Saturday, December 22, 2012

BEI YA VYAKULA YAZIDI KUWAUMIZA WAKAAZI DAR


NDANI YA SOKO KUU LA KARIAKOO
NDANI YA SOKO KUU LA KARIAKOO
Bei za vyakula katika masoko mbalimbali jijini Dar es Salaam zimepanda kwa kasi kuelekea kipindi cha Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Akizungumza na NIPASHE jana, Mwenyekiti wa soko la Mwananyamala, Hamis Marande, alisema hali ya upungufu wa mvua mikoani imechangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji mdogo wa chakula na hivyo kutoingizwa kwa wingi jijini.
Marande alisema sababu nyingine ni kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa mazao hayo hadi jijini, na hivyo kusababisha uuzaji wa juu ili kufidia gharama mbalimbali za safari.
Alisema tatizo hilo limekuwa kubwa kutokana na wauzaji kuwalazimu kununua kwa gharama kubwa ili kuwauzia walaji kwa gharama za juu kwa lengo la kufidia ununuzi wake.
“Madereva wa magari yanayoleta mazao, wanatoza gharama kubwa kwa madai bei ya mafuta yapo juu pamoja na gharama kubwa za vipuri vya magari…sasa lazima walaji waumizwe na wala si kwa sababu ya sikukuu,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kwa sasa mchele toka Kyela mkoani Mbeya, huuziwa kwa bei ya jumla ya Sh. 1,800 hadi Sh. 1,900 kwa kilo moja wakati awali ilikuwa ni Sh. 1,500 kwa kilo hivyo kuwalazimu kuuza kwa walaji kati ya Sh.2000 hadi 2,500 kwa kilo, huku unga wa sembe wakinunua kwa Sh.1,000 kwa kilo na kuuza Sh. 1,400, awali kilo ya unga ilikuwa Sh. 1000 na maharage huuza Sh.1,800 hadi 2,000 kwa kilo, awali yalikuwa yakiuzwa Sh 1500 kwa kilo.
Katika soko la Mabibo ambalo hujulikana zaidi kama ‘mahakama ya ndizi’, hali ya bei ya bidhaa mbalimbali imepanda hususani kipindi hiki cha kuelekea sikukuu.
Chombo alisema iwapo magari ya kuleta mazao toka mikoani yanachelewa, basi wale wachache walioingiza mapema, huuza bidhaa zao kwa bei ya juu kwa lengo la kujipatia maslahi zaidi.
Alisema katika kipindi cha baridi, hali ya mazao kama viazi, vitunguu na ndizi hushamiri sokoni hapo kutokana na kuingia magari mengi toka katika mikoa ya Njombe, Mbeya pamoja na nchi jirani ya Kenya.
Hata hivyo, waliitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kufanya utafiti wa kutosha ili kuweza kuwabaini wenye magari wanaoongeza gharama za usafiri kwa kisingizio cha upandaji wa mafuta.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment