Thursday, January 17, 2013

Mahakama ya kijeshi ya Somalia yawaua wanajeshi wawili waliokutwa na hatia ya mauaji na ubakaji


Mahakama ya kijeshi nchini Somalia Jumatano (tarehe 16 Januari) iliwaua askari wawili waliokutwa na hatia ya mauaji na ubakaji, uliripoti mtandao wa Hiiraan wa Somalia.
Kwa mujibu wa mahakama hiyo, askari hao Jamal Ahmed Abdikadir mwenye umri wa miaka 23, ambaye alikuwa askari polisi, alimuua mtu mmoja mwaka 2010, na askari mwingine Abdi Osman Magan mwenye umri wa miaka 32 aliyekuwa afisa wa jeshi, alimbaka mwanamke mmoja mwezi Oktoba 2011.
"Uamuzi wa kutekeleza hukumu hizo ulitolewa na mahakama ya kijeshi kwa kutumia sheria za Kiislamu pamoja na sheria nyingine za nchi," alisema Liban Abdi Yarow, mwenyekiti wa mahakama ya kijeshi ya Somalia. "Askari hawa wawili walikiri makosa yao mbele ya mahakama".
Kikosi maalumu kilifanya kazi hiyo ya kuwaua askari hao, huku maafisa wa ngazi za juu katika jeshi la Somalia na mkuu wa vikosi vya polisi vya nchi hiyo wakishuhudia.
Yarow aliwaonya askari wa serikali kutofanya makosa kama hayo na kama wakithubutu watakumbana na hukumu kama hiyo.

No comments:

Post a Comment