Tuesday, April 2, 2013

Nahodha: Zanzibar ina ufisadi wa kutisha

 
 
 
 
 
 
Rate This

nahodhaWAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, amesema Zanzibar inakabiliwa na ufisadi wa kutisha unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji kwa kurudisha nyuma maendeleo ya kiuchumui visiwani humo.Nahodha ambaye pia ni Waziri Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye viwanja vya Mzalendo Mkoa wa Mjini Magharibi jana. Alisema ufisadi huo umejikita katika sekta ya ardhi, mali za serikali yakiwemo majengo ya umma na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).
Nahodha alisema kuwa kwa bahati mbaya wahusika wa vitendo hivyo bado wanafumbiwa macho huku baadhi yao wakitumia siasa za Muungano kuficha uovu wao.
Alisema karibu sh bilioni 20 zimetoweka katika Shirika la Umeme Zanzibar na hadi sasa hakuna aliyekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Zanzibar inakabiliwa na matatizo makubwa ya matumizi mabaya ya ardhi, bahati mbaya waliofanya hayo wanaendelea kulindwa bila ya kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
Nahodha alikuwa miongoni mwa wana CCM waliojitokeza kushindana na Rais wa sasa Dk. Ali Mohammed Shein kuomba kuteuliwa kuwania kiti hicho mwaka 2010.
Vilevile amekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar kwa miaka 10 chini ya utawala wa Rais Amani Abeid Karume, jambo ambalo linatafsiriwa kuwa kauli hiyo inailenga serikali ya sasa ya Dk. Shein.
Aliwataka wananchi kuwa macho na viongozi wenye huruma ya mamba wakionekana kukaza misuli ya kutetea maslahi ya Zanzibar kumbe wao ndiyo wanaoitafuna na kuwabebesha ukali wa maisha wananachi.
Nahodha amelipua bomu hilo la ufisadi huku serikali ikiwa imebanwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kushindwa kutekeleza ripoti tatu za uchunguzi ambazo zimebaini ubadhirifu mkubwa wa mali za umma katika Shirika la Umeme Zanzibar na kuuzwa kwa majengo ya hifadhi ya mji wa urithi wa dunia kinyume cha sheria ya manunuzi ya serikali ya mwaka 2005.
Uchunguzi mwingine ulihusu majengo yaliyochukuliwa kinyume cha sheria na mengine kuuzwa kwa wawekezaji kwa bei poa yakiwemo yale ya kihistoria ya Mambo Msiige, jumba la yatima Forodhani na yaliyokuwa makao makuu ya Wizara ya Elimu Zanzibar.
Akishangiliwa na umati wa wanachama wa CCM, Nahodha alionya ukimya wa wananchi akisema si wajinga bali wanatoa nafasi kwa vyombo husika kusimamia sheria na kuchukua hatua baada ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kutimiza wajibu wake.
Alisema katika kila kona ya Zanzibar kunanuka ufisadi wa ardhi na wahusika wa migogoro hiyo ni baadhi ya viongozi wa serikali na watendaji ambao sasa ni wahubiri wakubwa wa kero za Muungano kama njia ya kuwazubaisha wananchi.
Alisema wakati umefika kwa serikali kusimamia misingi ya utawala bora kwa vitendo ikiwemo kuwachukulia hatua watu wanaokabiliwa na tuhuma za kashfa ya ufisadi wa mali za umma.
Akizungumzia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar alisema chama chake kitaendelea kubaki na msimamo wa kutetea muundo wa serikali mbili.
CHANZO TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment