Wednesday, December 26, 2012

Matukio haya Zanzibar hayatatuacha salama

Mji wa Zanzibar



 
 
 
 
 
 
Rate This
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Haipendezi kulazimisha mambo ambayo ni hatari kwa baadaye. Taifa letu linasifika kwa amani, umoja na mshikamano, ndiyo maana jirani zetu wanaopigana wanakimbilia kwetu wakiamini ni sehemu salama.
Lakini kama wasemavyo wahenga kuwa mgema akisifiwa tembo hulitia maji, ndivyo tumeanza kujipambanua huko visiwani Zanzibar kutokana na matendo ya itikadi za dini na siasa kuhujumiana kuzidi kushika kasi.
Juzi jioni tumeelezwa kuwa padri wa Kanisa Katoliki lililopo Mpendae, visiwani Zanzibar, Ambrose Mkenda, amejeruhiwa kwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake majira ya saa 12 jioni juzi wakati akitoka kanisani.
Padri huyo ambaye pia ni mweka hazina wa kanisa hilo, alipigwa risasi akiwa ndani ya gari lake na kujeruhiwa sehemu ya kichwa, hivyo kulazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja visiwani humo, kisha kuhamishiwa jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jana kwa matibabu zaidi.
Tunampa pole Padri Mkenda huku tukiitahadharisha serikali kuwa matukio haya ya Zanzibar hayatatuacha salama, ikiwa tunaendelea kufumbia macho vitendo hivyo na wahusika wanaovichochea.
Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba ni muda mfupi umepita tangu Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhili Soraga, amwagiwe tindikali Novemba 7, mwaka huu, huko Magogoni, Msumbiji, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Lakini itakumbukwa kuwa kabla ya Sheikh Soraga kumwagiwa tindikali hiyo, Zanzibar iligubikwa na matukio ya vurugu za kidini kiasi cha baadhi ya watu kuharibu mali za wenzao, baadhi ya makanisa na baa kuchomwa moto.
Matukio hayo yalihusishwa na itikadi za kidini huku wengi wakiitaka serikali ichukue hatua mahususi kuwasaka wahusika na kuwachukulia hatua, lakini mambo hayo yamechukuliwa kwa uzito mdogo.
Vurugu hizi za kuchomeana nyumba za ibada, kuteketeza baa, kuwajeruhi baadhi ya viongozi wa dini kwa sababu zozote zile, ziwe za kisiasa au kidini, hatukuzizoea katika ardhi ya Tanzania.
Ni kutokana na desturi hiyo, tunaitaka serikali kuchukua hatua haraka za makusudi kuhakikisha inakomesha michezo hii ambayo inaelekea kulitia doa taifa letu, ili kuhakikisha sifa ya amani, umoja na mshikamano wetu inabakia palepale.
Sisi ni wamoja na wote ni Watanzania, hivyo hatuwezi kukubali kwa namna yoyote ile kugawanywa kwa misingi ya dini, itikadi za kisiasa, ukabila, ukanda, rangi na mengineyo. Hiyo si Tanzania waliyoijenga waasisi wetu.
Kamwe hatuwezi kuweka amani yetu rehani kwa faida ya kundi fulani, daima lazima tuendelee kuwa kioo cha utulivu barani Afrika na dunia. Kwa hiyo, yanayotokea Zanzibar leo hatuyaungi mkono hata chembe.

CHANZO TANZANIA DAIMA.

No comments:

Post a Comment