Waislamu
nchini wametakiwa kuyaendeleza matendo mema yaliyoasisiwa na maulama
mbali mbali, ili kujenga jamii yenye maadili na kuendeleza taaluma zenye
manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Wito huo umetolewa na imamu wa
Masjid Gof Mkunazini Zanzibar Sheikh Mudh-hirddin Ally Kullatein katika
khitma maalum ya kumuombea marehemu Sheikh Said Mohammad Al-bir
aliyefariki dunia hivi karibuni nchini Kenya akiwa na umri wa miaka 73.
Khitma hiyo hiyo pia ilihudhuriwa
na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar al-hajj Maalim Seif Sharif
Hamad pamoja na Mufti Mkuu wa Zanzibar sheikh Saleh Omar Kabi.
Akitoa wasifu wake baada ya
khitma hiyo, sheikh Mudh-hirddin Kullatein amesema marehemu sheikh Said
Mohammad Al-bir ametoa mchango mkubwa kwa Zanzibar katika kuendelea
taaluma ya dini ya kiislam.
Amesema katika uhai wake aliweza
kuasisi darsa zipatazo mia moja pamoja na misikiti kadhaa katika maeneo
mbali mbali ya Afrika Mashariki ikiwemo Zanzibar, mambo ambayo yanapaswa
kuendelezwa.
Nae ndugu wa karibu wa sheikh
huyo sheikh Said Ahmed amesema msiba wa kuondoka kwa sheikh huyo sio wa
watu wa Lamu pekee ambako ndiko alikozaliwa, bali ni wa Afrika Mashariki
yote ambapo ametoa mchango wake katika kuendeleza dini ya kiislam.
Sheikh Ahmed amesema marehemu
sheikh Al-bir aliweza kujifunza na kusomesha taaluma tofauti katika uhai
wake, na wakati wote alikuwa akihimiza watu kusoma na kuendeleza
taaluma wanazozipata kwa maslahi yao ya dunia na akhera.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu sheikh Al-bir mahali pema Paponi (Ammin).
Hassan Hamad (OMKR)
No comments:
Post a Comment