Wednesday, February 13, 2013

MAJINA YA WALIOCHAGULIWA KAMATI KUU CCM

 
 
 
 
 
 
Rate This


Wakati wa upigaji kura
Wakati wa upigaji kura
WAZIRI Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim ameibuka kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama, Jakaya Kikwete na kisha kuridhiwa na wajumbe wa NEC.

Dk Salim amekuwa miongoni mwa wajumbe 14 wa Kamati Kuu waliochaguliwa juzi usiku kwenye mkutano wa NEC mjini Dodoma katika kinyang’anyiro kilichohusisha majina ya watu 42 waliopaswa kupigiwa kura. Majina 21 yalikuwa ni kutoka Bara na 21 wengine wa Zanzibar.
Hata hivyo Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alipozungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, hakuweka hadharani majina yote 42 yaliyopigiwa kura.
Nape alisema NEC iliridhia uteuzi wa Dk Salim kuwa Mjumbe wa NEC kupitia nafasi 10 za uteuzi wa Mwenyekiti wa CCM. Baada ya kuridhiwa, aliingizwa kwenye kinyang’anyiro cha wajumbe wa Kamati Kuu.
Kwa mujibu wa Nape, Mwenyekiti wa Taifa anazo nafasi 10 za uteuzi ambazo kati ya hizo, nne aliziteua wakati wa kuunda Sekretarieti zikabaki sita. Hivyo uteuzi huo wa Dk Salim umefanya zibaki nafasi nne ambazo yeye ndiye anajua ni lini atazijaza.
Kati ya wajumbe 14 waliochaguliwa kwenye Kamati Kuu, saba ni kutoka Bara na saba wengine ni wa Zanzibar. Kwa upande wa Bara ni Dk Emmanuel Nchimbi, Profesa Anna Tibaijuka, Steven Wasira, William Lukuvi, Adam Kimbisa, Jerry Silaa na Pindi Chana.
Kwa upande wa Zanzibar, pamoja na Dk Salim walioshinda ni Shamsi Vuai Nahodha, Dk Hussein Mwinyi, Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, Dk Maua Daftari, Samia Suluhu Hassan na Hadija H. Aboud. Ingawa Nape hakutaja idadi kamili ya wajumbe wote wa Kamati Kuu , chombo hicho muhimu cha maamuzi pamoja na wajumbe hao 14 wa kuchaguliwa, wengine ni wanaoingia kutokana na nyadhifa zao.
Nao ni Mwenyekiti wa Taifa pamoja na makamu wake wawili kutoka Bara na Visiwani, Katibu Mkuu, Manaibu wawili wa chama na wajumbe wa Sekretarieti.
Sekretarieti inahusisha Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Katibu wa Siasa Mambo ya Nje na Katibu wa Oganaizesheni, Katibu wa Fedha na Uchumi.
Wengine wanaoingia kutokana na wadhifa wao ni Waziri Mkuu, spika wa Bunge la Muungano na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar.
Aidha wengine wanaoingia kwenye chombo hicho cha maamuzi ni wenyeviti wa jumuiya za vyama, Katibu wa Wabunge wa CCM na Katibu wa Baraza la Wawakilishi wa CCM.
Kuhusu mambo mbalimbali yaliyotokana na mjadala na semina alisema yatatolewa baadaye. Alisema Kamati Kuu imekaa jana katika kikao chake cha kwanza.

No comments:

Post a Comment