Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na
wananchi wa Shehia ya shidi Jimbo la Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba
mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Jengo la skuli yao mpya
inayojengwa katika eneo hilo.
Tabia
ya kuendeleza tamaa iliyosheheni ndani ya vichwa vya baadhi ya Wazazi
ya kuwaozesha waume watoto wao wa Kike wakiwa bado wanaendelea na masomo
yao inapaswa kuachwa mara moja ili kujengewa ustawi bora watoto hao kwa
maisha yao ya baadaye.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo mara baada ya kuweka
jiwe la msingi la Jengo la Skuli mpya ya Shehia ya Shidi Jimbo la
Mkanyageni Mkoa kusini pemba wakati akizungumza na Wazazi, Walimu na
wanafunzi wanaoishi katika eneo hilo.
Balozi
Seif akionyesha furaha yake kutokana na juhudi kubwa zilizochukuliwa na
Wananchi wa shehia hiyo za kujiletea maendeleo ya Elimu kwa ujenzi wa
Skuli hiyo alisema tabia hii mbaya inayoonekana kuendelea kufanya na
baadhi ya wazazi inachangia kuviza maendeleo ya familia na hata Taifa
kwa ujumla.
Alisema
bado jamii inapaswa kuendelea kuwekeza katika Sekta hii muhimu ya Elimu
sambamba na wazazi kufuatilia nyendo za watoto wao kwa lengo la
kuhakikisha kizazi hicho kinajengewa mazingira madhubuti ya kuja kutoa
huduma kwa wananchi katika njia ya Kitaalamu.
“
Huu ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na wana Shidi katika kuwajengea
mazingira mazuri ya kielimu watoto wao na ni vyema mkajitahidi zaidi
katika miradi ya maendeleo ambayo haihusiani na itikadi za kisiasa”.
Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza wananchi hao wa Shehia ya
Shidi kwa uwamuzi wao wa kujisogezea miradi muhimu ya maendeleo na
katika kuunga mkono juhudi hizo ameahidi kusaidia Bati hamsini kuungana
na wale waliojitolewa kuchangia ujenzi huo ili kukamilisha kiwango
kamili kinachohitajika katika uwezekaji wa Skuli hiyo.
Ameishauri
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kufikiria kutoa upendeleo
Maalum kwa Jengo hilo jipya ambalo kukamilika kwake kutawaondoshea
usumbufu watoto wa kijiji hicho wanaolazimika kuvuka kwa kufuata elimu
masafa marefu.
“
Tunaelewa jukumu kubwa lililonalo Wizara ya Elimu katika kukamilisha
Majengo ya Skuli yaliyojengwa na Wananchi wenyewe kwa njia ya kujitolea
lakini wanapaswa kulifumbia macho hili la Shidi kutokana na uzito wake”.
Alifafanua Balozi Seif.
“
Zipo skuli nyingi hapa nchini ambazo zinaendelea kujioongeza majengo
mengine mapya kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya ongezeko la watoto wao.
Lakini hili la Shidi jipya na ndio kwanza wameanza kuanzisha skuli sasa
Wizara ya Elimu inapaswa kuliona hili”. Aliongeza Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar.
Akimkaribisha
Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Kanal Mstaafu Juma Kassim
Tindwa alisema Wananchi wa Shehia ya Shidi hawajakosea kuwekeza katika
Sekta ya Elimu kwani haypo ndio miongoni mwa malengo makubwa ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Katika
Risala yao wananchi hao wa Kijiji cha Shidi Wilaya ya Mkoani ambayo
iliosomwa na Mwalimu Rajab Abdulla Tamim alisema chimbuko la ujenzi wa
Skuli hiyo limetokana na Jumuiya ya Mazingira ya Mimka kwa kuwamua kutoa
changamoto ya mifuko kumi ya saruji kwa wananachi hao.
Mwalimu
Rajab alisema wananchi wa Shidi walifikia kuhamasika na kuanza harakati
za ujenzi mwaka 2004 ambapo hadi sasa likifikia hatua ya kukamilika kwa
linta jingo hilo limeshafikia gharama ya zaidi ya shilingi milioni
10.6.
Watoto
wa Kijiji cha Shidi kiliopo Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba hivi
sasa wanalazimika kufuata elimu zaidi ya masafa ya kilomita mbili na
tatu katika skuli za Ng’ombeni na Mkanyageni hali ambayo inaleta
usumbufu kwa wale wanaoanza darasa la kwanza.
No comments:
Post a Comment