Monday, February 4, 2013

AJALI MBAYA YASABABISHA VIFO VYA WATU WATANO MBEYA WIKI ILIYOPITA

SIRI ya ajali mbaya ya lori lenye namba za usajili T398 BSE, Scania Tipa iliyotokea wikiendi iliyopita katika Kijiji cha Mapogolo, Kata ya Itamboleo, Wilaya ya Mbarali mkoani hapa na kusababisha vifo vya watu watano na wengine 130 kujeruhiwa vibaya, imefichuka.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, lori lililopata ajali lililokuwa limebeba watu wengi, imevuja kuwa ni mali ya mwekezaji wa shamba la Kapunga Rice Project na lilikuwa limebeba vibarua wapatao 200, wenyeji wa Kijiji cha Kapunga waliokuwa wanakwenda kufanya kazi shambani kwake.
Ilidaiwa kuwa dereva wa gari hilo aliyejulikana kwa jina la Baraka Moleli, alikuwa akiliendesha kwa mwendo wa kasi na alikuwa akijaribu kuipita pikipiki huku abiria wake wakimshangilia.
Majeruhi na maiti walipelekwa katika Hospitali ya Mbarali ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alifika hospitalini hapo na kusema kuwa katika ajali hiyo wanaume wanne na mwanamke mmoja walifariki dunia na kati yao watatu wametambuliwa kuwa ni Samweli Mapugilo Mbena, 30, mkazi wa Ilembula, Bon Mfupa, 27, mkazi wa Mapogolo na Edger Mwakipesile, 35,  mkazi wa Nonde Mbeya.

No comments:

Post a Comment