CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimesema, baada ya kuutumia mwaka 2012 kupanga safu
ya uongozi katika chaguzi za ngazi zote zilizomalizika hivi karibuni,
mwaka ujao wa 2013 utakuwa wa kuchapa zaidi. Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara)
Mwigulu Nchemba (pichani) alisema, kazi itakayofanywa na CCM katika
mwaka huo, ni pamoja na kukagua upya utekelezaji wa ilani ya CCM na
kuhakikisha zile ambazo hazikamilika zinamalizwa.
“Mwaka huu wa 2012 unaomalizika tuliutumia zaidi kujipanga katika
uchaguzi wa ngazi zote ili kupata safu nzuri itakayoisimamia serikali
kutekeleza ilani ya CCM, sasa mwaka mpya wa 2013 utakuwa wa kazi zaidi
za kusimamia serikali ili kuhakikisha mwaka 2015 mpiganaji wa CCM
tutakayemteua kugombea urais anapita kiulaini”, alisema Mwigulu.
Akizungumzia tukio la Mbunge wa Arusha Godless Lema kushinda rufani yake
dhidi ya hukumu iliyomvua ubunge Aprili mwaka huu, Mwigulu alisema,
ushindi huo ni ushahidi kwamba serikali ya CCM inaongoza kwa misingi ya
utawala bora ambapo kila anayestahili haki anapata.
“Ushindi huu wa Lema, siyo kwamba anaakili sana au chama chake kina
maarifa sana yaliyosababisha ushindi, ila ni kutokana na serikali ya CCM
iliyopo madarakani kuheshimu na kujali haki na kwa kweli natumia fursa
hii kuipongeza Serikali kwa kuthamini na kusimamia haki wakati wote..
Ninyi si mnajua katika nchi zisizo na utawala bora jinsi ambavyo mambo
huwa kwenye kesi kama hizi. lakini hapa Tanzania ni tofauti kabisa”,
alisema, Mwigulu.
Aliwashangaa Chadema akisema, “Hawa ni watu wa aina yao, waliposhindwa
katika kesi Arusha walisema Ikulu imeingilia na majaji hawajui
kiingereza.. sasa leo wameshinda wanafurahi na kuona kwamba sasa majaji
wanajua kiingereza na hawakuigusa Ikulu kwamba imeingilia, maana pale
ilipotolewa hukumu umbali wake ni hatua chache na Ofisi ya Ikulu kuliko
Arusha”.
Mwigulu alitumia fursa hiyo kuwatakia heri Watanzania kwa sikukuu za
Krismas na mwaka mpya na kuwataka kuzitumia sikukuu hizo kwa makini na
kwa kiasi ili zisiwe chanzo cha matatizo kwao badala ya furaha.
“Chama Cha Mapinduzi kinawatakieni sikukuu njema za Krismas na mwaka
mpya, lakini tunawaomba msherehekee kwa kiasi huku mkichunga usalama
wenu na mali zetu”, alisema Mwigulu.
No comments:
Post a Comment