Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
amesema wananchi wanahitaji kuelimishwa zaidi juu ya uhifadhi wa
mazingira ili waweze kuyalinda na kuepuka kuyachafua.
Amesema uchafuzi wa mazingira mara nyingi umekuwa ukisababishwa na
wananchi wenyewe, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita kwa wananchi
kupatiwa elimu ya mazingira ili kuepusha uharibifu huo.
Maalim Seif ameeleza hayo wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa
Tanga bibi Chiku Galawa, mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege
wa Tanga kwa ziara ya siku mbili.
Amesema iwapo wananchi wataelimishwa ipasavyo wataweza kujiepusha
na uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kukata miti kiholela bila
ya kuzingatia athari za kimazingira.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Tanga bibi Chiku Galawa amesema uharibifu wa
mazingira ni moja kati ya changamoto kubwa zinazoukabili Mkoa huo, jambo
ambalo linarejesha nyuma maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa huo.
Amesema Serikali ya Mkoa huo inatafuta njia mbadala ya kutumia
nishati nyengine ili kupunguza matumizi ya kuni ambayo yanachangia
ukataji wa miti kiholela.
“Iwapo serikali itazuia matumizi ya makaa na kuni, serikali na
wananchi watapata nafasi ya kufikiria nishati mbadala ya kutumia kwa
ajili ya kupikia, lakini tukiendelea kutumia kuni mawazo yetu yatabakia
hapo hapo tu na tutaendelea kutumia kuni kila siku”,alitanabahisha bibi
Chiku.
Amesema ukataji wa miti kiholela katika Mkoa huo umekuwa ukichangia
kuwepo kwa athari za mabadiliko ya tabianchi yanayopelekea kuweko kwa
upungufu wa mvua pamoja na kuongezeka kwa hali ya joto.
Hata hivyo bibi Chiku amesema Mkoa huo umepiga hatua kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya barabara.
Akiwa Mkoani Tanga, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama
Cha Wananchi CUF anatarajiwa kuhutubia mikutano mitatu ya hadhara katika
viwanja vya Tangamano, Kwadiboma Sokoni na Handeni.
Na Hassan Hamad, Tanga
No comments:
Post a Comment