Maafisa wa Kenya mjini Mombasa wamenasa zaidi ya vipande 600 vya
pembe za ndovu vyenye uzito wa tani mbili na thamani ya shilingi milioni
87 (dola milioni 1), liliripoti shirika la habari la AFP hapo Jumanne
(tarehe 15 Januari).
Mkuu wa operesheni kwenye bandari Gitau Gitau alisema kwamba hakuna
mtu aliyekamatwa. Alisema kwamba nyaraka zilizotumika kuusafirishia
mzigo huo zitatumika kuwafuatilia wamiliki wake.
Wiki mbili zilizopita, maafisa wa Hong Kong walikamata zaidi ya tani
moja ya pembe za ndovu zenye thamani ya kiasi shilingi milioni 122(dola
milioni 1.4) katika shehena ya meli kutoka Kenya.
Katika siku za karibuni Kenya imeshuhudia kuongezeka kwa matukio ya ujangili. Karibuni majangili waliichinja familia moja ya tembo 11 na kuwangoa mikonga yao katika Mbuga ya Taifa ya Tsavo Mashariki katika kile maafisa wanachosema lilikuwa ni tukio baya kabisa nchini humo ndani ya kipindi cha miongo mitatu.
Mauaji hayo yalimpelekea Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga kuomba msaada wa kimataifa kuisadia Kenya kukabiliana na ongezeko la ukatili wa majangili.
Kwa mujibu wa Shirika la Wanyamapori la Kenya, Kenya ilipoteza kiasi
cha tembo 360 mwaka jana, ikiwa idadi kubwa kuliko wale 289 waliouawa
mwaka 2011.
Biashara ya kimataifa imepigwa marufuku tangu mwaka 1989 isipokuwa
kwenye kesi za nadra sana, baada za idadi ya tembo barani Afrika
kupungua kutoka mamilioni katikati ya karne ya 20 hadi kiasi cha 600,000
mwishoni mwa miaka ya 1980.
No comments:
Post a Comment