
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema askari anayedaiwa kuwa ni askari wa jeshi la wananchi Tanzania na kupiga Picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ametoroka.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema jana kwamba pamoja
na hatua yake ya kutoroka, jeshi litaendelea kumsaka kwa udi na uvumba
ili kumhoji na kujiridhisha kama kweli ni mwanajeshi wake kabla ya
kumchukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kifungu cha 147 cha Katiba
ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya 1977.
“Huyu kijana inasemekana alishawahi kupitia Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT), lakini wakati tunaendelea na uchunguzi alitoroka katika nyumba
aliyokuwa amepanga bila ya taarifa kwa baba mwenye nyumba,” alisema
Kanali Mgawe na kuongeza:
“Askari huyo alikuwa anaishi katika nyumba ya kupanga mita chache
karibu na Kituo cha Polisi cha Simanjiro, Arusha na alikuwa
akijishirikisha na ulinzi shirikishi.”
Alipoulizwa jina la askari huyo, Kanali Mgawe alijibu: “Yeye alikuwa anafahamika mtaani hapo kwa jina la kamanda.”
Hata hivyo, Kanali Mgawe alisema jeshi hilo litahakikisha linatoa
ripoti kamili kwa umma baada ya kumkamata na uchunguzi kukamilika ili
kuondoa utata uliogubika suala hilo.Alipoulizwa kama kuna tofauti gani
kati ya mwanajeshi kuingia kwenye mikutano ya wanasiasa na wale
wanaofanya kazi za kisiasa kama wakuu wa wilaya na mikoa, Kanali Mgawe
alijibu:” Wanajeshi wanaofanya kazi za U-DC au RC, wanaruhusiwa
kisheria.”
Alifafanua kuwa iwapo mwanajeshi atateuliwa kufanya kazi katika
taasisi yeyote ya Serikali nje ya jeshi, atatakiwa kuvua magwanda ya
jeshi na kufanya kazi hiyo mpaka atakapomaliza muda wake na baada ya
hapo ataruhusiwa kurejea jeshini.
“Kuna kitu kinaitwa ‘secondment.’ Mwanajeshi anaruhusiwa kufanya
shughuli zozote nje ya jeshi iwapo atahitajika kufanya hivyo. Ila kwa
masharti ya kuvua magwanda, hivyo wananchi wasishangae kuwaona baadhi ya
askari wetu ni wakuu wa wilaya na mikoa na baadaye kurudi jeshini
kuendelea na majukumu yao,” alisema Kanali Mgawe na kuongeza:
“Askari akiwa katika majukumu yake mapya, atafanya kazi zote
atakazopewa zikiwamo za kisiasa kama ilivyo kwa wakuu wa wilaya na
mikoa, lakini akirudi jeshini, anarudi kuwa askari mwenye utii na
kufuata kanuni za jeshi zisizofungamana na siasa.”
Na : Nuzulack Dausen
No comments:
Post a Comment