HOTUBA YA MWENYEKITI WA BARAZA LA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR KATIKA MAHAFALI YA NANE TAREHE 22 DISEMBA 2012
Mh. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar;
Mh. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mh. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar;
Mh. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali;
Wah. Mawaziri;
Wah. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi;
Wah. Wabunge;
Nd. Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana,
Assalamu alaykum,
Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye anayestahiki kushukuriwa kwa kutukirimu afya njema, uzima na uhai. Zaidi ya hayo akatuwezesha leo hii tukaweza kujumuika pamoja hapa katika mnasaba huu adhimu.
Amma, pili, nikushukuru wewe, mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar. Tunajua una majukumu mengi na mazito ya kitaifa likiwemo hili la leo. Lakini umeyaacha mengine na kuipa nafasi na muda wako shughuli yetu hii ya mahafali ya nane ya chuo chetu.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka kumi na moja iliyopita yanatokana na maamuzi ya hekima na busara ya mabaraza yote ya awamu nne zilizokuwepo madarakani. Mabaraza hayo yamekuwa yakipitisha sera na maamuzi mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa mambo na kazi za Chuo. Hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha malengo kadhaa ya Chuo. Katika mwaka uliopita wa masomo baraza lilifanya kazi kubwa ya kupitia mapendekezo ya mabadiliko ya mfumo mzima wa Chuo, na kupitia mapendekezo ya kanuni mbali mbali zinazohusu shughuli za Chuo.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Chuo pia kimeanzisha masomo kadhaa mapya katika mwaka huu wa masomo kwa ngazi mbali mbali. Mfano mzuri ni somo la PhD ya Kiswahili ambalo linasomeshwa na walimu wengi wao wakiwa ni Wazanzibari kutoka nje ya Chuo. Vilevile Chuo kimeanzisha skuli ya Sekondari kwa masomo ya Sayansi. Pia, Chuo kinaendesha program maalum ya kuwainua viwango wanafunzi ambao wamemaliza kidato cha VI lakini hawakupata alama za kutosha kuingia Chuo Kikuu.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Aidha, katika Chuo kwa sasa kina vituo viwili vya utafiti. Navyo ni kituo cha Ulimwengu cha Masomo ya Kiswahili na Maendeleo yake (Global Center for Swahili Studies and Advancement) na Kituo cha Utafiti wa Sayansi za Bahari na Mazingira, na Rasilimali Asilia (Tropical Research Center of Oceanographic and Environmental Sciences)
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Hata hivyo, Chuo kinakabiliwa na changamoto za kuinua na kujenga uwezo wa wafanyakazi kitaaluma. Kwa kudra zake Mungu, Chuo kimepata msaada wa kusomesha walimu wake kutoka Sultan Qaboos, ambae kaanzisha Sultan Qaboos Academic Fellowship Program for SUZA. Msaada huo umetolewa na Mfalme wa Oman kwa Wazanzibari kwenye kujenga uwezo wa Vyuo vya Serikali ya Zanzibar kwa kupitia SUZA. Chuo kitatumia neema hii kwa kupeleka wafanyakazi wafikao 50 katika mafunzo mbalimbali kwa mwaka huu. Program hii ikiendelea vyema, changamoto ya rasilmali watu iliyo bora kwa Chuo itatoweka.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Changamoto nyingine ni tafauti ya mishahara kati ya walimu wa Vyuo vya Bara na Zanzibar. Mishahara ya Bara ipo juu kwa zaidi ya 50% ya mishahara ya Zanzibar. Hali hii inaweza kuwashawishi walimu kuhamia Bara kufuata maslahi mazuri zaidi. Kutokana na umuhimu wa Chuo chetu hiki, kama unayoufahamu sana, ni vyema serikali ikafanya juhudi za makusudi za kuongeza mishahara ya walimu ili angalau ilingane na mishahara ya Vyuo vya Bara.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
“Anayeshukuru huongezewa”. Nasi tunaishukuru Serikali yetu kwani pamoja na uchache wa fedha ulionao, inatimiza wajibu wake katika kuhakikisha kuwa shughuli za kila siku za Chuo hazisiti. Kadhalika tunafarajika kwa misaada mbalimbali tunayopata kutoka nje. Chuo kinathamini misaada hiyo kutoka wahisani, mashirika na watu binafsi. Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Benki ya Dunia, Kampuni ya Bwana Said Salim Bakhresa, Ubalozi wa Uturuki, Ubalozi wa Ufaransa, Benki ya Watu wa Zanzibar, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Zanzibar, kutokana na misaada yao kwa Chuo.
Kwa kumalizia napenda kukushukuru Mheshimiwa kwa mara nyengine tena.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment