Thursday, December 27, 2012

Uchaguzi Oman shwari

fp02




 
 
 
 
 
 
Rate This

KARIBU Waomani 546,000 waliosajiliwa kupiga kura jana walijitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi wao watakaowawakilisha katika Mabaraza ya Manispaa. Viti vilivyokuwa vikigombewa ni 192 kutoka mikoa yote ya taifa hilo la kiarabu, ambapo wagombea 1,475 wakiwemo wanawake 46 walishindana kuwania nafasi hizo.
Kulikuwa na vituo vya kupigia kura 104 nchini kote, ambapo wapiga kura walitenganishwa kulingana na jinsia zao.
Uchaguzi wa Mabaraza ya Manispaa ni wa kwanza kufanyika nchini Oman, ukiwahusisha wananchi moja kwa moja.
Kabla ya uchaguzi huo, kulikuwa na Baraza moja tu la Manispaa katika mji mkuu Mascut ambapo wajumbe wake walikuwa wanateuliwa.
Mmoja wa wapiga kura wa Oman akitumbukiza kura yake.
Mmoja wa wapiga kura wa Oman akitumbukiza kura yake.
Uchaguzi huo mpya mbali ya kuwa na wajumbe wa kuchaguliwa lakini pia kutakuwa na baadhi ya wajumbe wa kuteuliwa.
Waandishi wa habari wa shirika la magazeti ya serikali Zanzibar ambao walitembelea wilaya za Samail na Nizwa, kilomita zaidi ya 100 kutoka Muscat wanasema uchaguzi uliendeshwa kwa misingi ya utulivu mkubwa.
Walisema uchaguzi huo unaoendeshwa kwa mfumo wa kisasa wa elektroniki unamchukua mpiga kura dakika 2 tu kumaliza kupiga kura yake.
Lakini cha kufurahisha, kwa kuwa uchaguzi huo uliendeshwa siku ya kazi, baada ya mpiga kura kumaliza kumchagua kiongozi anaemtaka, alipewa risiti maalum ambayo ilimzuia kutoendelea na kazi kwa siku hiyo.

Aidha walisema, wanaume wametenganishwa na wanawake, ingawa wote wanapiga kura katika kituo kimoja, lakini maeneo tafauti.
Akizungumza kuhusu uchaguzi huo, Gavana wa wilaya ya Samail (Wali Samail), Ahmed Abdullah Al-Kindy, alisema katika wilaya hiyo kuna wagombea 42 huku watu waliosajiliwa kupiga kura wakiwa 9,969, ambapo washindi wanne wa kwanza ndio watakaoiwakilisha wilaya hiyo katika baraza la Manispaa.
Hata hivyo, alisema kati ya wagombea hao hakuna mwanamke, na hiyo imesababishwa na woga wa kushindwa walionao wanawake pamoja na uhamasishaji mdogo.
Kuhusu watu wenye ulemavu, Gavana huyo alikiri kwamba hawakuandaa karatasi maalum za kupigia kura kwa kundi hilo, lakini alisema wameandaa vyumba maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu, ambavyo vina wasaidizi.
“Unajua huu ni uchaguzi wa kwanza, ndio kwanza tunajifunza, tunatarajia katika uchaguzi mwengine kila kitu kitakaa sawa,” alisema.
Khawla Hassan Al-Aamri(23) ambae amehitimu chuo katika masuala ya uhusiano wa umma na ambae anasubiri ajira, alisema uchaguzi huo ni muhimu katika historia ya Oman.
Aidha alisema uchaguzi huo ni changamoto kwa wanawake kuhakikisha wanagombea nafasi hizo katika uchaguzi mwengine utakaofanyika baada ya miaka minne.
Aidha alisema, matarajio yake ni kuona watu watakaochaguliwa wanakuwa wachapa kazi kuhakikisha maendeleo katika manispaa hiyo yanapatika kwa wananchi wote.
Matokeo ya uchaguzi huo yalitarajiwa kuanza kutangazwa jana (Disemba 22) baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa saa 1 usiku (saa 12 jioni) kwa saa za nyumbani.
 
Na Juma Khamis na Bakar Mussa, Oman

No comments:

Post a Comment