Saturday, December 1, 2012

JAJI MKUU MSATAAFU ASEMA JESHI LA POLISI LINA MTAZAMO WA CHAMA KIMOJA

Jaji mkuu msataafu asema jeshi la polisi lina mtazamo wa chama kimoja

Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta, amelishukia jeshi la Polisi na kusema linachangia kuchochea uvunjaji wa haki za binadamu nchini.
Amesema miongoni mwa haki zinazovunjwa na jeshi hilo ambalo kimsingi, linapaswa kuwalinda raia na mali zao, ni kuzuia uhuru wa kutoa maoni na kuandamana.
Jaji Samatta alisema hayo jana wakati akifungua kongamano la wasaidizi wa sheria, lililoandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), ikilenga kujadili mambo mbalimbali kisiwani Pemba.
Kauli ya Samatta imekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete, kulihusisha jeshi hilo na harakati za kisiasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye (Kikwete) ni Mwenyekiti wake.
Akifungua Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma hivi karibuni, Rais Kikwete, pamoja na mambo mengine, alikaririwa akitoa rai kwa chama hicho kujibu hoja za upinzani badala ya kuwategemea polisi.
Kauli ya Rais Kikwete ilitafsiriwa kwa namna tofauti, huku ikihusishwa na malalamiko ya siku nyingi ya upinzani na asasi za kiraia, kwamba CCM inasaidiwa zaidi na vyombo vya dola kubaki madarakani.
Ingawa Jaji Samatta hakugusia ama kulihusisha jeshi hilo dhidi ya chama cha siasa, alisema polisi ni moja ya vyombo vinavyotumika kunyima uhuru wa kutoa maoni na kuandamana kwa raia. “Polisi bado wana mitazamo ya mfumo wa chama kimoja, wanakataza maandamano hata pale ambapo ni wazi kabisa kuwa hakuna hatari, usumbufu au amani kuvurugwa,”alisema Jaji Samatta.
Alisema mtazamo huo ni potofu kwa sababu unasababisha wananchi kubakia (moyoni) na mambo yanayowasumbua.
Kwa mujibu wa Jaji Samatta, uhuru wa mawazo ni haki ya msingi isiyotokana na fadhila ya watawala kwa raia. Alisema haki hiyo na ile ya kuandamana ni za msingi na kwamba kuwazuia kufanya hivyo ni mtazamo potofu.
Aliwakumbusha polisi wanaominya uhuru wa kutoa maoni na kuandamana, wakumbuke kwamba katika mfumo wa demokrasia ya kweli, si lazima wananchi waimbe wimbo mmoja. “Katika demokrasia sio lazima kila mtu aimbe wimbo huo huo…uhuru wa mawazo ni wa msingi sana… unachukuliwa kama kitu cha kawaida, kila mtu ana haki ya msingi juu ya suala lolote linalogusa watu kwa jumla,” alisema.
Jaji Samatta alisema maandamano sio mtazamo potofu kama inavyodhaniwa na polisi, ndio maana katika nchi za mabara ya Ulaya, Amerika na Asia, ‘upepo’ huo unaendelea kutumiwa na wananchi kudai haki zao.
Alisema kuzuia maadamano kunaminya fursa kwa watawala kufahamu mambo mengi kutoka kwa waliowaweka madarakani, hasa kuhusu kitu wanachokitaka na wasichotaka. “Kwa nini wananchi wasiruhusiwe kutumia maandamano, kuwajulisha watawala kuhusu mambo yanayowakera ili yapatiwe ufumbuzi,” alihoji.
Hata hivyo, Jaji Samatta alisema ingawa haki ya kuandamana ina mipaka yake, lakini mipaka hiyo imewekwa na sheria na wala si jeshi la polisi. Hata hivyo, Jaji Samatta, alisema ipo haja kwa wananchi kutii sheria, kwa vile hali hiyo inachochea kustawisha demokrasia na uhuru.
“Vyombo vya serikali vinawajibika kwa sheria, kama ilivyo kwa mwananchi,” alisema.

AONYA KULIPIZA VISASI
Jaji Samatta alisema vitendo vya kulipiza kisasi si utamaduni unaoendana na ustaarabu wa taasisi za umma hususani vyombo vilivyo chini ya serikali, badala yake kuwajibika kwa mujibu wa sheria.
Alisema inapotokea vyombo hivyo kuipinda au kuidharau sheria, ‘tiba’ si vurugu, bali kuziomba mahakama zitamke juu ya uhalali wa vitendo hivyo na kuchukua hatua nyingine za kisheria.

AHIMIZA UWAJIBIKAJI ASASI ZA KIRAIA
Jaji Samatta alisema asasi zisizo za serikali, zinazoshughulikia haki za binadamu zinapaswa kuwajibika zaidi, zikisaidiana na vyombo vingine ndani ya nchi.

Chanzo – Nipashe

No comments:

Post a Comment