Dec
26
2012
HIVI karibuni imeelezwa kuwepo mpango wa kutaka kuwashirikisha
kikamilifu wananchi wa Zanzibar katika mchakato wa kutoa maoni kwa
sheria zitakazoandaliwa na serikali.
Hatua hii, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Katibu wa Baraza
la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad, ni kuzifanya sheria za Zanzibar
kwenda sambamba na matakwa na matarajio ya wananchi.
Ukiyatafakari maelezo haya juu juu utaona huu ni mpango mzuri na
unaokubalika katika mfumo mzuri wa utawala bora, lakini uzoefu
unaonyesha kuwa mara nyingi kinachosemwa na serikali ni tofauti na kile
kinachotekelezwa.
Kwa ufupi, kwa muda mrefu na mpaka hivi sasa, serikali imekuwa
ikiona ni haki yake kuudanganya umma kwa maneno matamu yaliyopakwa
asali, lakini kinacholiwa ni shubiri.
Nasema hivi kwa sababu nyingi zilizotokana na uzoefu. Mojawapo ni
kwamba mara nyingi tumeambiwa kwa vishindo kwamba Zanzibar imepania kuwa
na mfumo wa utawala wa haki na sheria na uliokuwa wa kweli na uwazi.
Lakini hili halionekani kutendeka na kila siku tunaona sheria
zinatoka juu na kutelemshwa chini na hata sheria ikiwa nzuri usimamizi
wake huwa mbovu na baadhi ya wakati unanuka na kukirihisha.
Kwa mfano, mpaka hivi sasa dhamana kwa mshtakiwa sio haki bali
inatokana na mapenzi ya hakimu. Wapo mahakimu waliokuwa na ubavu wa
kusema walipewa amri na wakubwa juu ya namna walivyotakiwa kuziendesha
kesi, lakini hao mahakimu na majaji hawakuwa na ujabari wa kusema
viongozi waliotoa amri hizo ni kina nani.
Katika utoaji wa dhamana mahakama za Zanzibar zimekuwa zikiweka
masharti magumu kama ya kulazimisha wadhamini wawe watumishi wa serikali
na kwa maana hiyo raia wengine hawana haki ya kuwawekea dhamana
washtakiwa.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu, alikiri hivi katika kipindi
kimoja cha Televisheni ya Zanzibar nyakati za asubuhi kuwa mwenendo huu
wa kutaka watumishi wa serikali wawe ndiyo wanaoruhusiwa kuwadhamini
washtakiwa ni mbovu.
Lakini kwa masikitiko makubwa, badala ya kueleza kwamba anachukua
hatua za kuirekebisha hali hii ya kusikitisha na kutisha alisema atakaa
na wenzake kujadili suala hili. Lini atafanya hivyo hakueleza.
Lakini hapa inafaa ieleweke kwamba wakati Jaji Mkuu anapanga kuwa
na kikao wapo watu waliokosa kupata dhamana na wanateseka mahabusu
kutokana na haya masharti magumu ya dhamana.
Ni kawaida kusikia katika mahakama za Zanzibar upande wa mashtaka
kuomba anayeshtakiwa aendelee kukaa mahabusu hata ikiwa imepita miezi
mitatu kwa vile upelelezi wa tuhuma zinazomkabili mshtakiwa,
haujakamilika.
Hapa unajiuliza kama upelelezi haukukamilika ilikuwaje basi mtu
akamatwe na kufunguliwa mashtaka? Au ndio kusema dhana au ndoto huwa
inatosha kuwa sababu ya msingi kumfungulia mtu mashtaka? Hii ni hatari
kubwa. Jambo hili linafaa lichunguzwe kwa makini na kufanyiwa
marekebisho ya haraka.
Njia moja itayosaidia kuzuia matumizi mabaya ya sheria au uonevu
wa aina moja au nyingine ni kuwa na kipengele kinachowapa watu
wanaofutiwa kesi kutokana na kukosekana ushahidi kulipwa fidia kwa
bughudha, hasara na mateso waliyoyapata wakiwa mahabusu wakati hapakuwa
na ushahidi wa kutenda kosa.
Njia hii itapunguza matumizi mabaya ya sheria na kupunguza uonevu
kwa kutumia vyombo vya dola na mahakama. Jingine linalofaa kutupiwa
macho ni huu mtindo wa wawakilishi kujadili na kupitisha sheria
mbalimbali bila ya kuwa na vikao vya kushauriana na wananchi katika
majimbo yao.
Hawa wawakilishi hudiriki hata kueleza bila ya aibu kwamba walikuwa
wanazungumza kwa niaba ya watu katika majimbo yao na wanaunga mkono au
kuukataa muswada wa sheria mia kwa mia wakati hawajafanya hata mkutano
mmoja katika majimbo yao kuujadili huo muswada wa sheria. Vilevile
huenda huyo mwakilishi hajataka hata ushauri juu ya huo muswaada wa
sheria kutoka kwa mume au mke wake, jirani au rafiki.
Ni vizuri kutoka sasa wakati wawakilishi wanapojadili muswada watoe
uthibitisho wa vikao vingapi walifanya katika majimbo yao na idadi ya
watu walioshiriki katika mijadala na sio kusimama ndani ya Baraza la
Wawakilishi na kutoa kauli zisiokuwa na ukweli.
Vile vile vyombo vya habari vya serikali, bado sio vya umma kama
tunavyotakiwa tuamini, viendeshe mijadala ya wazi juu ya hizo sheria
zinazotaka kutungwa ili wananchi waelewe kinachoendelea katika nchi yao.
Mimi binafsi sikumbuki hata siku moja kuambiwa kipo kikao katika
jimbo langu ambapo mwakilishi alikuwa anataka maoni ya wananchi juu ya
muswada wa sheria unaotaka kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi.
Njia gani hao Wawakilishi wetu wanatumia kujua fikra za wananchi,
wanazijua wenyewe na ni siri yao ya mioyoni. Sasa tunaambiwa unakuja
mfumo mpya. Tunasema ahlan wa sahlan, lakini kinachozungumzwa kiwe cha
kweli na sio danganya toto.
Watu wazima wanapodanganywa huona sawa na kutukanwa kwani
anayedanganywa ni mtu zuzu na asiyejua lolote. Kwa hivyo ni vizuri
tukabadilika, tena kwa haraka sana na kuhakikisha wananchi wanashiriki
katika kutunga sheria za nchi yao.
Lakini jingine muhimu ni kuhakikisha sheria zinasimamiwa kwa
uadilifu na pasiwepo mazingira ya watu kutia mashaka kwamba zinatumika
vibaya, hasa kukidhi malengo na utashi wa kisiasa.
Wote wanaovunja sheria au kunyanyasa watu, bila ya kujali nyadhifa
zao katika serikali wachukuliwe hatua ili kila mwananchi awe na uhakika
kuwa Zanzibar ni ya watu wote na sio wengine mabwana na wengine watwana.
Tunausubiri huo mchakato kabla ya kuutolea hukumu, lakini kama
lengo ni kudanganya basi wahusika waelewe kwamba kwa sasa watu wa
Zanzibar hawadanganyiki. Kama maneno matamu yanamtoa nyoka pangoni hiyo
haitoshi kama hayaendani na vitendo kupata imani ya Wazanzibari kwa
serikali yao.
Wanaofikiri bado wanaweza kuendeleza ubabaishaji wajue wamechelewa na historia itakapowahukumu wasije kusema wanaonewa.
Chanzo – Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment