Kiongozi wa Ujumbe wa wanafunzi wa Chuo Cha Ulinzi Cha Taifa Brigedia
General R S Laswai (aliyesimama) akiutambulisha ujumbe huo kwa Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad walipofika ofisini
kwake Migombani kwa ajili ya kuonana nae.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema katika jitihada za kukuza
uchumi wa Taifa, serikali inaweka mkazo katika kuziendeleza sekta kuu za
kiuchumi zikiwemo Utalii, Kilimo na Uvuvi.
Amesema sekta hizo zina mchango
mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa, na kwamba zitaendelea kupewa
kipaumbele ili kuhakikisha kuwa uchumi wa Zanzibar unakua hadi kufikia
asilimia tisa kwa mwaka.
Akizungumza na ujumbe wa
wanafunzi wa Chuo Cha Ulinzi Cha Taifa kilichoko Dar es Salaam
waliofika ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kuonana nae, Maalim Seif
amesema licha ya matatizo ya kiuchumi yanayoikabili dunia mara kwa mara,
hali ya uchumi wa Zanzibar inaendelea vizuri ambapo ukuwaji wake ni
kati ya asilimia sita hadi saba kwa mwaka.
Amesema athari za kiuchumi
zinazotokea duniani zimekuwa zikisambaa katika nchi mbali mbali ikiwemo
Zanzibar, lakini athari hizo zimekuwa zikidhibitiwa na serikali kwa
kuweka mipango imara ya kudhibiti uchumi wake.
Ameitaja mipango hiyo kuwa ni
pamoja kudhibiti mfumko wa thamani ya dola dhidi ya shilingi ya
Tanzania, pamoja na kuimarisha sekta za kiuchumi zinazokwenda na wakati
kulingana na mabadiliko ya kiuchumi duniani.
Ameielezea sekta ya utalii kama
sekta kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar baada ya kuporomoka kwa zao la
karafuu, na kwamba jitihada zaidi zinafanywa kuiendeleza dhana ya utalii
kwa wote, ili kila mwananchi aweze kunufaika moja kwa moja na sekta
hiyo.
Maalim Seif amefahamisha kuwa katika kutimiza malengo yake ya kukuza
uchumi serikali inaendelea kuwahamasisha wawekezaji wa sekta ya utalii
kuja kuwekeza hasa katika ujenzi wa mahoteli yanayofikia hadhi ya “nyota
tano”.Aidha amesema serikali inakusudia kuimarisha ulinzi katika maeneo ya utalii, ili kuhakikisha kuwa watalii wanaokuja wanaishi kwa furaha na amani, na hivyo kuweza kuitangaza Zanzibar kiutalii duniani.
“Sekta ya utalii “is very
sensitive”, watalii wanaposikia vurugu kidogo tu hao wanakwenda zao, na
hapo kabla baadhi ya mapapasi walikuwa wakiwanyanyasa na wengine
kutishia usalama wa watalii, lakini sasa serikali inajipanga kuhakikisha
kuwa watalii wanaishi kwa usalama na kufurahia ziara zao nchini mwetu”,
alifafanua Maalim Seif.
Amesema chini ya mikakati hiyo serikali inalenga kupokea watalii
wapatao laki tano ifikapo mwaka 2015 ambao itakuwa ni ongezeko la
asilimia mia moja ya watalii wanaoingia nchi kwa sasa.Akizungumzia kuhusu kilimo. Makamu wa Kwanza wa Rais amesema serikali inaendelea vyema na mpango wake wa kilimo cha umwagiliaji ambapo wamekuwa wakishirikiana na washirika mbali mbali wa maendeleo ikiwemo Korea ya Kusini ambayo imekubali kusaidia uimarishaji wa miuondombinu ya umwagiliaji.
Ameongeza kuwa wakulima wengi wa
Zanzibar wameshajiika kuendeleza kilimo, baada ya serikali kuamua
kupunguza gharama za kilimo ikiwa ni pamoja na gharama za kulimia pamoja
pembejeo.
Kuhusu Uvuvi Maalim Seif amesema
sekta hiyo pia inapaswa kuendelezwa kwa vile inawagusa wananchi wengi wa
visiwa vya Unguja na Pemba, na ni miongoni mwa sekta zinazoweza
kuwakomboa wananchi kiuchumi.
Amesema kwa sasa wavuvi wanapaswa kujiandaa kwa uvuvi wa bahari kuu,
ambao mafanikio yake yatawahamasisha wawekezaji wa mazao ya baharini
kuja kuwekeza katika sekta hiyo na kuongeza pato la Taifa.Nae kiongozi wa ujumbe wa wanafunzi hao wanaojifunza masuala ya kiuchumi Brigedia General R. S. Laswai ameelezea matumaini yake ya kuendeleza kozi hiyo kwa mafanikio kufutia maelekezo na mashirikiano wanayoyapata kutoka kwa viongozi wa serikali.
No comments:
Post a Comment