Wednesday, January 2, 2013

KHATMA YA MUUNGANO


 

Wakati harakati za mchakato wa Katiba na madai makubwa ya wananchi ya kutaka suali la Muungano wa Zanzibar na Tanganyika lipatiwe ufumbuzi ukiendelea, kuna mengi ya kujiuliza na kuiuliza Serikali juu ya Utendaji wake na usimamiaji wake wa demokrasia, uhuru na haki za binadamu hasa hapa visiwani, Zanzibar.

Nadharia ya Muungano wetu iko wazi kiasili. Iko wazi kwamba ni Muungano wa nchi huru mbili- Tanganyika na Zanzibar, zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kiilivyo, muungano huu ulipaswa uwe na misingi ya usawa kwa pande zote mbili zilizoungana bila kujali ukubwa na udogo wa mshirika mwenza wa Muungano huo.
Cha ajabu, Muungano wetu haukubakia na sura yake ya awali, yaani wa usawa kati ya pande mbili. Awali, Muungano ulikuwa na sura ya Kaka mkubwa kwa mdogo. Ikawa Zanzibar inafanywa ni kijisehemu cha mkoa tu wa Tanzania huku Tanganyika ikifa bila kufanyiwa maziko na hakuna anaelijulia kaburi la maiti hio ya miaka 51, inayonuka bila kuonekana mzoga wake ulipo.

Ukweli ni kwamba, Zanzibar ni zaidi ya kaka mdogo kwa muungano wa sasa.Zanzibar ndani ya Muungano imebanwa na kukandamizwa kila hali na kila muandishi mzalendo ameshaandika sana juu ya hili na sina haja ya kulirudia tena. Kinachonishangaza tu kwa sasa, ni kuona kila harakati anayoifanya Mzanzibari ya kujikwamua na madhila ya Muungano hata kwa njia ya kidemokrasia, mapamabano hayo huishia kwa matumizi makubwa ya nguvu za dola zinazopelekea maafa makubwa, tena ni kwa Wazanzibari tu kila siku, ambao hawana haki ya kuhoji haki zao katika Muungano wao.
Tukiamua kutaja mabavu na uharamia wa Serikali zetu mbili iwafanyiazo Wazanzibari, ili kuwaziba mdomo wasidai haki zao, basi tutapata kitabu kizima. Achilia matukio ya kuuwawa watu wenye mitazamo hasi dhidi ya Muungao kutoka Zanzibar, manyanyaso na mateso kwa raia na viongozi wa dini wanaopinga Muungano, mauaji ya kinyama ya dola dhidi ya Raia wa Zanzibar, hayo ni machache tu kuyataja.

Imekuwa kama utamaduni kwa vyombo vyetu vya Dola chini ya uelekezi wa Serikali kufanya kadiri wanaloweza kuzamisha na kukwamisha kila juhudi, kuzima kila pumzi, na kuliziba kila ombwe alipigalo Mzanzibari kudai haki yake kikatiba. Na hili ndilo linalowapa viongozi nguvu ya kujisifu kuwa nchi hii iko huru, ina demokrasia, na ipo kwa ajili ya watu. Ni kweli, ipo kwa ajili ya watu, lakini sio Wazanzibari.

Imekuwa kama mila na desturi kwa Serikali zetu, kila ujapo uchaguzi ngome ya jeshi ya kivita hufunguliwa Zanzibar. Tumeona 1995, 2000, na 2005, tuliletewa vifaru, mizinga na maroketi wachlia mbali ‘mijeda’ yenye magwanda hadi majumbani, katika vijisiwa hivi vidogo vyenye watu wasiozidi milioni moja na kuacha kupeleka majeshi kule bara ambako kuna watu zaidi ya milioni 40. Hivi haya ndio matunda ya Muungano? Hivi tuseme hapa Serikali inatupa Taswira kuwa Zanzibar ni nchi huru katika Muungano? Siamini.

Siamini kwa sababu hakuna haja ya kuwalazimisha watu wakubaliane na msimamo Fulani, ilhali wako huru kuchaguwa wanalolitaka. Na kufanya hivi ni bishara safi ya kuwa Muungano kati yetu haukuwa wa hiari, wala wa manufaa kwa pande zote mbili na kwa maana hio unapoteza sifa na maana ya kuitwa Muungano. Muungano wetu umekuwa ukitumika kuimaliza Zanzibar kwa kutumia vyombo vya dola kufanya mabavu dhidi ya wananchi.

Mifano mengine michache tu, kutekwa nyara kwa Ustadh Farid kulikohitimishwa ni kutiwa ndani kwa kesi za kubambikiwa zisizopunguwa sita, na zote hazina nyuma wala uso, ni matokeo ya kuungana kwetu kwa nia safi na wenzetu. Jengine, Maoni ya katiba yalioko hivi sasa Zanzibar, kila wazanzibari wakijieleza kwa uhuru, hukandamizwa, hutishwa na hata Warioba mwenyewe hasa ukitaja Muungano wa mkataba. Hapa hakuna haki.Kwanini iwe sisi tu, sio Tabora shinyanga na hata Tarime ambako hata Serikali inaogopa kufika kwa fujo za Wakurya?

Isitoshe, mchakato wa katiba Zanzibar hivi sasa umeshapandikizwa viluilui vya fitina kutoka kwa watu Serikalini kuhakikisha kuwa Zoezi na jaribio la kuukataa Muungano halifanikiwi kwa njia yoyote ile. Yote haya ni matunda ya Muungano ambao ni sawa na yale tuyaonayo wakati wa uchaguzi ya kuletwa watu kutoka bara kwa meli kuja kuvoti Zanzibar. Yaani hivi tu kila siku. Alimradi Serikali imeapa kupiga, kuuwa, kugaragaza kuulinda Muungano ambao wananchi hasa Wa Zanzibar wamechoshwa nao.Tusimumunye maneno!

Wanaoutaka Muungano Zanzibar wapo wengi lakini sio huu uliopo. Ukiachilia wasioutaka kabisa, basi wengi wanahisi uletwe mkataba mpya tukubaliane upya. Kwa upande mwengine, wako wanaotaka ubakie hivi hivi ulivyo lakini hawa ni wale wale, wao kwa wao, na akina mburumatari ambao bila ya kusema hivi watakosa vyeo walivyonavyo. Lakini wakiondoka leo madarakani hujutia maamuzi yao haya ndani ya roho zao.

Madhila ya Muungano kwa Zanzibar ni kama hewa yenye sumu, hakuna aliekuwa hajaivuta na hakuna aliekuwa haikumuathiri hata ukimsikia akijinadi kuwa muumini wa Muungano uliopo kiasi gani. Akiondoka hapo jukwaani hukohoa damu kama sisi wengine akiwa chumbani mwake au hata chooni. Lazima atakohowa tu! Hewa iliyochafuka haikwepeki hata ukijitahidi kiasi gani. Na kwa Zanzibar ndani ya Muungano, hakuna hewa safi, tusifichane. Si mimi, si Mansuri, si Shamsi wal si Mwinyi Haji, nguvu ya soda tu, sote tunakohowa damu kwa kudhuriwa na hewa mbovu ya Muungano!

Na kwa hatua hii uliyofikia Muungano wetu na matendo yafanywayo na Serikali zetu dhidi ya Wazanzibari ni zaidi ya ukoloni, au mateso ya ubaguzi wa rangi wa kule Afrika kusini enzi za makaburu. Nasema hivi kwa kukozesha sentensi, kwa sababu hakuna sifa hata moja ya kuonesha kuwa kuna tena Muungano wa usawa na nia njema. Kilichopo ni ujanja wa Tanganyika walioutumia kuivamia Zanzibar na kuichukuwa kama himaya yao. Na kwa hio Zanzibar imetwemwa na mkoloni mweupe, ikamezwa na mkoloni mweusi, yaani kwa kimombo, ‘from the frying pan, to the fire’ au ‘from gallows to the firing squad’!

Nasema hivi nikiwa na ushahidi kuwa nchi zote zilizoungana, hazitumii mabavu wala dhuluma dhidi ya upande mshirika wa Muungano huo, eti tu kwa sababu kuna watu wadai haki zao katika Muungano huo. Na kwa maana hii Muungano wetu umepoteza sifa kwani badala ya kutumia katiba, haki, na demokrasia ya maoni huru inatumia mabavu kwa kila jambo lifanywalo Zanzibar hata ikiwa hakuna haja ya kufanya hivyo. Kunani Zanzibar?
Tuachiwe tupumuwe!

No comments:

Post a Comment