Manispaa ya Mogadishu inapanga kufungua kituo chake cha kwanza
kinachoendeshwa na serikali tangu mwaka 1991 baada ya kununua magari
matatu ya kuzimia moto, Meya wa Mogadishu Mohamed Ahmed Nur alitangaza
wiki iliyopita.
Magari hayo ya kuzimia moto yalinunuliwa kwa msaada wa fedha kutoka
jamii ya Wasomali nchini Uingereza, Nur alisema, ingawa hakuainisha
kiwango cha fedha.
Gari moja limeshafika Mogadishu na mawili mengine yako njiani,
alisema, na kuongeza kuwa Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia
(AMISOM) inawapa mafunzo watu 15 wenye umri baina ya miaka 25 na 40 juu
ya mbinu za kupambana na moto.
"Tunawatarajia kufanya mabadiliko makubwa katika ukosefu wa vitendea
kazi vya kupambana na moto mjini Mogadishu baada ya kupata mafunzo
kamili," Nur alisema katika mkutano wa habari hapo tarehe 8 Januari.
"Tutaanzisha nambari za simu kwa umma kuweza kupiga wakati wanapohitaji
huduma za kupambana na moto."
Kwa zaidi ya miongo miwili, bila ya kuwa na kituo rasmi cha kuzima
moto, huduma zilizokuwa zinazomilikiwa na watu binafsi mjini Mogadishu
zimekuwa zikitoa ulinzi kiasi fulani, lakini zimekuwa pungufu sana kwa
kutoshughulikia ipasavyo mahitaji ya mji mkuu ya kupambana na moto.
Mustafa Abdirahman, mwenye umri wa miaka 34 na mfanyabiashara wa
nguo, alisema kuwa ana furaha kubwa kwa kununuliwa kwa magari ya kuzimia
moto katika mkoa wa Benadir. Abdirahman alipoteza kiasi cha dola 10,000
za bidhaa wakati duka lake lilipoharibiwa na moto mwaka jana.
"Nilikuwa na duka kubwa la nguo katika soko la Bakara ambalo
liliharibiwa kabisa wakati moto mkali ulipoanza ndani ya duka langu.
Nilipoteza kila kitu, kwa vile hakukuwa na yeyote aliyejaribu kuuzima
kwa sabau ulianza usiku na hakukua na huduma za kuzima moto," aliiambia
Sabahi.
Mkazi wa Mogadishu Fadumo Nur, mwenye umri wa miaka 42, pia alikuwa
muathirika wa moto wakati moto wa umeme ulipoanza katika duka lake la
vifaa vya elektroniki katika soko la Hamar Weyne mwanzoni mwa mwaka
2012. Nur alisema alibahatika kwa sababu vikosi vya AMISOM vilimsaidia
kuuzima moto huo na vilifanikiwa kuudhibiti.
"Nilipoteza kiasi cha dola 15,000 katika moto huo," aliiambia Sabahi.
"Wamiliki wenzangu wa biashara mjini Mogadishu wanalo tatizo hilo hilo.
Sisi kama wamiliki wa biashara, tunalishukuru baraza la manispaa na
tawala za mikoa kwa juhudi zao za kuleta magari mapya ya kuzimia moto
Mogadishu."
Mohamed Warsame, mwenye umri wa miaka 56, ambaye alikuwa akifanyakazi
katika Manispaa ya Mogadishu miaka ya 1980, alisema kwa Mogadishu
kupata magari ya kuzima moto kunaonesha maendeleo na kujijenga upya
baada ya uharibifu wa miongo miwili iliyopita. Alisema kuwa hii ni hatua
ya mwanzo tu, kwa vile Mogadishu inahitaji zaidi ya magari matatu, kwa
mji wenye watu wanaokadiriwa milioni 3.
"Kwa muda wa miaka 21, watu wengi wa Somalia walipoteza mali zao
wakati biashara zao ziliposhika moto kwa sababu mji haukuwa huduma
zinazofaa za kupambana na moto," Warsame aliiambia Sabahi.
"Mogadishu ilikuwa na kitengo cha kupambana na moto ambacho kilikuwa
katika mkao wa tahadhari usiku na mchana kila siku na kilihudumia sehemu
yoyote ya jiji," alisema. "Natumai kuwa huduma hiii itarejea kama
ilivyokuwa au kuwa bora zaidi."
No comments:
Post a Comment