CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) jana
kilikamilisha safu yake ya uongozi kwa kuwapitisha kwa kishindo viongozi
wa ngazi za juu wa Chama hicho katika uchaguzi ambao ulionekana kuwa na
nidhamu kutokana na kutokuwa na uharibifu wa kura.
Katika uchaguzi wa safu za juu za Chama
hicho, Mwenyekiti, Makamu wa Mwenyekiti Zanzibar na Bara wajumbe wa
mkutano huo walitekeleza ombi la Yusuph Makamba la kumchagua kwa
kishindo Jakaya Kikwete kuongoza CCM .
Akitangaza matokeo hayo Spika wa Bunge
la Tanzania ambaye ndiye alikuwa msimamizi,Anne Makinda alisema kwamba
Mwenyekiti alipata ushindi wa kura 2,395 sawa na asilimia 99.92 huku
kura mbili zikisema hapana.
Makamu Mwenyekiti Zanzibar Dk Ali Shein
alipata kura 2,397 wakati makamu wa Bara Phillip Mangula naye alipata
idadi hizo za kura huku kukiwa hakuna kura zilizoharibika wala kusema
hapana kwa viongozi hao wawili.
Awali kabla ya kutamka ushindi wa
viongozi wa juu, walitamkwa wajumbe 20 wa viti vya Bara na Zanzibar. Leo
halmashauri kuu ya CCM (NEC) itachagua Kamati Kuu ;na Mwenyekiti Jakaya
Kikwete ataunda sekretarieti. Kitu kikubwa kinachosubiriwa kwa hamu ni
nafasi ya Katibu Mkuu.
Akimnadi Kikwete Katibu Mkuu wa zamani
wa CCM, Yusuf Makamba, aliwaponda wanaCCM wanaojitangaza kutaka urais
mwaka 2015, akisema wanapaswa kujihadhari, vinginevyo watapigiwa kura na
wake zao pekee.
Mbali na hilo, aliwaponda waliokuwa na mpango wa kumkwamisha Kikwete ili asiteuliwe tena kuwania uenyekiti wa chama hicho.
Alisema kuna watu wanajitangaza kugombea
urais kupitia CCM mwaka 2015, lakini akaonya kuwa uongozi unatoka kwa
Mungu na kwamba mtu hujulikana kwa sifa kuu tatu; anavyojifahamu,
wenzake wanavyomfahamu na anavyofahamika na Mungu.
“Kuna watu wanasema nagombea urais,
wanatangaza nitagombea urais mwaka 2015 … hayo tuachie sisi, unaweza
kujikuta unapata kura yako na ya mkeo tu,” alisema Makamba huku
akishangiliwa na wajumbe.
Alisema sifa moja ya kiongozi mzuri ni kuwa karibu na watu na hiyo ni sifa ya Rais Kikwete na ndiyo maana amekuwa kiongozi bora.
Kuhusu hoja ya kumpunguzia Kikwete kazi
kwa kumwondoa katika uenyekiti, Makamba alihoji wanaotaka apunguziwe
kazi, wanataka apewe nani wakati wao kazi moja tu imewashinda.
“Eti wanasema ana kazi nyingi apunguziwe
kazi moja, nani kasema kazi zimemshinda? Halafu huyo anayesema ana kazi
moja na yenyewe inamshinda, halafu hawasemi … tumpeni nani?” Alihoji
Makamba na kuendelea:
“Kazi ipi iliyomshinda? Halafu wanasema
tupige kura za maruhani, awe nani?” Alisema Kikwete ni kiongozi mzuri na
amekuwa karibu na watu kuliko hata wasaidizi wake na kuongeza kuwa
“baadhi walipata adhabu hapa jana (Jumapili) kwa kuwa mbali na watu,”
akimaanisha walioshindwa ujumbe wa NEC.
Aliongeza kuwa baadhi ya wanaoomba
uongozi wanafanya hivyo kwa manufaa yao, badala ya chama. Alimmwagia
sifa Kikwete kwa utendaji mzuri katika chama na Serikali na kuongeza
kuwa anastahili kuendelea kuongoza chama hicho tawala huku akiwataka
wajumbe wampime Kikwete kwa kazi alizofanya, badala ya kumhukumu kwa
matendo ya kibinadamu.
Awali, Makamu Mwenyekiti mstaafu Bara,
Pius Msekwa alisema tangu enzi za TANU na ASP na pia kuasisiwa kwa CCM,
utamaduni umekuwa ni kwa Rais wa Tanzania kuwa pia mwenyekiti wa chama
hicho Taifa.
No comments:
Post a Comment