Saturday, December 22, 2012

Polisi yakamata silaha 889


silaha
JESHI la polisi nchini limekamata jumla ya silaha 889 na risasi 10,210 katika operesheni mbalimbali za kupambana na uhalifu kati ya Januari hadi Novemba mwaka huu.
Hayo yalibainisha jijini Dar es Salaam jana na Naibu Kamishna wa Polisi, Issaya Mngulu, alipokuwa akisoma taarifa ya hali ya uhalifu nchini.
Pamoja na hilo, alisema kumekuwepo na taarifa mbalimbali ya watu kupatikana na silaha na zinazomilikiwa kinyume na sheria, hali iliyochangia kutokuwepo kwa amani ya kutosha nchini.
Hata hivyo, alisema kwa agizo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, la kuwataka watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha, linaendelea vizuri na jumla ya silaha 98 zikiwemo za kijeshi na kiraia zimesalimishwa kwa mwezi Desemba pekee.
Mngula alisema matukio mengine ya usalama yanayojitokeza licha ya jeshi la polisi kukabiliana nayo ni ugaidi, uharamia, wahamiaji haramu na biashara haramu za usafirishaji binadamu, uhalifu dhidi ya mazingira na maliasili, uingizwaji bidhaa bandia, dawa za kulevya, migogoro ya kisiasa na kidini, pamoja na migogoro ya wanafunzi wa taasisi na vyuo vya elimu ya juu.
Aidha alisema jeshi la polisi linaendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutambua maeneo nyeti yenye vivutio vya uhalifu na kupanga ulinzi wa kutosha, kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu za kukabiliana na wahalifu pamoja na kuimarisha misako na doria.

No comments:

Post a Comment