Imewekwa na Mhammed khamis
Zaidi ya ekari 48 za msitu wa
Hifadhi wa Jozani zimeungua moto kufuatia moto uliozuka katika msitu huo
siku nne zilizopita, na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi bilioni
tatu.
Akizungumza wakati akitembelea
eneo hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
amesema tukio hilo ni la kusikitisha na limeitia hasara kubwa serikali
na taifa kwa ujumla.
Amesema mbali na hasara hiyo ya
kiuchumi lakini moto huo pia umesababisha athari kubwa za kimazingira
ambazo zinaweza kuchukua muda mrefu kuweza kurudi katika hali yake ya
kawaida.
Amewaagiza maafisa wa msitu huo
kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa hakuna watu
wanaotumia njia za kizamani katika uvunaji wa asali ili kuepuka athari
zaidi zinazoweza kujitokeza.
Maalim Seif amewataka wafugaji wa
nyuki kufuata maelekezo ya wataalamu wa Wizara ya kilimo na mali asili
ili kufuata njia za kisasa za uvunaji wa asali usiotumia moto ili
kudhibiti uharibifu katika misitu ya asili.
“Misitu yetu ya asili
tunayoitegemea zaidi ni huu wa Jozani kwa Unguja na ule wa Ngezi kwa
Pemba, ni wajibu wetu tuilinde na tuihifadhi kwa nguvu zetu zote ili
isitoweke”, alisisitiza Makamu wa Kwanza wa Rais.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa
Maliasili Dkt. Bakari Assedi amesema chanzo cha moto huo kinasadikiwa
kuwa ni wavunaji wa asali wanaotumia njia za zamani za kutumia moto.
Amesema msitu huo wa asili ambao
pia ni hifadhi ya taifa, ni muhimu katika kulinda na kuhifadhi misitu
na viumbe adimu ambapo kwa wastani kila baada ya miaka 15 kupatikana
kiumbe kipya katika msitu huo.
Amesema Wizara ya Kilimo na
Maliasili imekuwa ikiwashajiisha wafugaji wa nyuki kushirikiana na
Wizara hiyo kwa kupata utaalamu, na kwamba iko tayari kushirikiana nao
na kuwapatia nyenzo katika jitihada za kuendeleza ufugaji wa nyuki wa
kisasa.
Msitu huo pia ni muhimu kwa
shughuli za kitalii ambapo watalii kutoka nchi mbali mbali hufika katika
msitu huo kwa ajili ya kujionea wanyama adimu duniani wakiwemo ‘kima
punju’.
Dkt. Assedi amesema moto huo unaotarajiwa kumaliza kuzimwa hii leo umeathiri zaidi miti aina ya Mikaratusi na Mitondoo.
Mapema akizungumza na wapiganaji
wa kikosi cha zimamoto na uokozi katika eneo hilo, Maalim Seif
amewapongeza kwa juhudi zao za kuudhibiti moto huo licha ya kukabiliwa
na mazingira magumu.
Amesema serikali inathamini sana
mchango wao katika harakati za kuzima moto na uokozi, na kwamba
itashirikiana na kikosi hicho kwa kukipatia nyenzo zaidi ili kiweze
kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Amewataka wapiganaji hao kuandaa mbinu zaidi za kukabiliana na maafa yoyote yanaoweza kujitokez
No comments:
Post a Comment