
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif akizungumza na ujumbe
wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Ujerumani ofisini kwake Migombani.
Ujumbe wa Kamati ya Bunge la
Ujerumani umeelezea kuridhishwa kwake na matumizi mazuri ya misaada
wanayoitoa katika hatua za kusaidia miradi ya maendeleo nchini.
Kiongozi wa Ujumbe huo Bw. Clouse
Peter Willsch ameeleza hayo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake Migombani.
Ujumbe huo ambao upo nchini kwa
ajili ya kukagua miradi inayofadhiliwa na serikali ya Ujerumani katika
maeneo ya jeshi, umepata fursa ya kutembelea hospitali ya Lugalo jijini
Dar es Salaam na hospitali ya Bububu iliyopo Zanzibar, na kuelezea
kufarajika kwake na matumizi ya misaada hiyo.
Bw. Clouse amesema Ujerumani
itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika maeneo mbali mbali na
kusaidia juhudi za serikali katika kubabiliana na maafa.
Ameahidi kuziangalia kwa karibu
fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar ikiwa ni pamoja na sekta ya utalii
na viwanda vidogo vidogo, ili kuona namna ya nchi hiyo kuweza kuwekeza
katika maeneo hayo.
Mapema Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameueleza ujumbe huo kuwa Zanzibar
ni mahali salama pa kuwekeza, na kwamba zipo fursa nyingi na mazingira
salama kwa ajili ya uwekezaji.
Ameelezea matumaini yake kuwa
ujio wa ujumbe huo wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Ujerumani utasaidia
kuitangaza Zanzibar pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya Zanzibar na
Ujerumani.
Amesifu mchango wa Ujerumani kwa
Zanzibar ambapo imekuwa ikisaidia harakati za maendeleo katika sekta
mbali mbali ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa hospitali ya Bububu ambayo
iko chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Wakati huo huo Maalim Seif
amekutana na Balozi wa Cuba nchini Tanzania balozi Jorge Luis Tormo, na
kuelezea matumaini yake juu ya kuendelea kwa mashirikiano katika sekta
za biashara na kilimo.
Amesema Zanzibar na Cuba zinaweza
kushirikiana katika maeneo hayo kutokana na nchi hiyo kuwa na uzoufu
mkubwa katika masuala hayo, na kwamba kufanya hivyo kutaongeza maeneo
mapya ya ushirikiano baina ya nchi mbili hizi.
Cuba imekuwa ikishirikiana na
Zanzibar kwa kipidi kirefu hasa katika sekta ya afya ambapo imekuwa
ikituma wataalamu wake nchini pamoja na kuanzisha chuo kwa ajili ya
kuwafundisha madaktari wa Zanzibar.
Maalim Seif ameiomba Cuba kuangalia uwezekano wa kusaidia matibabu kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar nchini Cuba, ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif akiwa katika picha ya
pamoja na ujumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Ujerumani baada ya
mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwake Migombani.
Nae Balozi Luis Tormo amesema
yapo maeneo mengi ambayo Cuba inaweza kushirikiana na Zanzibar, na
kuahidi kupeleka mapendekezo yake nchi Cuba ili waweze kuyafanyia kazi.
Amesema kuna umuhimu wa kipekee
wa kuendeleza mashirikiano katika maeneo mengine ya kiuchumi, hatua
ambayo itakuza mashirikiano baina ya Cuba na Zanzibar.
Hassan Hamad (OMKR)
No comments:
Post a Comment