Dec
26
2012
MELI za mitumba zilizotumika kwa muda wa miaka 15 hazitosajiliwa au kupewa lesseni ya kuchukua abiria na mizigo visiwani Zanzibar.
Hatua hiyo imechukuliwa na serikali kufuatia muswada wa marekebisho ya sheria namba 5 ya mwaka 2006 unaotarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) Januari mwakani.
Marekebisho hayo ya sheria yamekuja kufuatia ajali mbili za kuzama meli katika mwambao wa Zanzibar na kusababisha mamia ya wananchi kupoteza maisha na wengine kutoweka baharini mwaka 2011 na mwaka huu.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, Rashid Seif Suleimani, anatarajia kuwasilisha muswada huo ambao umeanza kulalamikiwa na baadhi ya wawekezaji katika sekta ya usafirishaji baharini Zanzibar.
Kifungu cha 17 A(1) cha muswada huo kinasema: “Hakuna meli ambayo itazidi umri wa miaka 15 tokea tarehe ya kutumika kwake, itakayosajiliwa au kupewa lesseni kwa ajili ya kuchukua abiria na mizigo Zanzibar.”
Kwa mujibu wa muswada huo, chombo chochote cha usafiri kinachotua nchi kavu, ikiwa asili ya utengenezaji si kwa ajili ya matumizi ya kuchukua abiria, hakitosajiliwa au kupewa leseni kwa madhumuni ya kuchukua abiria katika visiwa vya Zanzibar kwa sababu za kiusalama.
Waziri Seif alisema katika muswada huo kuwa, hakuna meli itakayosajiliwa au kupewa leseni kwa madhumuni ya kuchukua abiria ndani ya Zanzibar ikiwa imebadilishwa kutoka katika muundo asili wa utengenezaji wake.
Aidha, muswada unapiga marufuku wawekezaji katika sekta ya usafirishaji kubadilisha muundo wa meli kama mashine za umeme, vyombo vya mawasiliano, winchi au vitu ambavyo havitokani na muundo wake asilia.
Hassan Ali, Zanzibar
No comments:
Post a Comment