SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar huenda ikaanza kuondokana na hasara ya
mamilioni ya fedha kutokana na kupotea kwa umeme kabla ya kuwafikia
watumiaji, iwapo wataalamu wake wataanza kutumia teknolojia za kisasa za
matengenezo ya umeme wakati nishati hiyo ikiendelea kuwafikia
watumiaji.
Hayo yamebainika baada ya wataalamu wa Shirika la umeme la Zanzibar
wakiongozwa na Mhandisi wa Mfumo wa Udhibiti wa shirika hilo, Haji Ameir
Haji, kutembelea kituo kinachotoa mafunzo ya umeme bila kuzima, cha Mc
Donald Live Line Technology kilichopo Morogoro sambamba na kujifunza
matumizi ya kurudisha uhai kwenye vyuma chakavu kwa kutumia ZINGA yaani
Zink Governise.
Mhandisi huyo kutoka Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) aliahidi
kufikisha elimu hiyo kwa viongozi wa juu wa shirika hilo ili kuangalia
uwezekano wa kukabiliana na hasara ya mamilioni ya fedha ambayo wamekuwa
wakiingia kwa ununuzi wa vyuma vipya, au kutumia njia ya muda mfupi ya
kupaka rangi vyuma vinavyoathiriwa na kutu kutokana na kuozeshwa na maji
ya chumvi.
Alisema mfumo huo ni mzuri hasa kwa Zanzibar ambako kuna watalii
wengi ambao hawajazoea kuishi bila umeme na wana imani kuwa utaalamu wa
kuziba mianya ya upotevu wa umeme ikiwemo kwa kukagua dosari katika
vikombe na nguzo, kutasaidia kupunguza hasara ambayo wanaamini ipo
kutokana umeme wao kuutoa mbali, jijini Dar es salaam.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo hicho, Donald Mwakamele alisema
kati ya asilimia 30 hadi 40 ya umeme umekuwa ukipotea kabla ya kuwafikia
watumiaji kutokana na sababu mbalimbali, mambo ambayo huenda
hayaangaliwi kwa undani zaidi na wahandisi kutokana na kujifunza kusuka
umeme na siyo elimu ya biashara ambayo ingewawezesha kufahamu hasara
kubwa inayopatikana hasa kwa kufanya matengenezo wakati umeme ukiwa
umezimwa.
Alisema kuwa ipo haja kwa kampuni za umeme kujua mbinu za kuzuia
mianya hiyo hasa kwa kutumi mfumo wa kutengeneza umeme bila kuzima
(liveline) badala ya mfumo waliouzoea wa kuzima (deadline) ili kuepuka
hasara na gharama kubwa zisizo za msingi na kumudu kujiendesha kwa
faida. Tayari wataalamu kutoka mataifa mbalimbali duniani wamekuwa
wakikitembelea kituo hicho kwa ajili ya kujifunza teknolojia hizo ambazo
Tanzania ni nchi pekee barani Afrika kutoa, na kama zitatumiwa vyema
itasaidia uchumi wa nchi kukua kwa kasi.
No comments:
Post a Comment