Monday, December 31, 2012

Marokeo Rasmi ya Sensa yatolewa

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wananchi katika uzinduzi wa matokeo ya awali ya sense ya watu na makazi katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.

 
 
 
 
 
 
Rate This

Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ina idadi ya watu Milioni 44,929,002 kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti mwaka huu wa 2012.
Matokeo hayo yanaonyesha ongezeko la idadi ya watu Nchini Tanzania  lililofikia watu  Milioni 33,000,000 ikilinganishwa na  lile la sensa ya watu  la Milioni 12,313,054   baada ya Uhuru .
Akitangaza matokeo ya awali ya sensa ya idadi ya watu  katika viwanja vya Mnazi Mmoja Mjini Dar es salaam Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alisema matokeo hayo yanaifanya Tanzania bara kuwa na Idadi ya Watu Milioni 43,625,434 wakati Zanzibar ina watu Milioni 1,303,568.
Rais Kikwete alifahamisha kwamba  takwimu zinaonyesha kuwa  Tanzania inakadiriwa  kufikia watu zaidi ya Milioni 51,000,000 ifikapo mwaka 2016 kiwango kisichokidhi mahitaji halisi ya uchumi na mipango mengine.
Dr. Kikwete alitahadharisha kwamba idadi ya watu imekuwa kwa kiwango kikubwa na ongezeko  lijalo linaweza kuwa mzigo mkubwa kwa Taifa ambapo alishauri kuwepo kwa mikakati katika kipindi cha miaka minne ijayo ili kukabiliana na ongezeko hilo.
Alizishauri familia kuzingatia  zaidi umuhimu wa suala la kuwa na uzazi wa mpango kwa lengo la kuwawezesha wazazi kuwa na uwezo na mbinu za kuzihudumia familia zao.
Rais Kikwete aliupongeza Umma, Washirika wa Maendeleo pamoja na Viongozi wa nyadhifa tofauti kwa juhudi zao zilizopelekea kufanikisha zoezi ya sense ya watu na makazi na kuviomba vyombo vya habari vilivyotoa mchango mkubwa katika zoezi hilo kuendelea kuelimisha ummamatumizi bora ya Takwimu za sense kwa kudumisha ustawi wa Jamii.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa awali wa matokeo ya sense ya watu na makazi Mwenyekiti wa Kamati kuu ya Taifa ya Sensa ambae pia ni Waziri Mkuu Mh. Mizengo Peter Pinda  alisema asilimia 90% ya gharama za zoezi zima la sense limesimamiwa na Serikali yenyewe.
Mh. Pinda alisema Kiwango hicho kimepindukia asilimia 20% ya gharama za sensa ikilinganishwa na Sensa ya mwaka 2002 ambapo zaidi ya asilimia 70% zilitumika katika zoezi hilo.
Akitoa salamu wakati wa uzinduzi wa matokeo ya awali ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 mwenyekiti Mwenza wa kamati kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema matokea ya sense yatakuwa na maana katika Taifa pale Taarifa zake zitakapotumika kikamilifu katika kupanga maendeleo ya Nchi.
Balozi Seif aliwaomba washirika mbali mbali zikiwemo             Taasisi za Serikali, Sekta binafsi, washirika wa maendeleo na Wananchi kuzifuatilia takwimu za sense kwa kuzitumia katika kupanga mipango ya maendeleo katika maeneo yao ya kazi.
Alisema hatua hiyo itasaidia kufanikisha malengo ya mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Tanzania {MKUKUTA} na mpango wa kukukuza uchumi na kupunguza  umaskini Zanzibar { MKUZA }.
Mwenyekiti huyo mwenza wa Kamati Kuu ya Sensa Tanzania Balozi Seif amewashukuru Viongozi wote wa juu, kati, Wananchi pamoja na washirika wa maendeleo kwa kuitikia wito wa serikali zote mbili wa kuwataka washiriki katikamzoezi la sensa ya mwaka 2012.
Naye kwa upande wake mwakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa Nchini Bibi Maryam Khan alisema Taasisi za Umoja huo zitaendelea kusaidia kitaaluma na uwezeshaji katika kuona Mataifa wanachama yanafanikiwa katika utekelezaji wa Mipango yao ya Maendeleo.
Bibi Maryam Khan alisema sensa ndio msingi muhimu inayotoa mwanga wa mipango ya maendeleo kwa kuimarisha miundo mbinu na kuipongeza Tanzania  kwa juhudi zake za kujiletea maendeleo kwa kutambua umuhimu wa kujua idadi ya watu wake.
Mapema Kamishna wa Sensa Tanzania Hajat Amina  Mrisho  alisema watendaji wa kamati ya sensa  watahakikisha machapisho yote ya sensa yatatolewa na kuchapishwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
Hajat Amina ameelezea faraja yake kutokana na watendaji wake kutimiza ahadi ya kutangaza matokeo ya sensa  kama ilivyojipanga na inajivunia ufanisi mkubwa iliyoupata katika zoezi zima la sense ya watu na makazi ya mwaka 2012.
“ Katika kipindi kifupi tumeweza kutoa matokeo ya awali ya sense ambapo inaonyesha umahiri mzuri walionao watendaji wa sense. Uzoefu wa Kitaifa na Kimataifa mara nyingi unaonyesha kuchelewa kwa matokeo ya takwimu za Sensa”. Alifafanua Hajat Amina Mrisho.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
31/12/2012.

No comments:

Post a Comment