Friday, January 4, 2013

Wachuuzi wachukiana na mamlaka, biashara katikati ya Nairobi

Antony Macharia anaichukulia njia ya waenda kwa miguu katika mtaa wa Ronaldo Ngara wa Nairobi kama ofisi yake.
  • Wachuuzi wakiuza vyombo kandokando ya barabara ya Moi katika mtaa wa biashara katikati ya Nairobi. Wachuuzi aghalabu hutumia mitaa hiyo wakati wa jioni, wakisababisha msongamano wa magari barabarani. [Bosire Boniface/Sabahi]
Kinjia kilichonyooka kwa umbali wa kilometa moja kandokando ya mtaa katika Wilaya ya Biashara ya Katikati ya Nairobi (NCBD) imejazwa na wachuuzi wanaouza bidhaa mbalimbali kutoka saa 10.00 jioni wakati ofisi zinapofungwa hadi kuzidi saa 4.00 usiku.
Macharia amekuwa akiuza viatu mahali hapo kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu kusaidia familia yake ya watu wanne. Biashara hii imenipa fursa ya kununua sehemu ya ardhi na gari, pamoja na kusomesha watoto wangu na kusaidia wanafamilia wengine," aliiambia Sabahi.
Hata hivyo, Macharia na wachuuzi wengine hawaruhusiwi kisheria kuuza bidhaa zao hapo.
Mary Wekesa, mwenye umri wa miaka 34 na mama wa watoto watatu ambaye anauza njegere, alisema polisi wa jiji hutumia mbinu zisizopendeza kutekeleza kanuni ambazo zinazuia wamachinga mitaani kutokufanya biashara katika NCBD.
"Maofisa wa polisi na viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Nairobi walitupiga, walikamata biashara zetu, na kutukamata kila walipotukuta katika maeneo yaliyozuiliwa," aliiambia Sabahi.
Alisema Soko la Wachuuzi la Muthurwa, ambako wachuuzi wanaruhusiwa kufanya biashara zao, ni mbali na katikati ya mji, na wafanyakazi wengi wa mjini hawako tayari kufunga safari kwenda huko.
Robert Kiriago, mrakibu mkuu mwandamizi wa Soko la Wachuuzi la Muthurwa, alisema serikali ilitumia shilingi milioni 700 (Dola milioni 8) kujenga soko hilo mwaka 2006 kwa maombi ya wachuuzi wa mitaani ambao walilalamika kuwa hawana sehemu iliyotengwa ya kufanyia biashara.
Soko limepanuliwa zaidi ya hekta 12 za ardhi mashariki pembezoni mwa mji na linahudumiwa na kituo cha mabasi.
"Miaka minne iliyopita lilianza vizuri, kwa kuwa wachuuzi wengi walifanya shughuli zao sokoni," aliiambia Sabahi. "Lakini katika miezi sita iliyopita, wachuuzi wameliacha soko kwenda kwenye njia za waendao kwa miguu katikati ya mji."

Mamlaka ya jiji inashughulikia kuzuia wachuuzi haramu

Tukio la tarehe 13 Disemba kati ya mamlaka ya jiji na watembezaji wa bidhaa za mikononi, wachuuzi wawili waliuawa na watu wengine kadhaa, ikiwa ni pamoja na polisi, walijeruhiwa baada ya maofisa wa polisi kuwazuia wachuuzi kadhaa waliokuwa wakifanya biashara zao kando ya River Road katikati ya jiji la Nairobi.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Chama cha Wachuuzi cha NCBD Stephen Waweru alisema polisi walitumia nguvu za ziada walipokuwa wakitimiza sheria inayozuia wachuuzi wa mitaani.
"Tunatambua kwamba uchuuzi katikati ya jiji ni kinyume cha sheria, lakini tunaiomba serikali kututengea maeneo ya mitaani kwa ajili ya kufanya biashara zetu kwa muda," alisema. Wauzaji hao wanaajiri zaidi ya watu 10,000, alisema, wengi kati yao wanaweza kugeuka kufanya shughuli za uhalifu.
Mtumishi wa Baraza la Manispaa ya Jiji la Nairobi Tom Odongo alisema viongozi wa jiji wanajaribu kuhimiza kukua kwa uchumi, lakini hata kama wachuuzi wanawakilisha sehemu muhimu ya uchumi, wanapaswa kufuata sheria na mipango.
Pamoja na msongamano ambao wachuuzi wanasababisha, kuna tatizo la afya kwa kuuza chakula mitaani, alisema. Mboga za majani na matunda vinawekwa hadharani katika vibamba, vinawekwa wazi katika vumbi na moshi wa injini. "Wanaacha karatasi za kufungia na mabaki ya mboga za majani kila sehemu katikati ya jiji na kuzifanya chukizo," aliiambia Sabahi.
Odongo alisema jiji linashughulikia changamoto zinazoikabili Soko la Wachuuzi la Muthurwa, kama vile maji, usafi na miundombinu, katika jitihada za kuwafanya wachuuzi kujisikia kutohitaji kuenea katikakati ya jiji.
Mkuu wa Polisi wa Eneo la Nairobi Moses Ombati aliiambia Sabahi kwamba msongamano unaosababishwa na wachuuzi unasababisha tishio la usalama. "Wachuuzi wanaendelea na matembezi ya pembezoni, kuwahatarisha wanaotembea kwa miguu wanaotakiwa kushindana na magari katika barabara kuu. Hili linasababisha msongamano wa barabarani," alisema.
Msongamano huo unaweza kuwapa wanamgambo kama vile wa al-Shabaab mazingira mazuri ya kuwapiga, alisema.

Madhara katika biashara halali

Wachuuzi wa mitaani pia wapo katika mgogoro na wafanyabiashara ambao wanawaona kuwa ni washindani wasio halali.
"Kuingia kwa wingi kwa wachuuzi kunasababisha ugumu miongoni mwa wafanyabiashara katikati ya jiji," alisema Timothy Muriuki, mwenyekiti wa Umoja wa NCBD. "Idadi yao kubwa inazidi wale wanaofanya biashara kwa uhalali katikati ya jiji. Wafanyabiashara wengi hawawapendi wachuuzi na wanataka mamlaka kutafuta suluhisho la kudumu."
Muriuki alisema wakati wa makabiliano na polisi, mali zinaharibiwa na biashara zinavurugwa katika mji, ambako kunaathiri shughuli muhimu za wamiliki wa biashara na wafanyakazi wao.
"Wafanyabiashara inabidi walipe kodi za majengo, leseni za biashara na ada nyingine za uendeshaji, lakini wachuuzi hawalipi chochote, kwa kuwa wanatembea," alisema Rajput Singh, mwenye duka kubwa katika Mtaa wa Tom Mboya ndani ya NCBD.
Hata hivyo, Sheila Atieno, mhudumu wa hoteli mwenye umri wa miaka 24, alisema ananunua vitu kutoka kwa wachuuzi wa mtaani katika wilaya ya biashara kwa sababu ni rahisi. "Inapofika saa 12.00 jioni, maduka yaliyo mengi yanakuwa yamefungwa na wachuuzi wananisaidia nisitembee zaidi ya kilometa mbili kwenda Soko la Wachuuzi la Muthurwa," aliiambia Sabahi.

No comments:

Post a Comment