Friday, March 29, 2013

Muuwaji wa Padri Mushi Zanzibar akamatwa.

Jeshi la Polisi Zanzibar limefanikiwa kumtia mbaroni kijana mmoja anaejulikana kwa jina la Omar Mussa Makame mkaazi wa Mwanakwerekwe mwenye umri wa miaka 35 kwa tuhuma za mauwaji ya Padri Mushi alieuwawa kwa risasi siku ya tarehe 17\2\2013 maeneo ya Betras Zanzibar wakati akiwa kwenye harakati za kuhudhuria ibada.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Bwana Mussa Ali Mussa amesema kuwa kukamatwa kwa mtu huyo kumekuja baada ya Jeshi hilo kwa kushirikiana na FBI kuchora mchoro wa mhusika wa tukio hilo ambapo waliweza kuchora mchoro huo baada ya kupata maelezo tosha kutoka kwa watu walioshuhudia kuwawa kwa Padri Mushi na ndio wao wakachoro mchoro halisi wa mauwaji hayo.

Aidha Kamishna Mussa amesema kuwa hatuwa ya kufanikiwa kumkamata kijana huyo imekuja baada ya wao kutoa mchoro sehem mbali mbali zikiwemo mitandao mbali mbali ya kijamii na ndipo wakatokea wasamaria wema na kusema kuwa kwa mujibu wa picha iliotolewa basi wao wanamjua mtu huyo na ndipo walipotoa taarifa ambazo zilifanikisha Jeshi hilo kumtia mbaroni kijana huyo.

Hata hivo Kamishna amesema kuwa hawakuridhika tu kutokana na ushahidi huo badala yake wao kama jeshi la Polisi walifanya gwaride maaalumu la utambuzi kwa kuwakushanya watu walioshuhudia tukio zima na kusema kuwa ni kweli aliekamatwa ndie mhusika mkuu wa mauwaji ya Padri Mushi.

Pamoja na hayo kamishna amefahamisha kuwa kwa sasa wanasubiri file la mtuhumiwa huyo litoke kwa mkurugenzi wa mashtaka ili waweze kumfikisha mtuhumiwa huyo katika vyombo husika.

Sambamba na hayo kamishna Mussa ametowa wito kwa jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuondoa uhalifu Nchini kwetu.

No comments:

Post a Comment