Tuesday, February 26, 2013

Zanzibar yasaka maoni kufeli kidato cha nne

wanafunzi

 
 
 
 
 
 
Rate This

Wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar imeamua kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya kadhia ya matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne, cha pili na darasa la saba. Naibu Waziri Wizara hiyo, Zahra Ali Hamadi, alisema hayo katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi waliofaulu darasa la saba katika shule ya Jadidida Wete mkoa wa kaskazini Pemba.
Aliwataja wadau hao kuwa ni pamoja na wajumbe wa kamati za shule, mabaraza ya wanafunzi pamoja na walimu ili kupata maoni yenye lengo la kutatua tatizo hilo.
Mh,Waziri  alikiri kuwa matokeo ya mwaka jana ni mabaya mno na pigo kubwa kwa wanafunzi, wazazi na walimu na akadai kuwa ni vema ikatafutwa njia ya kudumu kukomesha jambo hilo ili kunusuru taifa la baadaye.
“Sababu ziko nyingi kutokana na matokeo kuwa mabaya na serikali ya Muungano imetangaza kuunda tume ya kuchunguza kadhia hiyo na kitakachoonekana na tume kitafanyiwa kazi ili kuondosha aibu ya kushuka kwa ufaulu wa kila mwaka,’ alisema.
Aliwataka wanafunzi waliofaulu kutotosheka na kiwango hicho bali wajitahidi kutafuta elimu zaidi kwa faida yao na taifa kwa ujumla.
Aliwataka walimu na wazazi kushirikiana kwa karibu ili kuleta maendeleo ya jamii pamoja na kila mmoja kujua wajibu wake.
Shule ya Jadida ilianzishwa mwaka 1954 ambapo walengwa wakuu walikuwa ni kabila la Kihindi hadi mwaka 1964 ilipoingia katika mikono ya Serikali ya Mapinduzi. Katika matokeo ya mwaka huu jumla ya wanafunzi 50 wa darasa la saba wamejiunga na darasa maalumu la michepuo.

No comments:

Post a Comment