MSANII Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, ameepuka adhabu ya
kunyongwa hadi kufa kwa tuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven
Kanumba, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kumbadilishia mashtaka,
ambapo sasa anatuhumiwa kuua bila kukusudia.
Kutokana na mabadiliko hayo, Lulu ameepuka adhabu hiyo kwani hata
kama atapatikana na hatia, adhabu yake ni kifungo cha maisha au kuachiwa
huru.
Hii inatokana na kifungu cha 196 cha kanuni za adhabu ya kosa la kuua
bila kukusudia, ambapo anayepatikana na hatia anaweza kuhukumiwa
kifungo cha maisha, miaka kadhaa au kuachiwa huru.
Hata hivyo, baadhi ya wanasheria waliliambia gazeti hili kwamba
uzoefu wa adhabu nyingi za kuua pasipo kukusudia zilizowahi kutolewa
nchini, ni kati ya miaka 15 na wengine waliachiwa huru.
Lulu alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 11, mwaka huu akikabiliwa na tuhuma za kumuua Kanumba Aprili 7, 2012.
Alikuwa akidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 cha
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), shtaka ambalo mshtakiwa
anayepatikana na hatia adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
Hata hivyo, jana upande wa mashtaka ulieleza mahakamani kuwa kwa sasa
imebadilisha mashtaka kutoka kuua kwa kukusudia na kuwa kuua bila
kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha CP.
Mshtakiwa huyo alitarajiwa kusomewa mashtaka hayo mapya jana pamoja
na maelezo yote ya kesi, ambapo angesomewa ushahidi wa mashahidi wote
pamoja na vielelezo muhimu katika kesi hiyo.
Hata hivyo, hatua hiyo ilikwama kutokana na Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Tumaini Kweka anayeiendesha kesi hiyo kutokuwapo mahakamani
na badala yake aliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga.
“Upelelezi wa shauri lako umeshakamilika na tungeweza kukusomea
comital (maelezo ya kesi) leo, lakini kwa kuwa waendesha mashtaka hawapo
basi tunaliahirisha mpaka tarehe nyingine.”, alisema Hakimu Mkazi
Agustina Mmbando, anayesikiliza kesi hiyo katika hatua hiyo ya awali.
Taarifa hizo za kukamilika kwa ushahidi wa kesi hiyo zilipokewa kwa
furaha na shangwe na msanii huyo, kiasi kwamba alishindwa kujizuia
kuonyesha furaha yake.
Wakili wake Peter Kibatala aliiomba mahakama itoe ahirisho fupi hadi
Ijumaa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa mashtaka haya mapya pamoja na
maelezo ya awali.
Hakimu Mmbando alikubaliana na ombi hilo la Wakili Kibatala na akaahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa.
MWANANCHI

No comments:
Post a Comment