Monday, December 31, 2012

Padri aliyepigwa risasi Z’bar ashingizia dini

 
 
 
 
 
 
Rate This

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Baloz Seif
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, akimjulia hali Padri Ambrose Mkande.
Jamii nchini inapaswa kuzingatia suala la amani,Umoja na kuendeleza upendo miongoni mwao ili kusaidia kuzalisha kizazi bora kinakachozingatia haki na maadili katika maisha yao ya dunia. Nasaha hizo zimetolewa na Kiongozi wa Parokia ya Mpendae Padri Ambrose Mkenda wakati akijuliwa hali na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipotembelewa katika Hospitali ya Rufaa Kitengo cha Mifupa cha MOI Muhimbili Mjini Dar es Salaam.
Padre Ambrose anaendelea kupatiwa huduma za afya baada ya kujeruhiwa kwa Risasi hivi karibuni na watu wasiojuilikana mbele ya Mlango wa skuli ya Francis Maris ambapo ndipo yalipo makazi yake katika maeneo ya Tomondo Wilaya ya Maharibi.
Alisema zipo dalili za wazi zinazoashiria kuwepo kwa vikundi vya watu vinavyo shawishi baadhi ya wananchi hasa Vijana kujiingiza katika matendo yanayohatarisha usalama wa watu wengine.
Akielezea mkasa uliompata hivi karibuni wa kushambuliwa kwa Risasi na kupelekea kulazwa Hospitali Padre Ambrose aliufananisha mkasa huo na matendo yaliyoandaliwa kwa makusudi ili kupunguza harakati zao za kuhubiri amani miongoni mwa Jamii.
“ Mimi nipo Zanzibar kufanya kazi za mahubiri Dini tokea mwaka 1995 na kipindi chote hicho kazi zetu zinafahamika, zinaeleweka na kupokewa vyema na Jamii. Sasa mkasa huu utasemaje kuwa na ujambazi wa kutapa mali ? Alifafanua Padre Ambrose.
Kiongozi huyo wa Parokia ya Mpendae Padre Ambrose Mkenda amezishukuru juhudi za Viongozi wa Serikali zote mbili za kujali maisha ya raia wake pamoja na kujaribu kudhibiti matendo maovu katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Kiongozi huyo wa Parokia ya Mpendae Padre Ambrose Mkenda alisema Mchango wa Viongozi wa Dini katika kuhubiri suala la Amani nchini ni vyema ukazingatiwa na kuheshimika na Jamii.
Balozi Seif alisema Taifa na Jamii kwa ujumla imekuwa ikiendelea kuishi kwa amani na utulivu kutokana na mchango mkubwa wa Viongozi wa Dini ambao wamekuwa na makundi makubwa wanayoyaongoza.
“ Suala la amani iwe ya Taifa au Jamii husika inamuhusu kila mtu na ushahidi wa hayo unapatikana katika vitabu vyote vya dini ambavyo vimekuwa vikihubiri amani kila wakati”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuombea kwa Mungu Padre Ambrose apone haraka na kurejea katika familia yake na watu wanaomhitaji kuwasaidia katika matendo ya Ibada.
Othman Khamis Ame

No comments:

Post a Comment