Katika mkutano ulioitishwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Katoo Ole Metito kwenye Nyumba ya Harambee jijini Nairobi Jumatatu (tarehe 14 Januari), maofisa waandamizi wa usalama, watunga sheria kutoka Tana River Delta, wakereketwa wa kisiasa, wataalamu na wazee wa Jumuiya walijadili njia za kumaliza vurugu hizo.
"Lengo la mkutano lilikuwa kutafuta njia za kuhakikisha kwamba jumuiya zinazoishi katika maeneo yaliyoathirika zinaishi kwa pamoja kwa amani na kuondoa matukio ya mizozo baina ya makabila ambayo yanasababisha kukosa maendeleo na upotevu wa maisha," aliyekuwa mbunge wa Kaskazini ya Tana Omar Soba aliiambia Sabahi.
"Licha ya mikusanyiko ya pamoja baina ya makabila hayo, tumekubali kufanya mikutano ya amani ya pamoja kati ya makabila katika meaeneo yote yenye mizozo ili tuweze kutuliza chuki na hasira zilizopo," alisema.
Alisema viongozi wa jumuiya zote mbili waliapa kusaidia zoezi la kuweka silaha chini la serikali na kuendeleza mazungumzo baina ya makabila.
"Tutakwenda kila nyumba na kuzungumza nao ili wasalimishe silaha zilizo chini ya umiliki wao kinyume cha sheria ambazo tunazitumia kujiua wenyewe," Soba alisema.
Usalama kumaliza, hotuba za chuki
Wakati mkutano unaendelea Nairobi, wanaharakati wa haki za binadamu wa Waislamu kwa Haki za Binadamu (MUHURI) walifanya maandamano mtaani huko Mombasa wakilaani mauaji na kupinga wanachokisema kilikuwa hatua za taratibu za serikali katika kuzuia vurugu.Mkurugenzi mtendaji wa MUHURI Hussein Khalid alitoa wito wa uchunguzi wa jumla wa timu ya ulinzi katika Tana River Delta.
"Kushindwa kwa polisi kuzuia vifo hivyo kwa miezi kadhaa sasa ni kiashirio cha wazi kwamba kuna uhaba mkubwa wa ulinzi," aliiambia Sabahi. "Tunahitaji mabadiliko kuweka mbinu mpya ambazo zitashughulikia vurugu hizi iwe mwanzo na mwisho."
Isipokuwa kama kuna uchunguzi wa jumla wa usalama, vurugu zinaweza kuwa mbaya na kusababisha hali mbaya maeneo mengine yenye vurugu kama vile Mlima Elgon, Eldoret, Nakuru na wilaya za kaskazini mwa Kenya, Khalid alisema.
"Kama hawawezi kushughulikia vurugu katika eneo dogo kama Tana River Delta, nini kitatokea katika maeneo mengine ya Jimbo la Pwani, ambalo tayari linakabiliwa na vitisho vya vikundi haramu kama Mombasa Republican Council?" aliuliza. "Na nini kitatokea kwa nchi nzima ambako tunaona vurugu zinazohusiana na uchaguzi zikiongezeka?"
Metito pia alizungumzia tatizo hili wakati wa mkutano huko Nairobi. Aliwaasa wanasiasa dhidi ya kutumia lugha ya chuki katika kampeni zao na kuwahamasisha wafuasi wao kuleta vurugu.
"Uchunguzi uko katika hatua za mwisho na mtu yeyote, awe mwanasiasa au vinginevyo, atakayepatikana kuhusika na vurugu ama katika Tana Delta au sehemu nyingine za nchi atakamatwa na kushitakiwa," alisema. "Hatutaki watu wachache kuiingiza nchi katika matatizo tena."
Siasa, silaha za moto na migogoro ya ardhi
Benji Ndolo, mchambuzi wa sera katika Kituo cha Sheria na Utafiti wa Kimataifa huko Nairobi, alisema kwamba pamoja na maendeleo makubwa ya watumishi wa usalama katika eneo, mlipuko wa kuingiliana kwa makabila vimeendelea kwa sababu ya uwezo duni wa mbinu za polisi na kushindwa kuzishirikisha jamii kikamilifu ili kuleta makubaliano ya kusimamisha vita."Ninadhani kuwashirikisha viongozi wa jamii kwanza ni hatua sahihi kuondoa vurugu, lakini inapaswa kuimarishwa kwa kuunganisha intelijensia inayofaa ili kwamba wote wanaohusika na mauaji waweze kukamatwa -- na wale wanaopanga mashambulizi zaidi waweze kuwekewa vizuizi kabla hawajafanya mashambulizi hayo," aliiambia Sabahi.
Ndolo alisema, siasa, ueneaji wa silaha haramu na kugombea ardhi kwa ajili ya malisho ya wanyama vinachochea ugomvi kati ya wakulima wa Pokomo na Ormas, ambao ni wafugaji hasa. Kama suluhisho la muda mrefu, aliiomba serikali kutoa uamuzi wa haki kuhusu ardhi katika eneo hilo.
Soba alikubali kwamba migogoro ya ardhi inasababisha na vurugu katika eneo, lakini alisema anaamini kwamba hukumu za haraka zinazohusu kesi za umiliki wa ardhi zitawapa wananchi haki za ardhi wanazoitafuta na kuleta amani ya kudumu.
Inspekta Jenerali wa polisi David Kimaiyo, ambaye pia alihudhuria katika mkutano huko Nairobi siku ya Jumatatu, alikanusha madai kwamba polisi hawaweze kushughulikia vurugu. Alisema majeshi ya usalama yamebadilisha mbinu zao za kushughulikia vurugu zinazochochewa kikabila na kisiasa.
"Tumeimarisha [uondoaji wa] silaha haramu za moto kutoka katika mikono ya wananchi, sio tu katika Tana River Delta bali katika nchi nzima," alisema, japokuwa alikataa kutoa maelezo ya kina kuhusu operesheni ya uwekaji chini silaha.
"Mambo sio kwamba yako nje ya udhibiti," alisema. "Jinsi tunavyozungumza sasa, tumepata hali halisi ya huko Tana River Delta na maeneo yenye vurugu za kisiasa nchini, kuzuia aina yoyote ya vurugu katika harakati za uchaguzi mkuu ujao na hata baada ya uchaguzi."
No comments:
Post a Comment