Wednesday, December 26, 2012

CCM acheni siasa za chuki’

Mbunge wa Segerea, Dk. Makongoro Mahanga

 
 
 
 
 
 
Rate This

Viongozi  na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam wameshauriwa kuacha siasa za chuki, ubaguzi, ukabila, udini na makundi, ili chama hicho kipate nguvu za kupambana na vyama pinzani.
Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Mbunge wa Segerea, Dk. Makongoro Mahanga (CCM) alipofunga semina ya viongozi wa matawi na jumuiya za chama hicho za Kata ya Kiwalani.
Alisema baada ya kauli ya Mwenyekiti wa chama chao taifa, Rais Jakaya Kikwete, kuwaagiza viongozi na wanachama wa CCM kuacha siasa za chuki na ugomvi miongoni mwao wakati akifungua mkutano mkuu uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni alisisitiza kuwa ni agizo la wanachama wote.
Kwa mujibu wa Dk. Mahanga, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, ni wazi kwamba agizo hilo limeanza kutekelezwa kwa vile kauli za baadhi ya viongozi wa CCM kushambuliana hadharani zimepungua, hivyo kazi inayotakiwa ni kukiimarisha chama kwa kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
“Mkoa uliokuwa na siasa za chuki, ubaguzi, ukabila, udini na makundi miongoni mwa wana CCM ni Dar es Salaam ambapo baadhi ya viongozi tena wa ngazi za juu kabisa huwabagua baadhi ya wanachama wenzao kwa kuwaita majina ya ajabu kama ‘wakuja’, ‘mijaluo’, ‘makafiri’ na mengineyo.
“…Hii ilileta chuki hasa wakati wa chaguzi za ndani na kuhatarisha umoja, mshikamano na nguvu ya chama, nawashauri wote wanaowabagua wenzao taarifa zao zipelekwe kwenye chama ili wahusika wajadiliwe kwenye vikao vya maadili,” alisisitiza Dk. Mahanga.
CHANZO TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment