Saturday, December 1, 2012

TANZANIA YAKERWA KWA UPOTOSHAJI WA CNN


Tanzania yakerwa na upotoshaji wa CNN

Kituo cha habari cha CNN chaikera serikali

Kituo cha habari cha CNN chaikera serikali
Serikali imesema imesikitishwa na taarifa za upotoshaji zinazosambazwa na kituo cha televisheni cha CNN cha Marekani kuwa Ziwa Nyasa ni mali ya Malawi. Kufuatia madai hayo serikali imeitaka CNN kusahihisha habari ilizozitoa kuwa mpaka wa Tanzania na Malawi upo kwenye ufukwe wa pwani ya Tanzania madai ambayo si sahihi.

Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Assa Mwambene, ilisema serikali imesikitishwa na taarifa hiyo na kuisisitiza CNN iisahihishe mara moja.

Akiongea na wanahabari, Mwambene alisema katika kipindi kilichorushwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumamosi iliyopita CNN imekuwa ikionyesha kuwa mpaka kati ya Tanzania na Malawi upo pembezoni mwa ufukwe wa Tanzania.

“Tumesikitishwa sana na taarifa hiyo na tunashangaa kuona chombo kikubwa kama CNN kinaweza kutoa taarifa za uongo kwa kiasi hicho,” alisema Mwambene.
Alifafanua kuwa unapozungumzia mpaka wa Tanzania ni pamoja na nusu ya eneo la Ziwa Nyasa kaskazini mwa mpaka wa Tanzania na Msumbiji na mpaka halali upo katikati ya ziwa hilo kama ilivyo upande wa Msumbiji na Malawi.
Msemaji huyo wa serikali alisema suala hilo linatarajiwa kupelekwa katika Baraza la Marais Wastaafu wa Nchi za Umoja wa Ushirikiano wa Uchumi wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa majadiliano zaidi.
Mgorogoro wa mpaka baina ya Tanzania na Malawi unaopita ndani ya Ziwa Nyasa ulianza kuleta mgogoro mwaka huu baada ya nchi hiyo kudai kuwa ziwa hilo ni mali ya Malawi.
Malawi imeanzisha mgogoro wa mpaka baada ya Rais Bingu Mutharika kufariki dunia na Joyce Banda kuchukua madaraka mwaka huu.

Nchi hiyo inadai kuwa mikataba ya Wakoloni waliotawala nchi za Malawi na Tanganyika miaka ya 1890 walikubaliana kuwa ziwa hilo na mali ya Malawi lakini
Tanzania inapinga madai ya Malawi kwa kuzingatia maelekezo ya Sheria za Kimataifa kuwa nchi zinapotenganishwa na maji mipaka inakuwa katikati ya maji.
Wakati huo huo, Mwambene amesema maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara yataadhimishwa Jumapili ijayo Desemba 9, kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

CHANZO: NIPASHE, 1 Disemba 2012

No comments:

Post a Comment