Imewekwa na Hamed Mazrouy
TUME ya mabadiliko Katiba mpya nchini Tanzania, imeelezwa kuwa Baraza la Mapinduzi halikushauriwa wala kushirikishwa katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliyoundwa Aprili 26, 1964.
Wanasiasa wakongwe waliyokuwa katika Serikali ya Mapinduzi, wakati wa kuundwa kwa Muungano huo, Bw Salum Rashid na Bw Hassan Nassor Moyo waliiyambia Tume hiyo, walipokuwa wakitoa maoni yao Maisara, mjini Zanzibar.
Katika maoni yao walisema: Tangu awali ya kuundwa Muungano huo, kulikosekana uhaliali wake, licha ya kuwa umedumu kwa miaka hamsini huku kukiwa na malalamiko kadhaa ya wananchi.
Wakizungumza kwa pamoja, Wanasiasa hao waliunga mkono kuwepo kwa Muungano, lakini walishauri mfumo mpya wa Muungano wa Mkataba, ili kila nchi kuwa na mamlaka yake kamili:
“Kwa hali ilivyo miaka 50 ya Muungano kushindwa kutatua mambo mbali mbali, mfumo pekee unaofaa kwa sasa na kwa kizazi hiki ni Muungano wa Mkataba. Utaratibu wake utajulikana baadae,” walisema Wanasiasa hao.
Bw Moyo alisema Serikali ya Muungano, isiogope maoni ya wananchi kwani kwa takriban miaka 50 matatizo ya Muungano yameshindwa kutatuliwa na njia pekee kwa sasa ni kukubali kubadilisha mfumo wa Muungano huo:
“Tukiwa na mfumo mpya wa Muungano, utakwenda sambamba na wakati huu ambao idadi kubwa ya wananchi wameamka na kuona kuna matatizo katika Muungano wetu,” alisema Bw Moyo.
Bw Moyo ni Waziri wa kwanza wa Sheria wa Serikali ya Muungano, na Bw Salum Rashid alikuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi.
Kwa pamoja walishauri kuwepo kwa Muungano lakini walisisitiza, ili kuimarisha Muungano kwa nchi zote mbili, ni kusikilizwa kwa maoni ya wananchi ambao wanataka aina mpya ya Muungano wa Mkataba:
“Sisi ndiyo tulikuwa na dhamana wakati ule na tulitakiwa tuunganishe Serikali kwa kuimarisha udugu na kuimarisha uchumi wetu, bahati mbaya sasa kuna kero, mimi siziiti kero naita ni matatizo, ni wakati wake kuondoshwa” alisema na kubainisha:
“Msimamo wangu ni Serikali ya Mkataba na ndiyo ninavyoamini na naamini kwamba huu muungano tuliyonao ni Muungano wa Mkataba, hili siyo jambo jipya, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume walitia saini ya Mkataba,” hili sio jambo jipya,” alisisitiza Mzee Moyo.
Bw Moyo alitaka kurudishwa kwa utaratibu wa zamani, ili Rais wa Zanzibar aendelee kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, akimaanisha Muungano huo ni wa Tanganyika na Zanzibar.
Naye, Katibu Mkuu wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi, Bw Salum Rashid ambaye alikuwa Dar es Saalm na Mzee Karume siku ya kusainiwa Mkataba wa Muungano, alisisitiza kuwepo kwa Muungano wenye maslahi kwa wananchi wa nchi zote mbili:
“Serikali ya Muungano isiwe na woga wa kuvunjika kwa Muungano. Hilo sio jambo kubwa na wala siyo jambo geni, baadhi ya nchi za Afrika ziliwahi kuungana, na Muungano ukavunjika,” alisema na kufafanua zaidi:
“Sioni jambo zito kuvunjika kwa Muungano, mbona Muungano wa Senegal na Gambia ulivunjika na wote walikuwa ni wanachama wa Umoja wa Afrika na hakuna jambo lolote lililotokea,” alisema Bw Salum Rashid.
Alisema wananchi wanaotaka Muungano wa Mkataba, hawamaanishi kuvunja Muungano, bali wanataka mfumo mpya wa Muungano ili kuirudishia Zanzibar, mamlaka na madaraka yake kamili.
Alisema ifahamike kwamba, kuwa nje ya Serikali siyo sababu ya kuwa ni fursa ya kuzungumza hayo, lakini wakati ule likizungumzwa suala la Muungano, ilikuwa inaonekana ni uhaini:
Alisema kwa sasa haiwezekani tena kuburuzwa na hasa vijana. Hivyo matumaini yake kwa tume hiyo ni makubwa: “Naamini watafanya kazi zao kwa uadilifu mkubwa na maoni ya wananchi ambayo wameyatoa kwa Tume, yatatekelezwa,” alisema Bw Salum Rashid.
Alisema Muungano wa Mkataba ndiyo sahihi kwa sasa na hakuna sababa ya viongozi kuogopa hilo, Wazanzibari na hasa vijana wanataka nchi yao kuwa na mamlaka kamili.
Bw Moyo na Bw Rashid wote wawili kwa pamoja wamewatoa hofu Wazanzibari kuhusu utendaji wa Tume hiyo, na walisema wanaiamini kwamba itafanyakazi yake kwa uadilifu, bila upotoshaji.
Tume hiyo inayongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba na Katibu wa Tume, Assa Rashid tayari imeshachukuwa maoni ya baadhi ya viongozi wakuu, pamoja na Marais wastaafu wa Seriakli ya Zanzibar.
Viongozi waliyokwisha toa maoni yao ni pamoja na Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Rais Mstaafu Dk Salmin Amour, Dk Amani Abeid Karume na baadhi viongozi wengine wa Serikali ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment