Wakati neema ya mvua za vuli ikiendelea kunawiri katika maeneo mbali mbali nchini ikileta faraja zaidi kwa wakulima na wafugaji kwa kupata malisho ya Mifugo yao lakini kwa upande mwengine mvua hiyo hiyo imeonekana kuleta hasara.
Hasara hiyo inaonekana kuikumba Wizara ya Habari,Utamaduni, Utalii na Michezo kufuatia Jengo lake Maarufu la Makumbusho ya Taifa la Beit Al- Ajaib liliopo Forodhani Mjini Zanzibar kubomoka upande wa nyuma wa Jengo hilo.
Kifusi kilichodondoka kutoka kwenye Dari ya Jengo hilo robo yake kimeishia kwenye gari moja ndogo yenye nambari za usajili Z 897 DF inayomilikiwa na Bwana Said Saleh Saidi Mkaazi wa Forodhani ambae alikuwa ameiegesha pembezoni mwa Jengo hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifika mapema asubuhi katika eneo hilo kuangalia tukio hilo baada ya kupata taarifa hiyo na kuonyesha masikitiko yake kutokana na hasara hiyo kubwa.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alimueleza Balozi Seif kwamba Wizara hiyo ilikuwa ikiendelea na juhudi za kulifanyia matengenezo Jengo hilo kwa kipindi kirefu sasa.
Waziri Mbarouk alifahamisha kwamba jitihada hizo zilikuwa zikienda sambamba na matayarisho ya kutaka kuliezeka jengo hilokwa upande wa nyuma.
Alieleza kwamba kutokana na tatizo hilo Wizara ya Habari inakusudia kuwatumia Wataalamu wa Wizara yake kwa kukaa pamoja na Wahandisi wa Idara ya Ujenzi Zanzibar kuangalia hatua za kuchukuwa ili tatizo hilo lisije leta maafa.
Naye Mmiliki wa gari ndogo iliyoegeshwa pembezoni mwa Jengo hilo ambayo imeharibika kabisa kutokana na tukio hilo Bwana Said Saleh Said alisema alishuhudia mporomoko huo ukitokea muda mfupi baada ya kuegesha gari yake.
Bwana Said alimueleza Balozi Seif kwamba tukio hilo liliweza kuleta mtafaruk na kusababisha hofu miongoni mwa wakaazi wa eneo hilo pamoja na wale wafanyakazi wa jengo hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akimpa pole Bwana Said kutokana na hasara iliyomkumba alimtaka kuendelea kuwa na subra na kuamini kwamba hiyo ni mitihani ambayo inaweza kutokea na kumpata kuimbe ye yote na wakati wowote ule.
Hata hivyo Balozi Seif aliwanasihi watu wanaomiliki vyombo vya moto kuhakikisha kwamba wanakata bima ya vyombo vyao kwa lengo la kujinginga na hasara wakati vyombo vyao vinapopatwa na ajali.
No comments:
Post a Comment