Thursday, April 4, 2013

Korea Kaskazini nayo inajiandaa kukabiliana na vita hivyo hatari vinavyotarajiwa kuanza muda wowote

 
 
 
 
 
 
Rate This


MAREKANIMarekani imepeleka ndege za kivita Korea Kusini kwa lengo la kusisitiza dhamira yake ya kuisaidia nchi hiyo.Imedaiwa kwamba msaada huo unaotolewa na Marekani kwa nchi hiyo ni msaada wa kijeshi  dhidi ya vitisho vya Korea Kaskazini.


Ndege hizo aina ya F-22 zinadaiwa  kupelekwa kwenye ngome ya kikosi cha anga huko Osan, ngome kuu ya kikosi cha anga cha Marekani nchini Korea Kusini.
Hata hivyo, Marekani haijasema ilipeleka ndege ngapi za kivita Korea Kusini kutoka kwenye ngome yake ya kikosi cha anga cha Okinawa, Japan.
Wasiwasi uliongezeka tangu kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un kuamuru jaribio la silaha za nyuklia mwezi Februari, mwaka huu.
Wiki iliyopita  Korea Kaskazini ilisema kuwa inaingia katika vita na Korea Kusini, katika mwendelezo wa vita vya maneno dhidi ya utawala mjini Seoul na Washington.
Hii ni baada ya kuwekewa vikwazo vya kimataifa kufuatia jaribio lake la silaha za nyuklia.Shirika la Habari la Korea Kaskazini KCNA, lilitoa taarifa inayosema kuwa kuanzia sasa, uhusiano wa Kaskazini na Kusini utaingia katika hali ya vita, na kwamba masuala yote yanayojitokeza kati ya pande hizo yatashughulikiwa ipasavyo.
Tangu mwanzoni mwa mwezi huu Korea Kaskazini ilikuwa ikitishia kila siku kuishambulia Korea Kusini pamoja na kambi za kijeshi za Marekani.
Vitisho hivi vinakuja baada ya Marekani na Korea Kusini kuanzisha mazoezi ya kawaida ya kijeshi, na imeyaamrisha majeshi yake kukaa kwa tahadhari na kuwa tayari kushambulia wakati wowote.
Korea Kaskazini ilitoa tishio jipya kuishambulia Marekani, baada ya ndege mbili za Marekani chapa B-2 zenye uwezo wa kubeba makombora ya nyuklia kufanya mazoezi nchini Korea ya Kusini.
Tishio la Korea Kaskazini la kuingia vitani na Korea Kusini kumezusha wasiwasi mkubwa katika rasi ya Korea.
Wiki iliyopita  Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un aliamuru jeshi lake kujitayarisha kufuatia hatua ya Marekani na Korea Kusini kukataa kufuta mazoezi ya kijeshi ya kiwango kikubwa yaliyopangwa kufanywa kwa pamoja na nchi hizo mbili.
Kiongozi huyo alionya kuwa nchi yake iko tayari kukabiliana na nchi hizo mbili baada ya ndege hizo mbili za kijeshi za Marekani kupeleka kundi la majeshi nchini Korea Kusini.
Pyongyang inahofiwa kuwa hatua ya nchi hizo mbili – Marekani na Korea Kusini inanuia kufanya uvamizi wa kijeshi ndani ya nchi yake.
Hata hivyo tayari wachambuzi nchini humo walisema ghasia kamili zikiibuka itakuwa ni njia moja ya Pyongyang kujimaliza yenyewe.
Wachambuzi hao  pia walisema vitisho hivi vinanuia kuishawishi Marekani kuingia katika meza ya mazungumzo, kumhimiza Rais mpya wa Seoul kubadilisha sera yake dhidi ya Korea Kaskazini na kujenga umoja ndani ya nchi bila ya kutishia vita vikubwa kati ya Kusini na Kaskazini.

No comments:

Post a Comment