Wednesday, April 3, 2013

Maafisa wa Somalia waahidi kuboresha haki za binadamu kufuatia ripoti ya ubakaji

Serikali ya shirikisho ya Somalia iliahidi kuchukua hatua baada ya ripoti ya Shirika la Usimamizi wa Haki za Binadamu (HRW) kudadi kuwa watu wa vikosi vya serikali vya usalama vilikuwa vikifanya ubakaji na unyanyasaji mwengine katika makambi dhidi ya watu wa ndani waliokimbia makazi yao mjini Mogadishu.
  • Mwanamke wa ndani wa Kisomali aliyekimbia makazi yake akiwa amebeba mtoto katika kambi ya Hamarweyn huko Mogadishu mwezi Septemba 2012. Wanawake na wasichana wanaoishi katika makambi kama hayo wako katika hatari ya kubakwa, kushambuliwa na unyanyasi wa aina nyingine unaofanywa na watu wa vikosi vya usalama, Shirika la Usimamizi wa Haki za Binadamu liliripoti mwezi uliopita.  [Na Simon Maina/AFP] Mwanamke wa ndani wa Kisomali aliyekimbia makazi yake akiwa amebeba mtoto katika kambi ya Hamarweyn huko Mogadishu mwezi Septemba 2012. Wanawake na wasichana wanaoishi katika makambi kama hayo wako katika hatari ya kubakwa, kushambuliwa na unyanyasi wa aina nyingine unaofanywa na watu wa vikosi vya usalama, Shirika la Usimamizi wa Haki za Binadamu liliripoti mwezi uliopita. [Na Simon Maina/AFP]
"Nimesema hadharani na ninasisitiza juu ya ahadi yangu binafsi ya kurejesha usalama nchini Somalia na kuwawajibisha wale watakaoonekana na makosa ya ukiukwaji wa haki za binadamu," Raisi wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisema katika taarifa.
"Changamoto tunazokabiliana nazo katika kujenga upya taifa letu ni kubwa na usalama wa raia na kijeshi unabakia kuwa kipaumbele chetu kikubwa," alisema. "Zaidi ya hayo, mchakato wa kuzikarabati asasi zetu za usalama umeanza ili kushughulikia masuala kama vile ya nidhamu na utaalamu."
Ripoti ya HRW ilitolewa miezi minne baada ya Mahmoud kutoa onyo kwa vikosi vya serikali. " Askari yeyote atakayembaka mtu utauliwa," raisi alisema hapo mwezi Novemba.
Katika ripoti yake ya mwezi Machi, HRW ilisema kuwa wanaume wa kijeshi wakiwa na sare wamekuwa wakifanya uvamizi wa kingono nyakati za usiku wakiwalenga wanawake na wasichana wasio na ulinzi makambini.
HRW ilitoa wito kwa serikali ya Somalia kuimarisha haraka usalama wa watu wa ndani waliokimbia makazi yao (IDPs) na kuleta haki kwa watu wa usalama wanaodaiwa kubaka au kufanya unyanyasaji mwingine dhidi ya IDPs.
Waziri Mkuu Abdi Farah Shirdon alisema kuwa kuimarisha haki za binadamu nchini Somalia ni moja ya vipaumbele vya serikali mpya.
"Somalia inatarajia kujiunga na Tume ya UN ya Haki za Binadamu na hiyo maana yake ni kuwa tunapaswa kujaribu kuimarisha rekodi zetu na kukuza haki za binadamu katika kila kitu tunachofanya, alisema hapo tarehe 20 Machi kufuatia mkutano na Mtaalamu Huru wa Haki za Binadamu nchini Somalia Shamsul Bari.
Majira ya kiangazi hiki, serikali ya Somalia itafuata mpango wa haki za binadamu na kutangaza kurugenzi kuu ya haki za binadamu, haki za wachache na utawala wa sheria, Shirdon alisema.

Tume huru yaundwa

Mwezi Februari, serikali iliunda tume huru ya watu 13 ili kufuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu.
"Uamuzi wa kuunda tume huru ya haki za binadamu ulifanywa ili kushughulikia woga unaohusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wanawake," Mohamud alisema. "Sote tunafahamu vyema uwajibikaji wa pamoja ili kuzuia ukiukwaji wa haki za binadamu."
Mariam Yusuf, ambaye anaongoza kamati hiyo, aliwahakikishia Wasomali na washirika wa kimataifa kwamba wajumbe wa kundi lake wanaelewa juu ya jukumu lao kubwa sana, "Tuko makini sana katika kuendesha misheni hii na tunadhamiria kikamilifu ufanyaji wa uchunguzi huru juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu," alisema.
"Somalia imeshuhudia hali ya kutengana na mtikisiko wa ndani wa zaidi ya miongo miwili iliyopita, na kusababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa," aliiambia Sabahi. "Kukosekana kwa utawala wa sheria na usalama katika maeneo makubwa ya nchi katika miaka michache iliyopita imeunda mazingira ambapo makundi yaliyo katika mazingira magumu ya jamii ndio walengwa."
Abdirahman Hassan, afisa katika shirika la haki za binadamu la "Mstari wa Amani, alisema kuwa juhudi za serikali zinafanyakazi.
"Ubakaji ni tatizo kubwa jijini, lakini kwa zaidi ya miezi minne iliyopita -- baada ya uamuzi wa raisi kumuua askari yeyote ambaye atahukumiwa kwa ubakaji -- kesi za ubakaji zimepungua," alisema.
"Ingawaje sehemu kubwa ya jamii iliyo katika mazingira magumu, wakiwemo wanawake na watoto, bado wanakabiliwa na ukiukwaji, serikali imeshachukua hatua kadhaa ndani ya kipindi kifupi ili kuimarisha hali ya haki za binadamu nchini na kushughulikia ukiukwaji unaofanywa na [vikosi vya] usalama" aliiambia Sabahi.
"Tunasifia hatua zilizochukuliwa na serikali za kuunda tume huru ya kusimamia asasi za haki za binadamu, na tunaiomba serikali kuunda taasisi ya haki za binadamu pamoja na asasi za mahakama kwa ajili ya kuimarisha haki za binadamu nchini," alisema.
Serikali ya Somalia bado ina njia ndefu, kabla ya kuanzisha viwango vya msingi vya haki za binadamu, alisema mwanaharakati wa haki za binadamu Mohamed Ali alisema.
"Tunaitolea wito serikali kutafsiri ahadi zake katika utaratibu unaoonekana wa utekelezaji kunakohusika na kwa kufuata njia na mkakati wa haki za binadamu ambayo imetangaza," aliiambia Sabahi.

No comments:

Post a Comment