Uchambuzi: Kuibuka kwa Maalim Seif, fimbo ya Musa – 2
Na Ahmed Omar
Katika vitabu vyote vya dini kubwa duniani, kuna mkasa wa Nabii Musa aliyetumwa na Mungu kuwakomboa wana wa Israel kutoka utawala kandamizi wa Firauni. Firauni aliwatawala kama watumwa Waisraeli na akafanya vituko vingi duniani vya kukufuru hadi kufikia kujiita Mungu. Mungu alimpelekea habari Firauni kwamba angelizaliwa mtoto wa kiume ambaye atakua nabii na kuleta nuru na ukombozi kwa watu wa Israel.
Baada ya kupata habari hizo, Firauni hakuruhusu uhai wa mtoto yeyote wa kiume aliyezaliwa akifahamu kwamba ndiye adui kwa utawala wake. Aliwaangamiza watoto wachanga wote wa kiume waliozaliwa ili kuunusuru utawala wake.
Jambo la kushangaza ni jinsi Nabii Mussa (mtoto wa kiume) alivyozaliwa mbali ndani ya kipindi hicho hicho na alivyokuja kulelewa na kukulia ndani ya kasri ya Firauni mwenyewe.
Hii ni kwa sababu Nabii Mussa ni rehma kutoka kwa Mungu, hivyo Firauni na wasaidizi wake hawakuwa na uwezo wa kumuangamiza. Nabii Mussa alikuwa yuko chini ya nusura ya Mungu ambayo bila shaka inashinda nguvu za wote ambao wangetamani kumdhuru.
Chini ya kivuli cha simulizi hiyo kutoka vitabu vitukufu, hebu tugeukie historia ya kisiasa ya Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ambayo inaonesha kwamba hakuwahi kabisa kutamani kuwa mwanasiasa wala kuwa kiongozi tokea utoto wake na ujana wake, ijapokuwa kipaji cha uongozi kilionekana kwake mapema mno.
Mnamo mwaka 1975, akiwa kwenye kazi yake ya ualimu katika chuo cha uwalimu Beit-el-Raas (sasa sehemu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, SUZA) alipokea wito kutoka Ofisi ya Rais, wakati huo Mzee Aboud Jumbe Mwinyi. Ikumbukwe kwamba wakati huo, ikiwa ndio kwanza ni muongo mmoja baada ya Mapinduzi na Muungano, na pia mwaka mmoja tu baada ya kuuawa kwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Karume, nchi ilikuwa kwenye kipindi kigumu cha giza la kisiasa na kijamii. Kuitwa Ikulu hakukuwa na maana njema sana, katika hali ya kawaida.
Akiwa ameshangazwa na wito huo, kwa vile hakuwahi kuwa na mawasiliano wala mahusiano ya moja kwa moja na Ikulu, Maalim Seif aliitikia wito na Rais Aboud Jumbe akamwambia Maalim Seif kwamba kuanzia siku hiyo angelianza kufanya kazi katika ofisi yake kama katibu msaidizi maalum (special assistant) wa Rais.
Hivyo ndivo rehema ya Mungu ilivyomfikisha Maalim Seif ikulu ya Zanzibar ndani ya zama za “sharia za kimapinduzi” (revolutionary justice). Hakuota, hakuwaza, hakujisogeza wala hakuomba.
Mwaka 1977, Rais Jumbe aliamua kufanya mabadiliko ya baraza la mapinduzi. Kupitia mabadiliko hayo alimtangaza Maalim Seif pamoja na wenzake kuwa ni mawaziri wapya wateule wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, yeye Maalim Seif akiwa ni waziri wa elimu.
Kufuatia mabadiliko hayo serikali ya Jumbe ikapata nuru. Ilitoa unafuu mkubwa kwa wananchi ukilinganisha na utawala wa Karume uliotangulia. Baada ya Mapinduzi, wanafunzi hawakuweza kuendelea na maomo kwa mujibu wauwezo wao wa kupasi mitihani bali ilikuwa kwa kuzingatia makabila ya baba zao. Utaratibu uliotumika uliruhusu Waafrika asilimia themanini (80%), Waarabu asilimia kumi na tano (15%), Wahindi asilimia nne (4%) na Wakomoro asilimia moja (1%) kuendelea na masomo.
Baada ya kuwa waziri Maalim Seif alimshauri Jumbe kuubadilisha utaratibu huo na badala yake wanafunzi wachaguliwe kuendelea na masomo kwa uwezo wao wa kupasi mitihani na sio makabila yao. Jumbe na Seif walifanikiwa kufanya hivyo, japokuwa walipambana na upinzani mkali wa akina Seif Bakari na Natepe waliokuwa wakijifanya kuwa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar (Burgess 2009).
Sambamba na hili Maalim Seif alifanya jitihada ya kuwatafutia wanafunzi wa Kizanzibari nafasi maalum za kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam hata kama kiwango chao cha kufaulu kilikuwa chini ukilinganisha na wanafunzi wa Tanzania Bara. Hoja ya Maalim Seif, kama waziri wa elimu, ilikuwa ni kwamba Zanzibar inatoa kiwango kidogo cha wanafunzi wanaokwenda katika elimu ya juu ukilinganisha na Tanzania Bara na kwa kuzingatia kwamba elimu ya juu ni suala la Muungano.
Maalim Seif pia alimshauri Rais Jumbe nafasi za elimu ya juu baina ya wanafunzi wa Pemba na Unguja iwe kwa uwiano wa asilimia 40 – Pemba na asilimia 60 – Unguja. Kabla ya hapo kulikuwa na kiwango kikubwa cha ubaguzi katika kuchagua wanafunzi wa kujiunga na vyuo vikuu baina ya Unguja na Pemba kukiwa na upendeleo mkubwa kwa kisiwa cha Unguja, ili kujenga chuki baina ya watu wa Unguja na Pemba. Hata hivyo, kutokana na asilimia kubwa (60) ya nafasi za Unguja, wanafunzi kutoka Unguja hawakuweza kujaza nafasi zao na hivyo nafasi hizo kukamilishwa na wanafunzi kutoka Pemba (Burgess 2009).
Baada ya Rais Jumbe kulazimishwa kujiuzulu mwaka 1984, Rais mpya Ali Hassan Mwinyi aliingia madarakani. Mwinyi alimteua Maalim Seif kuwa waziri kiongozi wa serikali yake. Chini ya ushauri mzuri wa Maalim Seif, Zanzibar ilizidi kupata neema katika utawala wa Mwinyi. Zanzibar ilirudisha matumizi ya paspoti ili kudhibiti uingiaji holela wa watu na hivyo basi mambo mengi ya udhia kama vile ujambazi, uhalifu, madawa ya kulevya na maradhi ya kuambukiza yaliweza kudhibitiwa.
Upigaji watu kiholela na kuwaweka ndani mambo ambayo yalikuwa yakifanywa na Youth League katika awamu zilizotangulia yaliondoshwa. Serikali mpya pia ikawashawishi vijana kusoma na kupatiwa nafasi za masomo nje ya nchi. Halikadhalika vijana wasomi wakashawishiwa kuomba nafasi za uongozi serikalini, bila ya kuzingatia makabila ya baba zao au mahusiano ya baba zao na Uhizbu, Uafro au Ukomredi kama ilivyokuwa kabla (Burgess 2009).
Isitoshe, Mwinyi na Maalim Seif walianzisha katiba mpya ya mwaka 1984 iliyoruhusu utawala wa sheria na mipaka ya madaraka kwa mihimili ya dola ambayo iliandikwa na mwanasheria mkuu wa serikali wa wakati huo ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria wa sasa, Abubakar Khamis Bakar.
Vile vile, chini ya uongozi wa viongozi hao wawili, ulianzishwa mfumo mpya wa mahakama za kisheria na kufutilia mbali mahakama za wananchi zilizoanzishwa na Sheikh Karume ambazo zilikuwa zikiendeshwa kinyume na misingi ya sheria na haki. Haki za binaadamu katika katiba ya Zanzibar zililingana zaidi na zile zilizomo kwenye Tangazo la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kuliko zile zilizokuwemo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa kweli serikali ya Mwinyi na Maalim Seif pamoja na kudumu kwa muda mfupi sana, iliweza kuleta mabadiliko mengi. Mabadiliko mengine yalikuwa ni pamoja na uhuru wa wananchi kutoa maoni yao. Mambo mengi ambayo kwa njia moja au nyingine yalionekana kuwa ni ya kubana haki za raia ambayo yalikuja mara baada ya Mapinduzi, yalibadilishwa katika wakati huo. Vizuizi vingi vya kufaidi uhuru na haki za kiraia viliondolewa. Vyombo vya habari vya Serikali vilitakiwa kuanzisha vipindi maalum vya kuwapa nafasi wananchi kutoa maoni yao juu ya uendeshaji wa nchi yao. Vipindi kama ‘Zanzibar ni Njema’ katika Radio ya Zanzibar na ‘Jicho’ katika Televisheni ya Zanzibar (TVZ) vilivyotoa fursa kwa Wazanzibari kutoa maoni yao kuhusu uendeshaji na utendaji wa Serikali yao vilianzishwa katika kipindi hicho.
Lakini kubwa zaidi katika utawala wa Mwinyi na Maalim Seif ilikuwa ni kuruhusiwa biashara huria, yaani ‘Trade Liberalisation’ hatua ambayo ilipelekea ghafla kubadilika kwa hali za maisha ya watu na kuimarika kwa uchumi na pato la taifa. Jambo hili lilimchukiza sana Nyerere kwani ni kinyume na siasa yake ya ujamaa, lakini Mwinyi na Seif walimjibu Nyerere kuwa “tunataka kuuimarisha ujamaa kwa kutumia mfumo huria”. Majibu hayo yalimpoza Nyerere. Uhaba mkubwa wa chakula uliokuwepo kabla ulimalizika na umasikini ukapungua makali yake kwa kiwango kikubwa. Wafanyabiashara kutoka nchi za jirani kama Kenya na Tanzania Bara wakawa wanakuja Zanzibar kutafuta bidhaa. Maisha ya watu yakaboreka na neema kutanda. Hapo ndipo Mwinyi alipozaa msemo wake maarufu, Zanzibar ni njema atakae naaje na baadaye msemo huu ukawa miongoni mwa maneno ya hekima.
Huu ni upande mmoja wa hadithi ya mafanikio katika safari ya kisiasa ya Maalim Seif Sharif Hamad, ambayo ilidumu kwa kiasi ya muongo mmoja ndani ya serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM). Lakini ukweli ni kwamba safari hii haikuwa nyepesi sana na kulikuwa na vigingi vingi ndani yake.
Baada ya kifo cha Edward Sokoine, Nyerere alimteua Salim Ahmed Salim kuwa waziri mkuu mpya. Hivyo basi Salim Ahmed Salim kwa upande wa Jamhuri ya Muungano alitarajiwa sana kuwa mrithi wa kiti cha urais baada ya kustaafu Nyerere.
Kwa upande wa Zanzibar nako Maalim Seif alitarajiwa sana kurithi kiti cha urais baada ya Mwinyi kumaliza muda wake. Upepo huo wa kisiasa haukuwa ukiwapungia vyema wanamapinduzi wa Zanzibar. Wanamapinduzi hawakupendelea mabadiliko hayo kutokea na walifanya kila wawezalo kuubalisha upepo huo wa kisiasa ili Salim Ahmed Salim kwa upande wa Jamhuri ya Muungano na Maalim Seif kwa upande wa Zanzibar wasiweze kuwa marais wanaofuatia.
Kosa la Maalim Seif lilikuwa ni Upemba wake, wakati Salim Ahmed alikuwa na makosa matatu kwa mujibu wa kamusi la kihafidhina la Zanzibar: Kosa la kwanza ni Uarabu, kosa la pili ni Upemba kama Maalim Seif na kosa la tatu ni mwanachama wa zamani wa ZNP. Ijapokuwa Nyerere na Mwinyi walimuona Salim ndiye anayefaa zaidi kuwa raisi wa Jamhuri ya muungano, lakini alipigwa vita na wanamapinduzi.
Nyerere kwa kuwatii wanamapinduzi akasitisha azma ya kumteua Salim na badala yake akamteua Mwinyi kuwa rais mpya wa Jamhuri ya Muungano, baada ya yeye kung’atuka mwaka 1985.
Kwa upande wa Zanzibar majina matatu ya Idri Abdul-wakil, Maalim Seif na Salmin Amour ndio yaliojadiliwa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa (NEC) kuteua mmoja wao kuwa rais mpya baada ya Mwinyi kupelekwa katika kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano.
Mzee Idris alikuwa wa mwanzo kuomba jina lake liondoshwe kutokana na uzee. Maalim Seif alikuwa kijana na alijulikana zaidi katika chama, katika NEC na wananchi wa Unguja na Pemba, hivyo kulikuwa na kila aina ya uwezekano wa kushinda kura nyingi kulinganisha na Idris Abdul-wakil. NEC ilishangazwa sana kutangazwa ushindi wa Idris Abdulwakil. Hapana shaka wanamapinduzi waliingilia kati suala hilo na kumfanya Nyerere kuchakachua matokeo ya kura ili kumpinga Maalim Seif na kumpitisha Idris.
Hapa ndipo wakati mgumu kwa siasa za Zanzibar baada ya kuzaliwa CCM ulipoanza. Wazanzibari hawakufurahia Mwinyi kupelekwa Bara wala hawakufurahishwa na uteuzi wa Idris na kuachwa Maalim Seif kwa kuwa Mzee Idris hakujulikana vyema na Wazanzibari.
Takriban asilimia 80 ya wananchi wa Pemba na asilimia 63 ya wanachi wa Mkoa wa Mjini Maghrib Unguja walimpigia Idris kura ya “hapana” na hivyo kuzua mtafaruku mkubwa wa kisiasa. Baada ya wimbi la kukataliwa Idris kutanda Zanzibar na hivyo siasa za CCM kuwa ngumu mno, Nyerere alimshauri Idris kumteua Maalim Seif kuwa waziri kiongozi.
Lakini hata uteuzi huo wa waziri kiongozi haukuwafurahisha wanamapinduzi. Wao walitaka waziri kiongozi awe Salmin Amour. Hivyo basi wakazidisha na kuendeleza chuki na vita vyao dhidi ya Maalim Seif. Kila aina ya shutma na visingizio wakavitoa ili kumpotezea umaarufu Maalim Seif ndani ya chama na ndani ya serikali.
Moja ya shutma zilizowahi kutolewa ni kuwadharau, kuwavunjia heshima na kuwadhalilisha wanamapinduzi, akina Seif Bakari. Shutma nyengine ni kutaka kurejesha usultani Zanzibar. Katika kipindi hichi kuliimarika mahusiano ya kidiplomasia baina ya Zanzibar na Falme za Kiarabu. Wanamapinduzi wakatumia fursa hiyo kutoa shutma kwamba Maalim Seif ana mipango wa kurejesha utawala wa kisultani Zanzibar.
Katika ziara moja ya Maalim Seif nchini Oman katika jitihada zake za kuiletea neema Zanzibar, Sultan Qaboos Busaid alisema wazi kwamba ana kila sababu ya kuisaidia Zanzibar kwa kiwango kikubwa kwa kuwa ni wasomi wa Kizanzibari ndio walioijenga Oman bila ya serikali ya Oman kuchangia chochote katika elimu zao (Burgess 2009).
Maalim Seif na Qabous kupitia ziara hiyo waliahidiana mambo mengi ya maendeleo kwa Zanzibar kama vile ujenzi wa viwanja vya ndege, kutanua miradi ya maji na ujenzi wa barabara. Ahadi zote hizo zilibezwa, kupuuzwa na kuzuiliwa utekelezaji wake na wanamapinduzi.
Tuhuma nyengine dhidi ya Maalim Seif ni kuwapendelea Wapemba. Maalim Seif alituhumiwa kuwapendelea wapemba kwa ushauri wake wa mgao wa huduma na mipango ya maendeleo kwa asilimia 60 kwa Unguja na 40 kwa Pemba. Baada ya tuhuma kadhaa wa kadhaa kushindikana kutumika kama sababu na visingizio vya kumtoa Maalim Seif katika wadhifa wake, ikatumika shutuma ya kufanya upinzani ndani ya chama. Kupokonywa Maalim Seif uwaziri kiongozi kukawadia na habari zikazagaa kila upande. Mrithi wa nafasi Maalim Seif iliamuliwa kuwa Dk. Omar Ali Juma ili kuwatuliza Wapemba baada ya kitendo cha kutolewa Maalim Seif.
Hata hivyo Dk. Omar aliposikia habari hizo haraka alifika kwa Maalim Seif na kumwambia kwamba kuna habari kwamba unataka kutolewa katika nafasi yako na baadae nafasi nipewe mimi, lakini mimi sitokubali nikijua ni kuwagawa Wazanzibari na kujenga fitna. Tarehe 18 Januari 1988, Seif Sharif akapokonywa wadhifa wa uwaziri kiongozi na Dk. Omar Ali Juma akachaguliwa kuwa waziri kiongozi mpya, huku Dk. Omar akifurahia na wala hakukataa kama alivyoahidi kabla.
Baada ya kitendo cha Maalim Seif kufukuzwa Zanzibar haikuwa shuwari. Mengi yalizungumzwa, chama cha CCM kulaaniwa na kukataliwa, Nyerere kuonekana ndiye anayewagawa Wazanzibari na Muungano kushutumiwa. Matukio hayo yalimkera sana Nyerere na ndipo alipolazimika kumfukuza Maalim Seif kabisa katika chama ili akose jukwaa la kufanyia siasa.
Kikao cha NEC kilichofuatia kilijadili tuhuma dhidi ya Maalim Seif na wenzake saba tuhuma dhidi ya Seif na wote walitakiwa kujiuzulu nafasi zao katika chama, ambapo baada ya wote kugoma kufanya hivyo Nyerere akatamka mbele ya wajumbe wa NEC “kama mmegoma kujiuzulu kwa nafasi niliyonayo nimekufukuzeni nyote katika chama”. Maalim Seif na wenzake walifukuzwa katika chama siku ya mwezi 27 Ramadhani, kwa mujibu wa Waislamu ni usiku wenye uwezekano mkubwa wa kupatikana lailatul-qadr.
Baada ya Maalim Seif kutolewa serikalini na kufukuzwa katika chama, Wazanzibari wakaghadhibika mno. Watu makundi kwa makundi wakarudisha kadi za chama na wengine kuzichana. Wengine walitengeneza sanamu za Nyerere, hususan huko Pemba, na kuziharibu hadharani kuonyesha hasira zao.
Mara tu Maalim Seif alipowasili kisiwani Pemba kutokea Dodoma makundi kwa makundi ya watu walikuwa wakikusanyika wakiwa na hamu na shauku ya kuzungumza nae. Nchi ilipooza na siasa za chama cha mapinduzi Zanzibar zikakwama. Nyerere akahisi kwamba hata kuwa nje ya chama na serikali, Maalim Seif ataendelea kuwa tishio kwa nchi na chama hivyo tuhuma kadhaa zikabuniwa ili kumtia gerezani.
Serikali ilijaribu kwanza kutaka kumshtaki Maalim Seif kwa madai kuiba nyaraka za serikali lakini baada ya kushindwa kuthibitisha walimshtaki kwa kosa la kuitisha mikutano haramu. Seif alifungwa jela kwa kipindi cha miezi 30 kuanzia mwezi wa Mei 1989 hadi mwezi wa Novemba mwaka 1991.
Jitihada mbali mbali zikachukuliwa za kidiplomasia, Shirika la Amnesty International na wasomi kudai Seif Sharif atolewe jela. Baada ya hapo akatolewa pamoja na masharti na vikwazo vingi. Pamoja na yote hayo bado Maalim Seif aliapa kutimiza ahadi yake ya kuwatetea Wazanzibari kama alivyoahidi.
Na hilo ndilo ambalo amekuwa akifanya tangu wakati huo na hadi sasa. Mwalimu huyu ambaye hakuwahi kuwaza kama angekuwa kiongozi siku moja. Hii ina maana uongozi haikuwa tunu yake wala ndoto yake.
Tunaweza kusema uongozi kwa Maalim Seif ni rehma kwa Wazanzibari kutoka kwa Mungu ili aje awakomboe kutokana na utawala uliojengewa misingi imara kwa muda mrefu ya ubaguzi, chuki, farka, unyanyasaji, ukandamizaji na maonevu kadhaa wa kadhaa.
Maalim Seif ameletwa kuja kuwaunganisha Wazanzibari waliogawanywa tokea miaka ya 1950 na kuwafanya waonane kwamba wao ni ndugu wa damu. Maalim Seif amekuja kuwaunganisha Wazanzibari kudai nchi yao iliyopotea kupitia Muungano wa 1964 na kuirejesha ndani ya mamlaka yao ili waweze kujiamulia mambo yao yote kijamii, kisiasa na kiuchumi na hivyo wapate kuifaidi keki ya taifa lao tukufu.
Hivyo basi majemedari wa mapinduzi hawakuweza kuizuia rehema ya Mungu na hivyo hawakuwa na nguvu za kuiepusha rehma ya Mungu isimpeleke Maalim Seif ikulu ya serikali yenye misingi ya kimapinduzi. Viongozi wote wengine wanazuka, wanakuwa maarufu na kupotea, lakini sivyo kwa Maalim Seif ambae nyota yake inazidi kung’ara kila siku zikienda.
Jambo hili linawatahayarisha na kuwaiaibisha wale wenye mawazo ya akina Borafya Silima wanaodhani ipo siku wanaweza wakamtukana Maalim Seif akatukanika, wakamfedhehi akafedheheka, wakamkejeli akakejelika na wakamdharau akadharaulika. Kwa huyu haliwi, maana yeye ni mtu wa rehma kwa Wazanzibari na Zanzibar.
No comments:
Post a Comment