ndio uliogeuzwa uwe uhalifu.
Hili la kuihalifisha siasa, hata hivyo, najua linapingwa na waungaji mkono wa hatua hizi za serikali dhidi ya Uamsho hivi sasa, kwa hoja kwamba sisi tunaoiangalia kesi hii kwa jicho hilo ndio ambao tumeusiasisha uhalifu, yaani tunalazimisha kuichukulia kesi ya uhalifu kuwa ya kisiasa ili kupata muradi wetu! Ni uhalifu gani wa viongozi hawa? Nilitaja kuwa ni uchochezi, fujo, uharibifu wa mali na matusi, kwa kutaja machache!
Wawache wenye msimamo wao dhidi ya Uamsho wawe nao, na kwa sababu sambamba na msimamo huo wana pia na nguvu za dola – polisi, mahakama, jela na pingu; basi wawache pia wazitumie nguvu hizo kuthibitisha msimamo wao.
Lakini nasi tuongozwe na nguvu ya dhamira zetu kukataa. Kukataa kukaa kimya. Kukataa kuwauwa viongozi hawa. Kukataa kuiua dhamira ya Zanzibar kusonga mbele kama taifa. Tukatae kuiua heshima ya kuwa watu!
Na hapa ninataka kuweka sawa hilo, ili tunapoinuka sisi tunaowatetea viongozi wa Uamsho, tuinuke tukiwa tunajiamini licha ya ukweli kwamba tunaweza kunasibishwa na uovu wanaotupiwa wao. Tusije tukaingia kwenye mtego tukanasa. Nasema hivi kwa sababu nimesikia kwamba jamii ya Waislamu Zanzibar imetoa tamko la kutaka viongozi wa Uamsho watolewe hima, ama sivyo litatokea la kutokea.
Hapana. Mimi napingana na hilo. Mitego ya kuwanasisha wenye dhamira njema na nchi imeshategwa mingi huko nyuma. Na kila tuliponasa, ndipo wenye dhamira mbaya na nchi wakapata kujipenyeza. Wakavunja maduka. Wakaiba mali. Wakapiga watu. Wakaingia kwenye nyumba za ibada kuziharibu. Mwisho, kwa kuwa wao ndio wenye nguvu hizo za kuharibu lakini pia na taasisi za kidola za kusimamia misimamo yao, leo hii akina Sheikh Farid wapo walipo! Kizuizini!
Hilo linawezekana kabisa kujirudia. Taarifa iliyowahi kusambazwa mitandaoni wakati ule wa kutoweka kwa Sheikh Farid ilithibitisha kwamba kitendo kile kilipangwa na kupikwa makusudi ili fujo itokee, halafu wapangaji wapate kutimiza muradi wao. Hakuna sababu kwa nini iwe sasa hilo pia halijapangwa tena.
Ninarudia. Tusimame na viongozi wa Uamsho. Tusikubali kumeza uozo wanaotupiwa. Tuyasafishe majina yao. Tuwape nafasi wanazostahiki kama viongozi wanaopigania ukombozi wa nchi yao. Lakini tusinase kwenye mitego mingine.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano wa Tanzania zinajua fika kwamba kinachosimamiwa na Uamsho ni kitu gani hasa – wanaupinga mfumo uliopo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Uamsho wanataka mahusiano tafauti baina ya pande hizi mbili za Muungano kwa sababu ambazo wamezieleza waziwazi kwenye mihadhara yao waliyoifanya kila sehemu Zanzibar. Wameweka kila kitu wazi kwa mtu yeyote kukiona. Na ni hicho, kwa hakika, ndicho kilichowafanya viongozi hao kuwa “wahalifu”.
Tusizipe nafasi serikali hizi mbili kuiviza safari ya Zanzibar kuelekea kwenye mamlaka kamili ya kujitawala na kujiamulia hatima yake.
MWISHO
@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@

Prof. Sarungi, Muungano hautasimama kwa nguvu za kijeshi

KAULI ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Prof. Phelomon Sarungi,kwamba Jeshi la Wananchi wa Tanzania halitawavumilia wale wote wenye lengo la kuuvunja Muungano inatisha. Nasisitiza matumizi ya neno ‘kutisha’ maana ni neno hilo hasa ndilo ninalokusudia kulitumia katika makala hii.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi la tarehe 22 Agosti, 2004, Prof. Sarungi alisema kuwa Muungano na JWTZ ni watoto pacha, kwa hivyo Jeshi (ambalo hapa litakuwa ni Kurwa) halitavumilia kuona Muungano (Doto) unahatarishwa. Hiyo ilikuwa siku ya tarehe 20 Agosti 2004 huko Unguja Ukuu (na sio Zanzibar Mkuu kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoiita) katika shamrashamra za miaka 40 ya Jeshi hilo.
Uzoefu unatuonesha kuwa kila mara watawala wetu, hasa kutoka Tanzania Bara, wanapouzungumzia Muungano katika muktadha wa Uzanzibari, Wazanzibari na au Zanzibar, basi huamua kuijaza hadhira yao khofu za kuvunjika kwa Muungano huu na hatari inayoweza kutokea.
Kwa uchache, hii ni mara ya pili katika mwaka huu kwa kauli kama hii kutolewa Zanzibar. Katika mwezi wa Aprili kwenye sherehe za miaka 40 ya Muungano zilizofanyika kitaifa katika uwanja wa Amaan, Zanzibar, Rais Benjamin Mkapa alisema maneno yanayopishana kidogo na hayo kisintaksia lakini yanayofanana sana kisemantiki.
Alionesha kuwa kuna watu wanaouangalia kwa jicho baya Muungano wetu na kwamba yeye, akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atahakikisha anayatumia madaraka aliyopewa kuulinda Muungano huu.
Wacha niseme tena na tena kwamba hapa pana upotoshaji wa makusudi wa hoja hii. Wanapojibu maswali, kwa mfano, ya nini maana ya kuvunja Muungano na nani anataka kuuvunja Muungano huo, watawala wetu huenda mbali kabisa na ukweli. Hufanya upotoshaji wa makusudi ili kuhalalisha vitisho vyao dhidi ya raia wanaohoji.
Kwa watawala, kuuvunja Muungano kunamaanisha kupinga muundo uliopo wa Muungano. Kwa sasa, muundo ‘unaoambiwa’ upo kwa miaka yote hii 40 ni wa serikali mbili. Nasema ‘unaoambiwa’ kwa kuwa akina mimi tunaushuku huo u-wili wa serikali hizo mbili hapa. Tunachokiona mbele yetu, kwa hakika kabisa, ni kiwango kimoja tu cha userikali___ Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Tunapoiangalia Serikali ya Zanzibar na kuifasiri serikali kama chombo kikuu cha utawala kilichokabidhiwa khatma ya watawaliwa, basi hatuoni kuwa SMZ ndiyo inayoamua khatma ya Wazanzibari. Tunaamini, tena kwa ushahidi kabisa, kuwa khatma ya Wazanzibari, Uzanzibari na Zanzibar inaamuliwa Chimwaga.
Na mifano ya hilo iko mingi, inatosha kujaza kitabu cha kurasa alfu moja. Wa zamani kidogo ni ule wa kuondoshwa Mzee Abuod Jumbe Mwinyi katika nafasi ya urais wa Zanzibar na Mwalimu Nyerere, katika miaka ya ‘80. Hadi leo Wazanzibari wanajiuliza Mwalimu Nyerere alikuwa na mamlaka gani, kisheria, ya kumuondosha Rais waliyemuweka wenyewe!
Wa karibuni kidogo ni huu wa kupatikana mgombea Urais wa Zanzibar wa mwaka 2000. Hadi leo Wazanzibari wanajiuliza mipaka ya mamlaka na madaraka yao kwa nchi yao inaanzia wapi na kumalizikia wapi ikiwa hawathubutu hata kumuweka mgombea wanayemtaka wenyewe, sambe rais wao!
Lakini, kwa kutumia wasta wao walionao, nyenzo za kila aina za habari na uenezi, pamoja na nguvu kubwa waliyonayo kufanya mambo yawe vile wanavyoyataka, watawala wetu wamefanya ionekane kuwa kuukosoa muundo wao wa Muungano wa Serikali Mbili, ni kufanya hila za kuuvunja Muungano. Hawasemi kabisa kwamba watu wanapinga ‘muundo’ tu wa Muungano, bali husema wanapinga Muungano wenyewe.
Nauita huo kuwa ni upotoshaji wa makusudi wa hoja, nao ni miongoni mwa mambo yanayoufanya uhusiano huu baina ya Tanganyika na Zanzibar kuwa ni kizungumkuti. Ndio unaoonesha kuwa pana ‘siasa maalum ya Muungano kuelekea Zanzibar’ na ndio unaotilia shaka na shukuki dhamira ya watawala wetu.
Ndio maana, kwa kuwa watawala wamekuwa wakitaka ieleweke kuwa kuukosoa muundo wao wa Muungano ndiko kuuvunja Muungano, basi linapokuja swali la nani, kwa hivyo, anayetaka kuuvunja Muungano, jibu huwa ni yule anayeukosoa muundo wao.
Na kwa kuwa mtiririko wa matukio katika historia hii ya miaka 40 ya Muungano, unaonesha kuwa ni Wazanzibari ndio walioibuka kama wakosoaji wakubwa wa muundo huu, basi ni wao ndio wanaoonekana kutaka kuuvunja Muungano.
Ni kweli kuwa mifano ya harakati za Wazanzibari kuukosoa muundo huu iko mingi, kuanzia 1964 hadi sasa 2004. Nyuma, mwishoni mwa miaka ya ’60 na mwanzoni mwa miaka ya ’70, kulikuwa na Mzee Abeid Amani Karume mwenyewe. Yeye ndiye aliyekuwa mpinzani mkubwa wa muundo wa Muungano unaoigeuza Zanzibar kuwa koloni la Tanganyika. Kila siku alikuwa na shakashaka juu ya vile mwenzake, Mwalimu Nyerere, alivyokuwa anampelekesha.
Kisha ukaja wakati wa Mzee Abuod Jumbe. Upinzani wake wa muundo huu, ndio uliopelekea kulazimishwa kujiuzulu na Mwalimu Nyerere (kama nilivyotangulia kutaja hapo juu). Kisiasa, wakati huo uliitwa wa ‘Kuchafuka kwa Hali ya Kisiasa Zanzibar’.
Kuondoshwa kwa Mzee Jumbe kulifuatiwa na kipindi kifupi cha Mzee Ali Hassan. Yeye alikaa kwa muda mchache na, bila ya shaka, alikuwa amebanwa na woga kwa kile kilichomuondosha mtangulizi wake. Hata hivyo, Mwalimu Nyerere alikuwa amelegeza kamba yake kidogo kwa Zanzibar na, kwa hivyo, hapakuwa na mtikisiko mkubwa wa wazi wazi.
Lakini aliyemfuatia, yaani Mzee Idris Abdulwakil, alikuwa kama alivyokuwa Mzee Karume na Jumbe. Kuna matukio mingi yanayoripotiwa kuhusu namna alivyopingana waziwazi na wakuu wa Dodoma. Mara nyingi ilipotokezea kuizungumzia Zanzibar mbele ya Muungano, alikuwa akisema mwenyewe na sio kumtuma waziri wake.
Na hata ilipotokezea kuwa amedharurika na hivyo waziri wake kuchukuwa nafasi hiyo, yeye alithibitisha kwamba huo ndio uliokuwa msimamo wa serikali yake. Hakuwahi kuwa msaliti wala mwoga kwa hilo. Na kwa hakika hasa, ni sababu hiyo ndiyo iliyomfanya asisimame tena kugombea Urais kwa mara ya pili pale mwaka 1990, kama ulivyo utamaduni uliojengeka wa rais kukaa vipindi viwili.
Ni ndani ya wakati wake pia, aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake walipofukuzwa CCM na Mwalimu Nyerere kwa hilo hilo la kupingana na muundo wa Muungano.
Ya Awamu ya Tano, wakati wa Dk. Salmin ni ya karibuni zaidi na wengi tunayakumbuka. Jitihada za kujiunga na OIC, jaribio za kubadilisha katiba, mbali na mikwaruzano mingi kati yake na Dodoma zilikuwa ni katika harakati za kivitendo kupingana na aina ya muungano tuliyonayo.
Kwa hivyo, mtiririko huo unaonesha kuwa ni kweli kuwa Wazanzibari wamekuwa wakipingana na muundo uliopo wa Muungano kwa siku nyingi sana. Lakini, si kweli hata kidogo kuwa mtiririko huo unaonesha kuwa wamekuwa wakiupinga Muungano wenyewe. Wangelikuwa hawautaki, usingelikuwepo kitambo mno.
Turudi tena kule tulikoanzia, kwenye kitisho cha Profesa Phelomon Sarungi dhidi ya ‘wavunja Muungano’. Ninarudia tena kuwa Waziri huyu wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ametoa kitisho___ kitisho cha kutumia jeshi kuhakikisha kuwa Muungano unadumu. Hiki ni kitisho sio tu kwa wakosoaji wa Muungano, bali pia kwa uhuru, demokrasia na udugu wetu. Kwa nini?
Kwanza ikumbukwe kuwa Profesa Sarungi ni Mbunge wa CCM na Waziri wa Ulinzi katika serikali ya CCM, chama ambacho Muundo wa Serikali Mbili ndiyo sera yake. Yeye, kwa chama chake hicho na nafasi yake hiyo, ni miongoni mwa wanaounda tabaka la watawala, ambao wameamua kuaminisha kuwa kuukosoa muundo wao wa muungano ndiko kuvunja muungano na ambako, kwa mujibu wa Profesa Sarungi, hakutavumiliwa na jeshi.
Pili, Wazanzibari walio wengi hawajapata kuridhika na muundo huu wa Muungano. Zanzibar, kama ilivyo kwa Tanzania nzima, kuna vyama vyengine vya siasa visivyokuwa CCM na vyenye sera tafauti ya muundo wa Muungano. Matarajio ni kwamba vyama hivi vitashiriki katika uchaguzi mkuu wa 2005 na inawezekana kwa kutumia uhuru na demokrasia yao, Wazanzibari kuamua kukiunga mkono chama kisichokuwa CCM ili kiwasaidie kubadi
li muundo huu wa
Muungano.
Na kwa hivyo, ikiwa kwanza na pili hapo juu ni sahihi, basi mtiririko huo ukijumlishwa na kauli ya Profesa Sarungi unatupelekea katika hitimisho moja tu, nalo ni kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania halitakubali kuwaona Wazanzibari wakikiweka chama kisichokuwa CCM madarakani.
Kwa hitimisho hili, nikiwa kama Mzanzibari, siwezi kujizuwia kusikitika kwa ombwe na ombolezo kwamba Mama yangu Zanzibar anataka kuingizwa katika maafa mingine. Kwa mara nyingine tena, historia ya nchi yangu inataka kuchafuliwa kwa makusudi na, kama ilivyokuwa huko nyuma, mara hii pia si kwa maslahi ya Mzanzibari yeyote___ si kwa aliye madarakani, wala aliye nje ya madaraka, wala kwa wa jana, wala kwa wa leo, na wala si kwa kesho!
Siku zote khofu za Wazanzibari ni uingiliaji kati kutoka Bara. Na wana kumbukumbu nyingi za hayo, ya karibuni zaidi ikiwa ni mauaji ya Januari 2001. Si uzushi kwamba vikosi vingi vililetwa Zanzibar kutokea Bara na yale matukio yaliyoripotiwa ya ubakaji na udhalilishaji mwengine yalipata baraka zote kutoka huko.
Hakuna yeyote ambaye angelipenda picha zile zijirejee. Hakuna linalolitia uchungu kuliko kumuona mkeo au mwanao akinajisiwa mbele ya macho yako. Sote tunalaani yale yanayotokea Darfur hivi sasa, maana yanafanana sana na haya. Wazanzibari wasingelitaka kupelekewa Janjaweed.
Lakini je, kwa kutokutaka huko, ndio Wazanzibari walazimike kutokukiweka chama chengine chochote kisichokuwa CCM kushika madaraka ya nchi yao? Ikiwa ni hivyo, basi kuna tafauti gani baina ya kuwa nchi huru na kuwa koloni? U wapi uhuru hapo? I wapi demokrasia? U wapi utu na u wapi udugu?
Pengine nimekwenda mbali mno katika kuifafanua kauli hii ya Profesa Phelomon Sarungi. Lakini labda nawe ungelijiweka katika nafasi kama yangu, ya kuwa Mzanzibari, kisha ukaayangalia madonda yote ambayo historia imekutia katika kiwiliwili chako. Nina hakika ungeliuhisi ule mtonesheko wake. Ungeliuhisi uchungu wake. Ungeliumia kama ninavyoumia.
Nasisitiza kuwa utumiaji nguvu wowote ule hautaifaidisha chochote Zanzibar na kwamba hautasaidia kuuimarisha Muungano wa Tanzania. Muungano huu utadumu tu ikiwa utakuwa na nafasi katika nafsi za watu wenyewe, yaani ikiwa utazitosheleza nafsi zao na kujibu maswali yao. Jeshi, mizinga, risasi na vyenginevyo, haviwezi kuusimamisha ikiwa watu watakusudia kuuangusha.
Kwani historia iliwahi kushuhudia Muungano imara zaidi ya ule wa Kisovieti? Kuna Muungano gani uliokuwa ukilindwa na jeshi imara zaidi yake? Leo hii uko wapi? Na huko ambako bado Urusi inaendelea kung’ang’ania (kama Chechenya) kunatokea nini kila siku? Si maafa tu, misiba na vilio?
Hata hivyo, kama nilivyokwishaonesha kuwa kinachokosolewa na Wazanzibari sio Muungano wenyewe. Kama kuna yeyote anayeuthamini Muungano huu, basi ni Wazanzibari. Kinachokosolewa hapa ni muundo tu wa Muungano. Tungetaka kuwa na Muungano wa kiadilifu na ulio wazi zaidi na sio wa hila na kizungumkuti hiki.
______________________________________________________________
Makala hii ilichapwa kwanza katika gazeti la Rai na kisha kurejewa katika An-Nur kwenye mwezi Septemba, 2004. Mwandishi hakumbuki namba za matoleo wala tarehe hasa ambazo makala hii ilitokea.

No comments:

Post a Comment