"Sifikirii kuwa uongezaji huo uondolewe kwa nafasi zote, lakini unapaswa kuzuiwa kwenye taaluma za kiufundi," mbunge David Kafulila aliiambia Sabahi.
Alisema maprofesa wa chuo kikuu, madaktari, wauguzi, marubani na watu katika uga unaohitaji maarifa ya kiufundi wanapaswa kuwa ndio wafanyakazi raia tu wanaostahili mkataba wa kuongezewa muda wa kazi kupita ule umri wa kustaafu.
Katibu Mkuu, wakurugenzi wa idara na wafanyakazi wengine wa utawala, kwa upande mwingine, wanapaswa kustaafu kazi wakiwa na umri wa miaka 60 kama ilivyoamuliwa kisheria, alisema, akiongezea kwamba uongezaji wa muda aghalabu hutolewa kwa upendeleo na siyo kwa sifa. "Kwa hakika tunahitaji kupitia tena sheria ili kushughulikia matatizo haya kwa haraka."
Kulingana na data kutoka kwenye Utafiti wa Sera kwa Maendeleo ya Taasisi Tanzania, vijana milioni 3.5 waliingia katika utumishi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, lakini ni kazi mpya milioni 1 tu zilizopatikana kwa ajili yao.
Mbunge Tundu Lissu alisema serikali imekuwa haifanyi vizuri pale linapokuja suala la kutoa kazi mpya kwa Watanzania wanaoingia katika utumishi, na kuchelewesha umri wa kustaafu kunazidisha tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.
Ingawaje Tanzania iliingia katika mfumo wa soko huria mwaka 1987, bado kuna makampuni mengi yanayomilikiwa na serikali katika tasnia mbalimbali na serikali inabakia kuwa mwajiri mkuu katika nchi.
"Kwa kuwastaafisha wale wanaofikia miaka 60, [serikali] inaweza kuzalisha ajira zaidi kwa kizazi cha vijana," aliiambia Sabahi.
Hata hivyo, Celina Kombani, waziri wa nchi katika ofisi ya rais, utumishi wa umma, alisema uongezaji wa mkataba unatolewa kulingana na sifa, na serikali inapaswa kuwa na uwezo wa kuweka matarajio yanayozingatia mahitaji ya nchi.
"Baadhi ya wafanyakazi wanaweza kuwa hawako katika idara za kiufundi, lakini wanaweza kuwa wameanzisha miradi muhimu kwa ajili ya nchi ambayo inahitaji uangalizi wao wa karibu ili iweze kuendelea," Kombani aliiambia Sabahi. "Kwa hiyo, mazingira kama hayo yanatulazimisha kuongeza kipindi chao na tutaendelea kufanya hivyo."
Kuhamishia uzalishaji wa ajira katika sekta binafsi
Benson Mahenya, mchumi na mkurugenzi wa Andrew's Consulting Group, alisema Watanzania wanapaswa kuacha kuifikiria serikali kama mwajiri pekee nchini."Kufikiria kwamba serikali inaweza kuajiri kila mhitimu wa chuo hakuna mantiki," Mahenya aliiambia Sabahi.
Alisema wahitimu wapya wa chuo kikuu wanaweza kuwa wajasiriamali kwa kuwekeza katika biashara ndogondogo ambazo zinahitaji mtaji mdogo. "Wahitimu wa chuo kikuu wanapaswa kuelekeza elimu zao katika kujiajiri," alisema. "Ni sekta binafsi tu inayoweza kuchukua wahitimu wa vyuo vikuu walio wengi."
Mahenya pia alipendekeza kwamba wafanyakazi wapya wajitolee katika taasisi mbalimbali na wizara ili kuongeza uzoefu unaotakiwa.
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Makongoro Mahanga alikiri kwamba sera kuhusu ajira za serikali zinahitaji kuboreshwa.
"Nadhani mtu anapofikia umri wa miaka 60, anapaswa kustaafu," aliiambia Sabahi. "Nimesikia malalamiko [kuhusu kuongeza muda], na sikusudii kukosoa serikali yangu hapa, lakini mnajua serikali ina njia yake ya kurekebisha sheria, muda utakapofika itarekebishwa."
Mahanga alisema serikali inashughulikia kutatua tatizo la kukosekana kwa ajira kwa kuhamasisha wawekezaji binafsi. "Serikali inawajibika sana kuhusiana na hili," aliiambia Sabahi. "Tumepitisha sheria ya ubia wa serikali na watu binafsi, ambayo inakamilisha jitihada za serikali kuongeza uwekezaji na kisha kuanzisha ajira nyingi zaidi."
Nafasi ya kupata uzoefu
Stanley Kahangwa, mwenye umri wa miaka 27, aliyehitimu shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema hajapata kazi kwa miaka mitatu tangu alipohitimu."Serikali inapaswa kuhamasisha mpango wa mafanikio," Kahangwa aliiambia Sabahi, akiongeza kwamba vijana wanapaswa kupewa fursa ya kufanya kazi na waajiriwa wa serikali wenye uzoefu kabla hawajastaafu kama njia ya kuhamisha ujuzi kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Didier Wilson, mwenye umri wa miaka 26 aliyehitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema anauza matufaha katika Barabara ya Nyerere huko Dar es Salaam. Alihitimu katika masomo ya utawala wa umma mwaka 2010, lakini hajafanikiwa kupata kazi ya kudumu.
"Matumaini yangu yalikuwa makubwa [baada ya kuhitimu], lakini kila ofisi niliyokwenda na karibia matangazo yote ya kazi yanahitaji uzoefu wa miaka mitano hadi saba, ambao sina," alisema. "Kwa hiyo nilijisemea mwenyewe, 'Wacha nijaribu kuuza matufaha, ambayo hayahitaji uzoefu.' "
No comments:
Post a Comment